Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akionesha mfano wa hundi
aliyokabidhiwa na Ofisi ya Bunge leo Ikulu, Jijini Dar es Salaam ambapo
fedha hizo ameelekeza zitumike kutengenezea madawati ya shule hapa
nchini(kulia)ni Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Dkt. Tulia Ackson.
Muonekano wa Madawati ambayo
yanatarajiwa kutengenezwa na yaliyoidhinishwa na Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi kama yanavyoonekana katika picha.
Kamishna Jenerali wa Magereza
nchini, CGP John Casmir Minja(kushoto) akiwa na Mkuu wa Jeshi la Kujenga
Taifa, Bregedia Jenerali, Michael Isamuhyo(katikati) wakifuatilia
hotuba ya Rais Magufuli(kulia) ni Mtendaji Mkuu wa SUMA – JKT, Bregedia
Jenerali C.Yateri.
Kamishna Jenerali wa Magereza
nchini, CGP John Casmir Minja akiongea na Wandishi wa Habari kuhusu
namna Jeshi hilo lilivyojipanga kutekeleza jukumu lililopewa.
Baadhi ya Maafisa Waandamizi wa
Jeshi la Magereza pamoja na Maafisa Waandamizi kutoka Makao Makuu ya
Jeshi la Kujenga Taifa waliohudhuria hafla hiyo.
Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, CGP John Casmir Minja akisalimiana
na Katibu wa Bunge, Dkt. Thomas Kashilila wakipokutana katika Viwanja
vya Ikulu, Jijini Da es Salaam(Picha zote na Lucas Mboje wa Jeshi la
Magereza).
……………………………………………………………………………………………….
Na; Lucas Mboje wa Jeshi la Magereza,
JESHI LA MAGEREZA nchini pamoja
na Jeshi la Kujenga Taifa limepewa jukumu la kutengeneza madawati yenye
thamani ya Bilioni 6 ambayo yatasambazwa katika Mikoa yote ya Tanzania
Bara na Zanzibar.
Jukumu hilo kwa Vyombo vya Ulinzi
na Usalama limetolewa leo Aprili 11, 2016 na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, katika hafla
fupi ya makabidhiziano ya mfano wa hundi ya Bilioni 6 za pesa ya
kitanzania kutoka Sekretarieti ya Bunge ya Jamuhuri ya Muungano wa
Tanzania pesa ambazo zimepatikana kufuatia kubana matumizi ya uendeshaji
wa Ofisi hiyo.
Rais Magufuli amesema kuwa Ofisi
ya Bunge pamoja na Watendaji wake wameonesha moyo wa kizalendo kwa Taifa
lao kwani wametekeleza kwa vitendo maelekezo ya kubana matumizi ya
fedha za Serikali hivyo kuokoa kiasi hicho cha Bilioni 6 ambazo
wamezikabidhi ili zitumike katika kutatua changamoto ya uhaba wa
Madawati katika shule nyingi hapa nchini.
“Nikupongeze sana Dkt. Thomas
Kashilila, Watendaji wote wa Ofisi ya Bunge kwa moyo wenu wa upendo,
uzalendo mkaamua kiasi hiki cha fedha Bilioni 6 zikafanye kazi ya
maendeleo kwani mngeweza kuzitumia fedha hizi katika matumizi mengine
hata Mhe. Spika asingejua”. Alisema Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli amewataka
Makatibu Wakuu wote wa Wizara pamoja na Watendaji Wakuu wote wa Taasisi
za Umma/Serikali kuiga mfano huo wa kizalendo aliouonesha Katibu wa
Bunge, Dkt. Thomas Kashilila kwani huo ndio mwelekeo anaoutaka katika
Serikali yake ya Awamu ya Tano.
Awali akiongea kabla ya
Makabidhiano ya hundi hiyo Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson amesema kuwa kiasi hicho cha fedha
kimepatikana kufuatia kubana matumizi katika maeneo mbalimbali ikiwemo
kupunguza safari za nje, gharama za machapisho mbalimbali, gharama za
viburudisho na chakula, matibabu kwa wabunge, mafuta na uendeshaji wa
mitambo nk.
Akizungumzia utekelezaji wa
jukumu la utengenezaji wa madawati hayo Kamishna Jenerali wa Jeshi la
Magereza Nchini, John Casmir Minja amesema kuwa Jeshi la Magereza lipo
tayari kutekeleza agizo la Rais na amejipanga kutumia nguvu kazi ya
Wafungwa waliopo magerezani pamoja na Maafisa na Askari wa Jeshi hilo
ili kukamilisha kazi hiyo kwa wakati kama ilivyokusudiwa.
“Mhe. Rais ametoa maelekezo ya kwenda kufanya kazi hiyo kama
operesheni maalum hivyo sisi kwa upande wa Jeshi letu tupo tayari
kuifanya kazi hiyo kama ilivyoelekezwa kwa kuzingatia maelekezo ya Mhe.
Rais”. Alisema Jenerali Minja.
Jeshi la Magereza Tanzania
limepiga hatua kubwa ya Maboresho juu ya utengenezaji wa bidhaa bora za
Samani hivyo kupelekea kuibuka mara kwa mara Mshindi wa kwanza katika
Maonesho mbalimbali ya Kibiashara hapa nchini.






0 maoni:
Chapisha Maoni