![]() | |
|
KATIBU
Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Seif Sharif Hamad amesema uamuzi wa
chama chake kususia uchaguzi wa marudio uliafikiwa na Baraza Kuu la
Uongozi na hauna uhusiano na taarifa kwamba amenunuliwa na Chama Cha
Mapinduzi pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Aidha
Seif amelazimika kutolea ufafanuzi ukarimu aliofanyiwa na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar kumlipia safari ya matibabu kwenda India; Serikali
ya Jamhuri ya Muungano kulipa gharama za kuwepo katika Hoteli ya Serena
na kutembelewa na viongozi wa ngazi za juu akisema, havina uhusiano na
kurubuniwa.
Katika
kile kinachoonekana ni ‘kuwaangukia’ wanachama wake kupitia mkutano wa
waandishi wa habari aliofanya jana mjini hapa, Seif alisema huo ni
ukarimu na utamaduni wa viongozi unaotokana na ubinadamu .
Alisema
uamuzi wa kujitoa katika uchaguzi wa marudio wa Machi 20 ulitokana na
chama hicho kutokubaliana na uamuzi uliofikiwa na Tume ya Uchaguzi ya
Zanzibar (ZEC) kwa sababu uchaguzi huo ulikidhi mahitaji na matarajio ya
wananchi CUF iwe madarakani.
Kwa
mujibu wa mwanasiasa huyo aliyekuwa mgombea wa urais wa Zanzibar kupitia
CUF, zipo taarifa kutoka kwa baadhi ya watu wanaodai kwamba alijitoa
kwenye uchaguzi huo wa marudio baada ya kurubuniwa na CCM ili ipate
ushindi mkubwa.
“Taarifa
hizo hazina harufu ya ukweli,” alisema. “Kilichofanywa na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar kugharimia safari yangu ya kwenda India matibabuni
pamoja na kutembelewa na viongozi wa ngazi za juu akiwemo Rais John
Magufuli , kwanza ni wajibu wa serikali kwa sababu mimi ni Makamo wa
Kwanza wa Rais mstaafu….lakini huo ndio ukarimu na uhusiano wetu
Watanzania unaotokana na ubinadamu,” alisema.
Alisema
msimamo wa CUF kutoitambua Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya Rais
Dk Ali Mohamed Shein, upo pale pale kwa sababu chama hicho kinaamini
kilishinda katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 kwa kupata majimbo ya
uchaguzi ya Unguja na Pemba.
“Chama
cha CUF hakijabadili msimamo wa kutoitambua Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar chini ya Rais Dk Ali Mohamed Shein kwani sisi tunaamini kwamba
tulishinda katika uchaguzi wa Oktoba 25 kwa kupata ridhaa ya wananchi
walio wengi ambao walikipigia kura chama chetu na kupata ushindi wa
majimbo yaliyopo Unguja na Pemba,” alisema.
Juzi
wakati Rais wa Zanzibar akizungumza na waandishi wa habari na kutangaza
Baraza la Mawaziri, Ikulu, alisema ushindi wake unatambuliwa na wananchi
walio wengi ambao ndiyo walioipa ridhaa CCM na kushika hatamu ya
kuongoza dola kwa asilimia 91.4.







0 maoni:
Chapisha Maoni