Posted by Esta Malibiche on JAN 28,2017 IN NEWS
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Bw. Christopher Ole Sendeka kuchukua
hatua kali kwa wote waliohusika na upotevu zaidi ya sh. bilioni moja za
vyama vya ushirika.
Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo jana
jioni (Ijumaa, Januari 27, 2017) alipozungumza na watumishi wa Mkoa wa
Njombe wakati wa majumuisho ya ziara yake ya kikazi ya siku saba mkoani
hapa.
Alisema kati ya fedha hizo sh.
milioni 532.736 zilipotea katika SACCOS ya Kurugenzi Njombe pamoja na
sh. milioni 900 zilizopotea katika Chama cha Ushirika cha Akiba na
Mikopo kiitwacho Wafanyabiashara Njombe SACCOS.
“Maofisa Ushirika nchini
mmeendelea kudhoofisha jitihada za Serikali katika kuimarisha ushirika.
Katika eneo hili ninahitaji Mkuu wa Mkoa ufuatilie suala hili na
kuwachukulia hatua wahusiuka wote,” alisema.
Waziri Mkuu aliwaagiza Wakuu wote
wa Wilaya kuwatumia warajisi wa ushirika kuimarisha ushirika Mkoani
Njombe.”Tunataka ushirika ulete tija kwa wananchi na hatutaki ushirika
ulioambatana na harakati za kugawa watu. Endeleeni kuwashughulikia
wanaushirika wasio waaminifu,”.
Aidha, Waziri Mkuu aliwasisitiza
watumishi wa umma wote nchini kuzingatia uadilifu, uaminifu,
kutojihusisha na rushwa na kutumia ipasavyo fedha za umma Serikali
itachukulia hatua kali dhidi ya watumishi wote wanaotumia nafasi zao
kujinufaisha binafsi.
Alisema anataarifa za Watendaji wa
Wakuu wa Wilaya ya Makete akiwemo Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Bw.
Francis Namsumbo, Mweka Hazina Bw. Edward Mdagachule, Ofisa Utumishi,
Bw. Nicodemas Tindwa na Mkaguzi wa Ndani Bw. Michael Shija kuhusika na
upotevu wa sh. milioni 71 zikiwemo sh milioni 41 za UNICEF.
Waziri Mkuu alisema kuwa watumishi
hao wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya utoaji wa rushwa kwa vyombo
mbalimbali ili kuficha ubadhilifu huo. “Mkuu wa Mkoa hakikisha hatua
stahiki zinachukuliwa kuhusiana na matukio haya,”.
Pia alimuagiza Mkuu huyo wa Mkoa
kuhakikisha kuwa ……..wa Wanging’ombe Bw. Edwin Kigoda anachukuliwa hatua
stahiki kwa ubadhilifu wa sh. milioni 37.9 zilizotolewa kwa ajili ya
kuwajengea uwezo Walimu katika stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu
(KKK).
Mbali na watumishi hao pia Waziri
Mkuu alimtaka Bw. Ole Sendeka kumchunguza na kumchukulia hatua Ofisa
Ardhi wa Mji wa Njombe, Bw. Addo Kabange ambaye anatuhumiwa kuuza
viwanja mara mbili, kuchukua rushwa na kujipatia viwanja vingi kwa bei
nafuu na kuviuza kwa wananchi kwa bei ya juu.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu
alisema atawaelekeza Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Fedha za Serikali
(CAG), Msajili wa Hazina na Mrajisi wa Ushirika kuanza kufuatilia
malalamiko kuhusu umiliki wa kiwanda cha chai cha Lupembe pamoja na
kufuatilia mwenendo wa mgawanyo wa hisa za kiwanda hicho.
Alisema alipotembelea kiwanda cha
chai cha Lupembe ambapo alifarijika kukuta kiwanda hicho kimeanza
kufanya kazi baada ya kusimama kwa takriban miaka nane kutokana na
mgogoro uliopo baina ya mwekezaji wa Kiwanda hicho na Umoja wa Wakulima
wa Chai Muvyulu.
Waziri Mkuu alisisitiza kwamba
Serikali ya Awamu ya Tano haitavumilia migogoro ya kuzuia ajira kwa
wananchi, hivyo aliahidi kushughulikia malalamiko kutoka pande hizo
mbili na kutafuta njia ya kutatua mgogoro uliopo.
Alisema baada ya kusomewa taarifa
ya kiwanda na kwa upande mwingine taarifa ya wanaushirika alibaini
kuwepo kwa mgogoro unaohitaji kutatuliwa ili kuwezesha shughuli za
kiwanda kuendelea kwa amani na usalama.
Aidha, Waziri Mkuu alielekeza
shughuli za ulimaji na uvunaji wa majani ya chai kutoka kwa wakulima na
kupeleka katika kiwanda hicho iendelee na kiwanda kisisimamishe kazi ili
kulinda soko la wakulima na ajira za watumishi wa kiwanda hicho,”
alisema.
Alisema kwa kuwa kiwanda hicho
kinamilikiwa kwa ubia, alimwelekeza Mkurugenzi wa kiwanda hicho
kuhakikisha kuwa wanaweka wawakilishi wawili au watatu wa wanaushirika
katika Bodi ya Kiwanda hicho.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu
alizungumzia suala la kuchelewa kuanza kwa mradi wa chuma cha Liganga,
ambapo alisema ucheleweshaji huo si wa makusudi bali ni mpango wa
Serikali wa kujiridhisha na vipengele mbalimbali vya mkataba ili uwe wa
manufaa kwa Watanzania.
Hata hivyo, Waziri Mkuu alisema
baada ya kutembelea eneo ambalo uchimbaji utakapofanyika, na kujionea
maendelezo ya wananchi yaliyopo, alipata mashaka na kiasi cha sh.
bilioni 13 kilichotengwa na wawekezaji kwa ajili ya fidia kwa wananchi
watakaopisha mradi huo.
Alisema Serikali haina budi
kufanya tathmini ya kina na kujiridhisha. “Nataka nimkumbushe Mheshimiwa
Mbunge (Deo Ngalawa-Ludewa) na Mwenyekiti wa NDC kujiridhisha na
wahusika wanaotarajiwa kupata fidia hiyo,”.
Akizungumzia kuhusu maslahi ya
watumishi, Waziri Mkuu alisema Serikali kupitia Bodi ya Motisha na
Mishahara inaendelea kufanya tathmini ya uzito wa kazi ili kupanga upya
viwango vya motisha na mshahara kwa watumishi wote.
Pia aliwasisitiza waajiri wote wakiwemo Wakurugenzi kutenga fedha kwa ajili ya likizo, masomo na uhamisho, kuandaa leave roster na mipango ya mafunzo kwa watumishi.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAMOSI, JANUARI 28, 2017.
0 maoni:
Chapisha Maoni