Mbunge
wa Jimbo la Singida Kaskazini (CCM), Lazaro Samwel Nyalandu amewahimiza
madiwani kuwandaa wananchi mapema kwa ajili ya kupokea na kutumia
vizuri shilingi Milioni 50 za Rais Magufuli ili ziweze kuwasaidia
kuboresha hali zao za kiuchumi.
Nyalandu ametoa wito huo jana wakati akizungumza mbele ya wajumbe wa kamati ya huduma za jamii halmashauri ya wilaya ya Singida.
Alisema
mkoa wa Singida umepata bahati ya kuwa miongoni mwa mikoa 10 nchini,
ambayo itakuwa ya awamu ya kwanza kunufaika na fedha hizo ambazo ni
ahadi ya rais aliyoitoa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita.
“Kwa
bahati hii sisi wawakilishi wa wananchi tunapaswa kuimba wimbo moja nao
ni kuwandaa wananchi wetu mapema ili waweze kuchangamkia fursa hii
ambayo itawasaidia kujiongezea kipato kitakachowasaidia kuishi maisha
bora,” alisema Nyalandu ambaye ameongoza jimbo hilo kwa vipindi vinne.
Akisisitiza,
alisema kuwa wananchi wanapaswa kuelimishwa pia kuwa fedha hizo ni za
mzunguko, mwananchi akikopeshwa analazimika kuzirejesha kwa wakati ili
mwananchi mwingine naye aweze kunufaika kwa fedha hizo na kudai kwamba
hizo fedha zinalenga kuwanufaisha wananchi wote wa kijiji husika.
Aidha,
Nyalandu alisema kuwandaa huko kuende sambasamba na kuwasaidia
kuanzisha vikundi ujasiriamali na kuvisajili vile vile kuwasaidia kubuni
miradi yenye tija itakayowasaidia kurejesha fedha na kupata faida ya
kukidhi mahitaji.
“Nimelileta
hili mbele yenu mapema ili sote tuweze kujipanga vizuri na mwisho wa
siku,jimbo letu liwe mfano wa kuigwa na majimbo mengine mkoani kwetu na
hata ya nje ya mkoa kwa matumizi sahihi na mazuri ya fedha za rais
Magufuli,” alisema Nyalandu.
Wakati
huo huo, mbunge huyo alisema kuwa fedha za mfuko wake wa jimbo zote
amezielekeza katika ununuzi wa madawati ya shule za msingi na sekondari.






0 maoni:
Chapisha Maoni