Posted by Esta Malibiche on JAN 13,2017 in NEWS
Na Nathaniel Limu, Manyoni
Mkuu
wa wilaya ya Manyoni mkoani Singida, Geoffrey Mwambe amefanikiwa kuzuia
msichana mwenye umri wa miaka 14 (jina tunalo) kuolewa na ameagiza
arejeshwe mara moja shuleni kuendelea na masomo yake.
Mtoto huyo aliachishwa shule mwaka juzi
2015 akiwa darasa la sita katika shule ya msingi Idodiandole
halmashauri ya Itigi wilaya ya Manyoni.
Imeelezwa kwamba mtoto huyo aliachishwa
shule kutokana na tatizo la ugonjwa wa kifafa lakini miezi mitatu baada
ya kuachishwa shule, mchakato wa kuozeshwa ulianza kufanyika.
“Fundi mwashi Jeremieah Antony (20)
mkazi wa Mwanzi Manyoni mjini aliweza kumuoa mwanafunzi huyo kwa ndoa
ya kimila nyumbani kwa mama mzazi wa bwana harusi,” alisema Mwambe.
Mkuu huyo wa wilaya, alisema kuwa
wazazi wa binti huyo walitumia kigezo cha ugonjwa wa binti yao,
kumwachisha shule na kufanya juhudi za kumwozesha, ili waweze kujiepusha
na shida ya kumuhudumia.
Mwambe alitumia nafasi hiyo kukemea
vikali vitendo vya kuoza wasichana wadogo hasa wanafunzi na kwamba
watakaokamatwa kwa tuhuma hizo, watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Aidha, alisema bwana harusi Jeremiah,
mama wa bwana harusi Janeth Makole na kaka wa bwana harusi Alexander
Anthony, wamefikishwa polisi kwa uchunguzi zaidi wakati wazazi wa
mwanafunzi huyo, bwana na bibi Robert Mlewa wanaendelea kutafutwa.
Wakati huo huo, mkuu huyo wa wilaya,
amemwagiza Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya wilaya ya Manyoni,
amlipie gharama za sare na vifaa vya shule na afisa elimu na ofisa
maendeleo ya jamii wamsimamie na wawe walezi wake kuhakikisha anafika
mbali kielimu.
“Nitumie fursa hii kuwashukuru na
kuwapongeza wenyeviti wa vitongoji vya Samaria na Mwanzi, mtendaji kata
na diwani kata ya Manyoni, kwa kunipatia taarifa hii iliyofanikisha
kuzuia ndoa hii haramu,” alisema Mwambe.
Kwa upande wake mwanafunzi huyo,
amesema hapo awali aligoma kuolewa, lakini kutokana na shinikizo la
wazazi wakidai tayari wamekula mahari na hawana uwezo wa kurejesha,
hivyo hakuna namna lazima aolewe, ndipo kukubali kwa shingo upande kutii
amri ya wazazi.
0 maoni:
Chapisha Maoni