JESHI LA ULINZI LA WANANCHI WA TANZANIA
KURUGENZI YA HABARI NA UHUSIANO
Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa
Tanzania limeshitushwa na kusikitishwa kwa taarifa zinazo lituhumu JWTZ
kuhusu unyanyasaji wa kijinsia unaodaiwa kufanywa na Wanajeshi wetu kwa
Wananchi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
JWTZ chini ya Umoja wa Mataifa
(MUNUSCO) limekuwa likitekeleza majukumu ya Ulinzi wa amani katika
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo takribani miaka mitatu sasa.Katika muda
ambao JWTZ limekuwa nchini Congo hapakuwepo na tuhuma kama hizo.
Aidha, JWTZ limetekeleza na
limeendelea kutekeleza majukumu kama hayo katika nchi mbalimbali duniani
kama vile Msumbiji, Liberia, Visiwa vya Comoro (Anjouan), Lebanon,
Sudan katika jimbo la Darfur na sehemu nyingi kama hizo.Katika
kutekeleza majukumu hayo JWTZ limeyatekeleza kwa nidhamu na weledi wa
hali ya juu.JWTZ limekuwa moja ya majeshi mengi yanayofanya vizuri na
kutoa mchango mkubwa katika Ulinzi wa amani katika nchi ambazo
limetekeleza majukumu hayo.
Hivi karibuni kumezuka tuhuma
nchini Congo kuhusu Wanajeshi wa JWTZ kuwanyayasa kijinsia wananchi wa
Congo. Kimsingi JWTZ haliwezi kupuuzia taarifa hizo, hivyo limeanza
kuchukuwa hatua za kiuchunguzi ili kubaini ukweli wa tuhuma hizo ingawa
rekodi za majukumu ya ulinzi wa amani zilizokwisha fanywa na JWTZ sehemu
mbalimbali zinaonesha kuwa hakukuwa na tuhuma kama hizo.
Kufuatia tuhuma hizo, JWTZ kwa
kushirikiana na Umoja wa Mataifa unafanya uchunguzi wa kina ili
kujiridhisha na ukweli wake. JWTZ halitasita kuchukua hatua kali kwa
watakaobainika katika tuhuma hizo. JWTZ bado lipo imara na linaendelea
kutekeleza majukumu yake nchini Congo kwa kufuata sheria na taratibu za
Umoja wa Mataifa.
Imetolewa na Kurugenzi ya Habari na Uhusiano
Makao Makuu ya Jeshi, Upanga






0 maoni:
Chapisha Maoni