Jumanne, 19 Aprili 2016

WANAFUNZI 65 WA SHULE YA SEKONDARI CHALINZE WANUSURIKA KIFO BAADA YA BWENI LAO KUTEKETEA KWA MOTO

images (1) VICTOR MASANGU, BAGAMOYO
WANAFUNZI  65 wa shule ya sekondari chalinze iliyopo Wilayani Bagamoyo mkoani Pwani wamenusurika kupoteza maisha baada ya bweni moja la kulalia  kuteketea kabisa  kwa moto wakati wao wakiwa darasani kwa ajili ya kujisomea masomo ya usiku.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Majid Mwanga kuhusina na tukio hilo alisema kwamba limetokea jana majira ya saa 3:20 usiku wakati wanafunzi hao wakiwa madarasani wanajisomea.
 
Mkuu huyo alibainisha kwamba chanzo cha moto huo inadaiwa ni shoti ya umeme ambayo imesababisha moto huo kuteketeza vifaa vyote vikiwemo magodoro,vitanda,vitabu  vilivyokuwemo katika bweni hilo ambalo lilikuwa likilaliwa na wanafunzi wapatao 65 wa kiume.
“Taarifa za awali ambazo tumezipata chanzo cha kuungua kwa jengo hili ni umeme, lakini kwa kweli ni tukio la kusikitisha kwani vifaa vyote na mali za wanafunzi hao 65 ikiwemo magodoro,vitanda, madatfari yao yote yameteketea kwa moto huo,”alisema Mwanga.
Aidha Mwanga akizungumzia kuhusina na juhudi za serikali ambazo tayari wameshazichukua hadi sasa ikiwemo  kuwahifadhi wanafunzi hao  65 katika jengo lingine kwa  muda wakati wanaendelea na jitihada zingine za kuangalia ni namna gani ya kulijenga jengo linguine kwa haraka.
Alisema kuwa kwa sasa kutokana na tukio hilo la kuungua kwa shule hiyo amewaomba wadau mbali mbali wa maendeleo kujitoa kwa hali na mali kutoa michango yao kwa ajili ya kuwezesha ujenzi mwingine wa jengo hilo ikiwemo na mahitaji ya msingi wanayostaili kusaidiwa wanafunzi hao waliounguliwa na mali zao.
Katika hatua nyingine alisema  kwamba baada ya moto huo kutokea hakukuwa na msaada wowote wa gari ya zima moto hivyo kuliweza kuchangia kwa kiasi kikubwa kuendelea kushika kasi ya moto na kuteketeza vitu vyote katika jengo hilo, ambapo jitihada za kuuzima zilifanywa na jeshi la posili viongozi wa serikali pamoja na wananchi wenyewe.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa mamlaka ya mji mdogo Chalinze Hussein Mramba amekiri kutokea kwa tukio hilo ambapo alisema kwamba mkakati waliyojiwekea ni kushirikiana na wadau wa maendeleo ili kuweza kuhakikisha kwamba wanajenga jengo linguine ili wanafunzi waweze kupata sehemu ya kulala.
 SHULE hiyo ya sekondari Chalinze iliyopo wiayani bagamoyo Mkoa wa Pwani ina jumla ya idadi ya  wanafunzi 1151.ambapo kati yao 65 kwa sasa wameunguliwa na vitu vyao vyote hivyo kunahitajika juhudi za serikali katika kuhakikisha wanatoa msaada wa hali na mali ili waweze kuendelea  masomo yao.
 
 

0 maoni:

Chapisha Maoni