Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) limesikitishwa na taarifa zilizosambaa katika mitandao
kuanzia jana zikiwahusisha viongozi wa timu moja ya daraja la kwanza na
baadhi ya watumishi wa TFF.
Pamoja na kwamba taarifa hizo
zilizosambazwa hazihusiani na kesi ya kupanga matokeo iliyoamuliwa siku
ya tarehe 03/04/2016, TFF inachunguza kubaini uhalisia (authenticity) wa
taarifa hizo na itachukua hatua kali sana kwa watumishi wa shirikisho
na viongozi wa timu husika watakaobainika kushiriki vitendo vilivyo
kinyume na maadili ya mpira wa miguu.
TFF imekwishaweka bayana nia ya
kupambana na yeyote atakayehusika katika upangaji matokeo na uhalifu
mwingine unaoharibu ustaarabu wa mpira kwa njia yoyote ile.
Pia Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) linatoa onyo kwa baadhi ya viongozi, watumishi wa TFF na
wadau wa mpira wa miguu kwa ujumla wanaotumia majina ya viongozi wa juu
wa TFF katika kufanikisha mipango yao kwa manufaa binafsi.
TFF inawaomba wapenda mpira wa miguu kuwa watulivu na waangalifu wakati suala hili linashughulikiwa.
Aidha, kuhusu hukumu ya Kamati ya
Nidhamu ya TFF ni muhimu ikaeleweka wazi kwamba zipo taratibu za kukata
rufaa kwa mujibu wa kanuni ili upande usioridhika na maamuzi
yanayotolewa uweze kuhoji maamuzi husika.
Ni vema tukaacha kamati huru
zifanye kazi zake kwa mujibu wa taratibu. Kutoa hukumu mtaani au kwenye
vyombo vya habari kunaweza kuwanyima haki wanaostahili na kutengeneza
kichaka cha kujificha watenda maovu.






0 maoni:
Chapisha Maoni