Jumanne, 31 Januari 2017

Wanaotengeneza vyombo feki vya muziki, matangazo vya Candy wabainika


Posted by Esta Malibiche on JAN 31,2017 IN BURUDANI

kibo1
Mkurugenzi wa Kampuni ya Uhuru Music (T) Ltd, Maneno Sanga (kulia), akiwa na Mkurugenzi wa Kampuni ya Hualang Electric ambao ndio watengenezaji wa vyombo vya muziki vya Candy, Yang Hongwei wakati wa kusaini mkataba wa kibiashara wa kusambaza vyombo vya muziki na matangazo vya kampuni hiyo kwa nchi za tano za Afrika Mashariki.
kibo2
Baadhi ya vyombo vya muziki na matangazo vya Candy ambavyo vinasambazwa nchini na kampuni ya Uhuru Music (T) Ltd.
kibo3
……………………………………………………………………………
Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.
Kampuni ya kusambaza vifaa vya muziki na matangazo ya Uhuru Music (T) Ltd, ya jijini Dar es Salaam, imewaonya matapeli wanaoghushi nembo ya vyombo vya muziki na matangazo vya Candy kuwa siku zao zinahesabika na wakati wowote watakumbana na nguvu za dola baada ya mbinu wanazotumia kufanya utapeli huo kubainika.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo, Maneno Sanga ilisema kuwa kikosi kazi cha kampuni hiyo kimegundua njia wanazotumia matapeli hao ambao ni pamoja na kutengeneza vyombo vya muziki na matangazo nchini kwa kutumia teknolojia duni na kubandika nembo bandia ya Candy.
Alibainisha kuwa maharamia hao ambao wana karakarana zao katika maeneo ambayo wameisha yabaini, wamekuwa wakiharibu sifa ya bidhaa hizo ambazo zinatengenezwa na kampuni ya Hualang Electric Company Ltd ya China.
“Uhuru Music (T) Ltd, ndio ambao tuna mkataba wa kusambaza vyombo vya muziki na matangazo vya Candy kwa nchi tano za Afrika Mashariki ikiwemo Tanzania na sio vinginevyo” alisema na kuongeza kuwa pia kuna mawakala ambao wana mikataba na kampuni yake katika kanda tofauti nchini.
Alisema wamewasiliana na mamlaka zote ikiwa ni pamoja na vyombo vya usalama kuhusiana na uhalifu huo ambao pia unaikosesha serikali mapato na kuwatia hasara wananchi kwa kuwauzaia vifaa visivyo na ubora unaotarajiwa.
Anataka watu ambao wanahitaji kununua vifaa vya muziki vya Candy kujiridhisha kwanza kabla ya kufanya manunuzi kwa kuangalia alama tatu muhimu ambazo zinavitambulisha vyombo hivyo ikiwa ni pamoja na ile ambayo ipo katika nembo ya kampuni hiyo ambayo ni kama iliyopo katika fedha za noti.
“Katika logo ya Candy ukiangalia vizuri kuna alama ya fedha ambayo inabadilika badilika na kusomeka maandishi Candy American Technology” anasema na kuongeza kuwa kama bidhaa hiyo ya Candy katika nembo yake haina hiyo chombo hicho ni feki.
Anasema utambulisho mwingine unapatikana kupitia simu ya mkononi aina za Smart kwa mteja ku-scan  alama ya siri ya biashara (Barcode) ambayo inapatikana katika bidhaa hizo na kumletea taarifa zote ikiwa ni pamoja na jina la kampuni yake ya Uhuru Music (T) Ltd.
Pia anabainisha kuwa nembo (logo) za Candy ni za chuma na wala si plastiki kama zilivyo hizo za feki hivyo ni wajibu wa wateja kuzitambua alama hizo na kukataa kufanywa dampo la bidhaa feki ninyingi ni hafifu na zisizodumu katika matumizi.
Anasema wameamua kutoa ufafanuzi huo na kuunda kikosi kazi cha kuchunguza uharamia unaofanyika baada kupokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya wateja ambao wamenunua ala za muziki zenye nembo ya Candy kwa bei ya chini, mbaya zaidi havikuwa na ubora unaotakiwa.
“Tulipofuatilia tulibaini wanapotengenezea,  mbinu wanazotumia kuwahadaa wateja na tumeshirikisha mamlaka zingine wakati wote wa ufuatiliaji” anasema na kuongeza kuwa kuanzia sasa kinachofuata ni hatua za kisheria.
Anazitaja vyombo hivyo vya muziki na matangazo kuwa ni pamoja na vipaza na vinasa sauti, vyombo vya matangazo, spika, mic kwa ajili ya kurekodi muziki, vinanda, stendi maalum za kurekodia, vyombo vya matangazo katika magari na Deck za aina mbalimbali.
Pia taa kwa ajili ya kumbi za disco, vifaa vya kuchanganyia muziki, vifaa vya studio kwa ajili ya kurekodia na bidhaa zingine ambazo zinahusiana na masuala ya muziki na matangazo.
Uhuru Music (T) Ltd, ndio wenye mkataba pia wa kusambaza vyombo hivyo vya muziki na matangazo katika nchi za Kenya, Uganda, Burundi na Rwanda.

0 maoni:

Chapisha Maoni