Na Masanja Mabula –Pemba
MADIWANI wa wadi kumi
zinazounda Baraza la Mji Wete Kisiwani Pemba , wamekula kiapo cha utii
na kuahidi kushirikiana na Uongozi wa Baraza hilo katika kupambana
na wafanyabiashara wanaokwepa kulipa kodi .
Wakizungunza na mwananchi baada
ya kiapo hicho kilichosimamiwa na Hakimu wa Mahakama ya Mkoa wa
Kaskazini Pemba , Isihaka Ali Khamis , waliapa kuziba mianya yote
inayotumiwa na wafanyabiashara kuikosesha mapato Serikali .
Walisema kwamba katika utendaji
wao wa kazi hawatamuonea mtu kwa sababu za kisiasa , bali
watahakikisha kila anayehusika na ulipaji kodi anatimiza wajibu wake
kisheria.
Ali Shariff Omar Diwani wa Wadi
ya Bopwe alisema , anafahamu mbinu zinazotumiwa na baadhi ya
wafanyabiashara kuingia bidhaa kienyeji na kuwataka wafanyabiashara hao
kujisalimisha kwani hawatakuwa tena na fursa hiyo .
“Nawaomba wafanyabiashara
watubu na wajisalmishe mapema , kwani mbinu na mianya wanayoitumia
kukwepa kodi zinajulikana , kwa hili hakuna huruma na hataonewa mtu kwa
misingi ya kisiasa ”alieleza .
Kwa upande wake Diwani wa wadi
ya Piki Asha Khamis Nassor alisema mbali na kudhibiti mianya ya wakwepa
kodi , pia aliahidi kuimarisha vikundi vya ushirika ambavyo vimekuwa
vikizalisha ajira kwa vijana hususani wanawake .
Alisema katika kuviimarisha
vikundi hivyo , hakutakuwa na ubaguzi wa vyama vya siasa huku akiwaomba
wanawake wenzake kuumuunga mkono ili aweze kufanikisha malengo
aliyoyakusudia .
“Nimekuja na muono wa mbali wa
kuviimarisha vikundi vya ushirika katika wadi yangu , hii itasaidia
kuongeza ajira kwa vijana hususani wanawake , kwa hili naomba
ushirikiano wao ”alisema .
Mapema katika nasaha zake kwa
Madiwani Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Om,ar Khamis Othman aliwataka
kutekeleza majukumu yao ya kazi kwa kuwatumikia wananchi wote bila ya
kuwabagua kwa misingi ya vyama vyao hasa kwa kuzingatia sheria za
tawala za mikoa namba 4 /2014.
Katika hotuba iliyosomwa kwa
niaba yake na Katibu Tawala Mkoa huo Yussuf Mohammed Ali aliwasisitiza
madiwani hao kutobweteka na ushindi pamoja na dhamana zao mpya , bali
wajipange kusimamia kazi kwa kushirikiana nawatendaji wa baraza la mji .
“Wacheni kubweteka na ushindi
ulioupata pamoja na dhamana zenu hizi mpya , bali jipangeni kusimamia
majukumu yenu kwa kushirikiana na watendaji wa Baraza la Mji
”alifahamisha Tawala .
Mapema Mkurugenzi wa Baraza la Mji Wete Mgeni Othman Juma
aliwataka madiwani hao kuwa waadilifu katika kusimamia mapato ya baraza
ili fedha zinazokusanywa ziweze kutumika katika miradi ya maendeleo ya
wananchi .
Madiwani hao kutoka chama Cha
Mapinduzi (CCM ) walichaguliwa kushika nafasi hizo katika uchaguzi Mkuu
uliofanyika machi 20 mwaka huu , uchaguzi ambao ulisusiwa na Chama
Cha Wananchi (CUF) ambacho ndiyo chama kikuu cha Upinzani Zanzibar .
0 maoni:
Chapisha Maoni