Posted by Esta Malibiche on JAN 13,2017 in NEWS
Na. Ahmad Mmow, Lindi.
Katika
harakati za kuongeza uzalishaji wa zao la korosho wilayani Kilwa mkoani
Lindi, halmashauri ya wilaya hiyo kupitia idara yake ya kilimo
inatarajia kugawa bure miche 50000 ya zao hilo kwa wakulima katika msimu
huu wa kilimo wa 2017/2018.
Akizungumza
kwa niaba ya mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, mwanzoni mwa wiki
hii katika kijiji cha Lihimalyao Kusini, mkuu wa idara ya kilimo ya
halmashauri hiyo, John Mkinga, alisema halmashauri ya wilaya ya Kilwa
inamkakati kabambe wa kuongeza kiwango cha uzakishaji wa mazao ya
biashara na chakula katika wilaya hiyo.
Ambapo
kwa msimu huu idara hiyo inatarajia kugawa kwa wakulima miche 50000 ya
mikorosho. Mkinga ambae alieleza hayo kwa niaba ya mkurugenzi mtendaji
wa halmashauri ya wilaya hiyo, Zabron Bugingo, baada ya kutakiwa na mkuu
wa mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi kujibu malalamiko ya wananchi ambao
hadi sasa hawatambuliki ambao walipeleka barua kwa waziri wa TAMISEMI na
Rais zenye malalako. Ikiwamo wilaya hiyo kutelekezwa katika sekta ya kilimo.
Alisema
huo utakuwa ni mwendelezo wa juhudi za kuhakikisha kiwango cha
uzalishaji wa zao hilo Katika wilaya hiyo unaongezeka ili kuongeza
kipato cha wakulima, halmashauri na taifa kwa jumla.
"Msimu
wa mwaka jana tulizalisha na kugawa bure miche 12000 kwa wakulima.
Ikiwamo wakulima wa kata hii na tarafa ya Pande, pia tuligawa mbegu kwa
baadhi ya wakulima na mpango huo ni endelevu," alisema Mkinga.
Kuhusu
uzalishaji wa mazao ya chakula, Mkinga alisema serikali inatambua
umuhimu na faida ya nchi kujitosheleza kwa chakula. Kwakutambua hilo,
idara ya kilimo ya halmashauri hiyo imekuwa ikipeleka maombi serikali
kuu ya kupatiwa matrekta kwa ajili ya kuyagawa kwa wakulima ili kuongeza
uzalishaji wa mazao hayo wilayani humo.
Mkuu
huyo wa idara ya kilimo alibainisha kwamba hadi sasa baadhi ya vijiji
wilayani humo, ikiwamo baadhi ya vijiji vilivyopo katika tarafa ya
Pande vimepatiwa matrekta.
"Napenda
kuwashauri wakulima waunde vikundi kwasababu matrekta hayo hatumpi
mkulima mmojammoja, mwaka huu tumeomba tena na tukipewa tutagawa katika
vijiji vingine," alisema Mkinga.
Aidha
aliwahakikishia wakulima wa korosho kwamba dawa za kuuwa wadudu na
kuzuia ukungu zitafikishwa kwao kabla ya mwezi Aprili mwaka huu, ili
waweze kuzitumia kwa wakati.
Mkuu
wa mkoa Zambi alikwenda kijijini hapo ikiwa ni utekelezaji wa agizo la
waziri wa nchi ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(TAMISEMI), George Simbachawene. Aliyemtaka kwenda wilayani humo,
hususani tarafa ya Pande na kata ya Lihimalyao. Ili kupata ukweli wa
barua zilizotumwa na watu ambao hadi sasa hawajafahamika kwenda kwake
yeye na Rais Magufuli.
Ingawa
walitumia majina na kughushi saini za baadhi ya viongozi wa vijiji vya
Lihimalyao Kusini, Rushungi na kata ya Lihimalyao. Barua zilikuwa na
malalamiko mbalimbali dhidi ya serikali kwamba wilaya hiyo imetupwa
katika huduma za jamii, hakuna usalama, maliasili na rasimali zinaporwa
na haziwanufaishi, wilyaa hiyo inawalimu wa shule za msingi wasio na
sifa hakuna maji na hakuna juhudi zozote zilizofanywa na serikali katika
kuondoa tatizo la maji na matumizi ya jembe la mkono katika tarafa ya
Pande na wilaya kwa jumla.
Hata
hivyo malalamiko mengi yalionekana ni ya uongo. Huku viongozi wa vijiji
hivyo na kata hiyo ambao majina yao yametumika kwenye barua hizo
walikanusha kuandika na kumuomba mkuu huyo wa mkoa kupitia vyombo vya
ulinzi na usalama awatafute, awakamate na awafikishe kwenye vyombo vya
sheria walioandika barua hizo.
Kwa madai kwamba yaliyoekelezwa kwenye barua hizo yalikuwa ya uongo na dalili ya uchochezi baina ya wananchi na serikali yao.
0 maoni:
Chapisha Maoni