MKUU wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza
amezindua vituo viwili vya huduma za afya na upimaji virusi vya Ukimwi (VVU) kwa hiari vilivyojengwa
kandokando ya barabara kuu ya Iringa Dar es Salaam, mkoani Iringa vikilenga kutoa
huduma hizo kwa madereva wa masafa marefu.
Vituo hivyo ambavyo pia vitatoa huduma
kwa wananchi wanaovizunguka, vimejengwa katika mji mdogo wa Ilula, wilayani
Kilolo na kijiji cha Wenda, Iringa Vijijini kwa msaada wa wadau wa sekta ya
usafirishaji nchini watakaogharamia uendeshaji wake hadi mwaka 2018.
Meneja wa kampuni ya Impala Terminals
Tanzania ambayo ni sehemu ya wadau hao, Jorge Rico Grillo alisema kampuni yao
kwa kushirikiana na mashirika ya Puma
Energy Foundation na Trafigura walitoa fedha kwa shirika la kimataifa linalojishughulisha
na afya la North Star Alliance na kujenga vituo hivyo.
Grillo alisema pamoja na vituo hivyo
viwili, wadau hao wamejenga vituo vingine vinne katika mikoa ya Dar es Salaam
na Mbeya vilivyozinduliwa kwa nyakati tofauti wiki iliyopita.
Alisema lengo lao ni kuona madereva
wanaotumia barabara hiyo inayokwenda hadi nchi za Malawi na Zambia wanakuwa
katika mazingira rafiki yatakayowawezesha kupata ushauri na huduma mbalimbali
za afya wakiwa safarini.
Mwakilishi wa shirika la North Star Alliance,
John Mwachama alisema kwa kupitia vituo hivyo madereva watapata elimu ya afya, madhara
ya dawa za kulevya na pombe pamoja na huduma bure ya upimaji na matibabu wa
magonjwa mbalimbali ikiwemo VVU, kisukari na mengineyo jambo litakalowawezesha
kuchukua tahadhari kabla na wakati wakitumia barabara hiyo.
Meneja Uendeshaji wa Puma Energy
Tanzania, Lameck Hiliyai alisema kujengwa kwa vituo hivyo kutasaidia makampuni
ya usafirishaji kuwatumia madereva wanaojali afya zao.
Mwakilishi wa kampuni za usafirishaji,
Arif Abri wa kampuni ya FM Transporter alisema hakuna udereva salama kama
madereva hawatakuwa na tabia ya kujua hali za afya zao.
Abri alisema dereva akijua afya yake
itamuwezesha kufanya maamuzi ya busara yanayoweza kusaidia mikakati mbalimbali
ya serikali ya kupunguza hasara na vifo vinavyotokana na ajali.
Akizindua vituo hivyo, Mkuu wa Mkoa wa
Iringa alisema vituo hivyo vitakuwa vya manufaa sana kwa madereva na wananchi
walio jirani navyo kwani vinaongeza upatikanaji wa huduma zinazotolewa pia
katika vituo vingine binafsi na vya serikali.






0 maoni:
Chapisha Maoni