(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
…………………………………………………………………………………………………….
MKE wa Waziri Mkuu, Mary Majaliwa
amefanya ziara katika Hospitali ya wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi na
kutoa msaada wa mashuka kwa akinamama waliojifungua.
Pia ametumia fursa hiyo
kuwapongeza madaktari na wauguzi wa Hospitali ya wilaya ya Ruangwa
kutokana na kuwahudumia vizuri wananchi na kuwaomba waendelee kufanya
kazi hiyo kwa mujibu wa maadili ya kazi yao.
Mke wa Waziri Mkuu ameyasema hayo
jana wakati alipotembelea wodi ya akinamama waliotoka kujifungua na
kufurahishwa na hali ya utoaji huduma hospitalini hapo, ambapo
aliwasisitiza kuendelea moyo huo kwa sababu wao ndio wamebeba dhamana
ya afya za wananchi.
“Nimefurahi kukuta wazazi
wanahudumiwa vizuri na wenyewe wamekiri kwamba huduma zinazotolewa
hospitalini hapa ni za kuridhisha, tofauti na tulivyozoea kusikia
wagonjwa wakiwalalamikia wauguzi, hivyo ni jambo la kujivunia, hongereni
sana” amesema.
Mmoja wa wagonjwa waliolazwa
katika wodi hiyo Hamisa Rashid ambaye amelazwa katika wodi hiyo amesema
alifikishwa hospitalini hapo wiki mbili zilizopita akiwa katika hali
mbaya na ameweza kuhudumiwa vizuri na sasa anakaribia kutoka.
“Mimi nilikuwa sijitambui, siwezi
kufanya kitu chochote lakini baada ya kuletwa hospitalini hapa madaktari
kwa kushirikiana na wauguzi wamenihudumia vizuri na sasa naweza hata
kwenda chooni mwenyewe na bila msaada wao mimi ningekuwa nimepoteza
maisha kutokana na hali yangu ilivyokuwa,” amesema Hamisa.
Mbali na kutoa msaada huo wa
mashuka pia ametoa baiskeli mbili kwa ajili ya wanawake wawili walemavu
lengo likiwa ni kuwawezesha kufanya shughuli zao za kijamii kwa urahisi.
Akizungumza baada ya kupokea
msaada huo, Rehema Omary amemshukuru mke wa Waziri Mkuu kwa msaada huo,
ambapo alimuomba Waziri Mkuu, Majaliwa awawezeshe kwenda kushiriki
katika shughuli mbalimbali zinazofanywa na walemavu ikiwemo michezo.
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa
Lindi, Godfrey Zambi amewataka watumishi wa hospitali hiyo kufanya kazi
kwa bidii na kuachana na utendaji kazi wa mazoea kwa sababu umepitwa na
wakati.
Pia amesema amefurahishwa na
kitendo cha wagonjwa kukiri kuwa wanahudumiwa vizuri tofauti na
hospitali zingine hivyo kuwataka kuendelea na ari hiyo ya kufanya kazi
kwa bidii, maarifa na weledi mkubwa.
Imetolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu






0 maoni:
Chapisha Maoni