![]() | |
|
RAIS Paul
Kagame wa Rwanda amempongeza na kumsifia Rais John Magufuli kutokana na
mfumo wa uongozi wake hasa nia yake thabiti ya kupambana na ufisadi.
Kagame
aliyasema hayo juzi katika hafla ya chakula cha jioni aliyoiandaa kwa
ajili ya mgeni wake, Rais Magufuli aliyepo nchini humo kwa ziara ya
kikazi ya siku mbili katika taifa hilo .
“Kwanza
nataka ujue kuwa hapa ni nyumbani kwa kaka yako. Tangu uchaguliwe kuwa
Rais, uwepo wako umekuwa wa kipekee, matendo na maneno yako yanaakisi
maono yetu,” alisema Rais Kagame.
Aidha, alisema jitihada na msimamo wa Dk Magufuli katika kupambana na tatizo la rushwa na ufisadi ni wa kupongezwa na kuigwa.
Akiwasili
nchini humo juzi, Dk Magufuli alisafiri umbali wa takribani kilometa
1,460 kwa barabara, ikiwa ni ziara yake ya kwanza ya kikazi nje ya
Tanzania tangu achaguliwe kushika wadhifa huo Oktoba mwaka jana.
Msafara
wa Rais huyo ulipokewa kwa shangwe na wananchi wa Rwanda wakati ukipita
kwenye mji wa Rusumo kwenda mpakani mwa nchi ya Rwanda na Tanzania.
Baada ya
kuwasili Rusumo ambako ni mpaka wa Tanzania na Rwanda katika wilaya ya
Ngara kwa Tanzania, Dk Magufuli na mwenyeji wake walifungua majengo ya
Kituo cha Pamoja cha Utoaji wa Huduma za Mpak ani kilichopo upande wa
Tanzania, kisha wakafungua daraja la mto Kagera.
Dk
Magufuli akiwa na mkewe Mama Janeth Magufuli jana waliungana na wananchi
wa Rwanda kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 22 tangu kutokea kwa mauaji
ya kimbari yaliyosababisha vifo vya watu takribani milioni moja.
Maadhimisho
hayo yamefanyika katika eneo la Gisozi mjini Kigali yalipo makumbusho
ya mauaji ya Kimbari ambako Rais Magufuli na mkewe wakiwa na mwenyeji
wao Rais Paul Kagame na mkewe Mama Janeth Kagame waliweka shada la mau
katika eneo walipouawa idadi kubwa ya wananchi wa Rwanda na pia
wakawasha mwenge wa matumaini kwa walionusurika katika mauaji hayo na
kwa Taifa zima la Rwanda.
Pamoja na
kupata historia ya mauaji hayo ya kimbari, Rais Magufuli akiongozwa na
mwenyeji wake alitembelea jumba maalumu lililohifadhi kumbukumbu ya watu
waliopoteza maisha, ambako alipata maelezo kutoka kwa wahifadhi wa
makumbusho hiyo, na pia kujionea picha na mabaki ya mifupa na mafuvu ya
binadamu waliouawa.
Akizungumza
baada ya kutembelea jumba hilo la makumbusho, Rais Magufuli alielezea
kusikitishwa kwake na mauaji hayo na kusema tukio hilo halipaswi
kurudia.
“Haitatokea
tena, hatuwezi kubadilisha yaliyopita lakini tunaweza kubadilisha mambo
ya sasa na yajayo, mauaji haya hayapaswi kutokea tena,” alisema Rais
Magufuli.
Rais
Magufuli ambaye aliingia nchini Rwanda juzi ikiwa ni ziara yake ya
kwanza nje ya nchi tangu aingie madarakani Novemba 5, mwaka jana,
aliondoka Kigali jana jioni na kurejea jijini Dar es Salaam.







0 maoni:
Chapisha Maoni