SHULE ya Msingi Ipogolo ya mjini Iringa
imepata msaada wa madawati 50 yenye thamani ya zaidi ya Sh Milioni 3
yaliyotolewa na kituo cha tiba asilia na tiba mbadala cha Lupimo Sanitarium
Clinic chenye tawi lake mjini hapa.
Mkuu wa shule hiyo yenye changamoto
lukuki, Amani Mkeremy alisema watoto wengi wa shule hiyo yenye wanafunzi 1,328
wanakaa chini kwa kuwa tatizo la madawati ni kubwa linalohitaji kutatuliwa kwa
misaada ya wadau mbalimbali wa sekta ya elimu.
Akishukuru kwa msaada huo aliosema
utsaidia kupunguza tatizo hilo, Mkeremy alisema wakati mahitaji ya shule ni
madawati 664, yaliyopo ni 300 tu jambo linalofanya mazingira ya kufundishia
wanafunzi hao shuleni hapo yawe magumu.
Akikabidhi msaada huo kwa Mkuu wa Mkoa wa
Iringa Amina Masenza juzi, Mkurugenzi wa Lupimo Sanitarium Clinic Dk John
Lupimo alisema; “tumemtoa msaada huu ikiwa ni mkakati wetu wa kurudisha kwa
jamii sehemu ya kile tunachopata kutoka kwao.”
Lupimo alisema mpango wa serikali ya Dk
John Magufuli wa kutoa elimu bure kwa wanafunzi wa shule za msingi hadi
sekondari utakuwa wa mafanikio makubwa katika maendeleo ya sekta ya elimu endapo
wadau wake watashiriki kuzimaliza changamoto mbalimbali zinazoikabili.
Akipokea msaada huo kwa niaba ya shule
hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa alishtushwa kusikia shule hiyo mbali na kuwa na
upungufu mkubwa wa madawati lakini pia ina upungufu wa vyumba 18 vya madarasa
na matundu 28 ya choo.
Alipokuwa akiwasilisha taarifa yake kwa
mkuu wa mkoa, mkuu wa shule hiyo alisema; “ shule hii iliyoanzishwa mwaka 1972
ina vyumba vya madarasa 18 tu wakati mahitaji ni vyumba 35 na ina matundu ya
vyoo 32 wakati mahitaji ni matundu 60 kwa ajili ya wavulana na wasichana.”
Akioneshwa kukerwa na taarifa hiyo inayodhihirisha
wanafunzi hao kusoma katika mazingira magumu, Mkuu wa Mkoa Masenza alisema
atalazimika kumfuta kazi afisa mtendaji wa kata ya Ipogolo (Ruaha),Bahati Mlafi
endapo itabainika katika mpango wake wa maendeleo hakuna mkakati wa kumaliza
tatizo hilo.
Akijitetea Mlafi alisema wabao mpango wa
kuboresha mazingira ya shule hiyo yanayohusisha kuihamisha kutoka katika eneo
ilipo kwasababu ya udogo wake ili wapate eneo kubwa litakalokidhi mahitaji.
Akimshukuru Dk Lupimo kwa msaada huo
alisema; “lazima kila shule iwe na sheria itakayowalazimisha wazazi kulipa
madawati yanayoharibiwa kwa makusudi na wanafunzi.”
Akizungumzia upungufu wa madawati mjini
Iringa, Masenza alisema kuna upungufu wa madawati 3000 kwa shule za msingi na
334 kwa shule za sekondari.
Awali Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela alisema; “Changamoto ya madawati katika shule mbalimbali za wilaya hiyo ni kubwa lakini pamoja na ukubwa wake tunapambana nayo ili kabla ya April 30 kila shule iwe na madawati yanayohitajika.”






0 maoni:
Chapisha Maoni