Kushoto ni mmiliki wa ukumbi wa
ZANCINEMA Mohammed Bajbeir, akiwa pamoja na Andy Jones, raia wa
Uingereza, mtengenezaji wa filamu za ‘As Old sa My Tongue’ na ‘I shot
Bi. Kidude’, zinazoonesha historia ya maisha hadi kufa kwa msanii
mkongwe marehemu Fatma Baraka ‘Bi. Kidude’, wakizungumza na waandishi wa
habari juu ya kumbukumbu ya msanii huyo aliyefariki dunia Aprili 17,
2013. (Picha na Yussuf Simai-MAELEZO, ZANZIBAR.
……………………………………………………………………………………………..
Na Salum Vuai, MAELEZO
KATIKA kuadhimisha kumbukumbu ya
mwaka wa tatu tangu kufariki kwa msanii mkongwe aliyeitangaza sana
Zanzibar duniani Fatma Baraka ‘Bi. Kidude’, filamu mbili zinazohusu
maisha na kifo chake zitaoneshwa mjini Zanzibar.
Mohammed Bajbeir, mmiliki na
Mkurugenzi wa ukumbi wa sinema uliopo mjini Zanzibar, ZANCINEMA,
amewaambia waandishi wa habari jana, kwamba maonesho ya filamu hizo
yanalenga kuwapa fursa Wazanzibari na wageni, kumjua kwa undani nyakanga
huyo wa sanaa ya uimbaji na unyago.
Marehemu Bi. Kidude, alifariki
dunia Aprili 17, 2013 baada ya kuugua maradhi ya kisukari yaliyochangiwa
na umri mkubwa, na kuzikwa kijijini kwao Kwambani katika mazishi
yaliyoweka rekodi miongoni mwa wasanii kwa kuhudhuriwa na watu wengi
wakiwemo viongozi mbalimbali wa ngazi za juu wa Zanzibar na Tanzania kwa
jumla.
Bajbeir amezitaja filamu hizo
kuwa ni ‘As old as my tongue’ inayoelezea kwa urefu maisha ya msanii
huyo katika tasnia ya muziki, pamoja na ‘I shot Bi. Kidude’ (Kifo cha
Bi. Kidude), ambayo inaelezea kuumwa kwake hadi pumzi zake za mwisho.
Filamu hizo zimeandaliwa na
kutengenezwa na Andy Jones, raia wa Uingereza, ambaye alikuwa akimsoma
na kumfuatilia marehemu Bi, Kidude kwa miaka kadhaa hadi akamudu
kuandika filamu hizo zinazogusa mtima wa kila anayeziangalia.
Akizungumza na waandishi wa
habari jana katika ukumbi wa ZANCINEMA ulioko Funguni mjini Zanzibar
kuelekea siku ya kumbukumbu ya Bi, Kidude, Jones alisema Wazanzibari
wana kila sababu ya kumuenzi gwiji huyo wa sanaa ambaye amefanya kazi
kubwa kuitangaza nchi yake ulimweguni, kisanii na kiutamaduni.
Aidha, alieleza kwamba, kwa namna
Bi. Kidude alivyokuwa mtu wa watu wa kila rika, mcheshi, na mwenye
imani asiyeangalia kipato, anastahili kukumbukwa kwa namna ya pekee.
“Wapo watu wa mataifa ya nje
ambao hawakuwa wakimfahamu, lakini waliposikia kazi zake, walisafiri
hadi Zanzibar kwa ajili ya kumjua na kumshuhudia jukwaani akionesha
uwezo wake,” alisema Muingereza huyo.
Alifahamisha kuwa tayari filamu
hizo zimeshaoneshwa katika nchi mbalimbali duniani, lakini maonesho ya
Zanzibar yatakuwa ya kipekee.
Aidha, alisema zimewahi kuoneshwa
katika matamasha ya Zanzibar, Sauti za Busara na lile la filamu (ZIFF),
ambapo watu wengi walivutiwa nazo.
Andy Jones, alifika Zanzibar kwa
mara ya kwanza mwaka 2000, na kuendelea kuja kila mwaka hadi 2006
alipokamilisha filamu ya kwanza, ‘As old as my tongue’ kuhusu historia
ya Bi. Kidude.
Alieleza kuwa, alitumia pauni
15,000 za Kiingereza (sawa n ash. 51,000,000 kwa thamani ya sasa),
kutengeneza filamu ya ‘Kifo cha Bi. Kidude’ (I shot Bi, Kidude),
iliyochukua miaka miwili na nusu hadi kukamilika.
Jones alisema, wakati wa uhai
wake, marehemu Bi, Kidude alikuwa akilipwa asilimia kumi ya mauzo kila
ilipouzwa, na sasa fedha hizo ameamua kuzigawa kwa Akademi ya Muziki wa
Nchi za Jahazi (DCMA) ya Zanzibar kwa ajili ya kuwaendeleza wasanii wa
kike wanaochipukia.
0 maoni:
Chapisha Maoni