Serikali
imesitisha waraka wa muongozo uliotolewa kuhusu matumizi ya mihuri kwa
wenyeviti wa Mitaa na vijiji mpaka pale itakaposhirikiana na kukubaliana namna
bora ya kuendesha masuala ya kuhudumia wananchi.
Akizungumza
na baadhi ya wenyeviti wa mtaa, Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali
za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene amewataka wenyeviti wa mitaa nchini
kufanya kazi kwa kuzingatia Sheria na taratibu zilizopo.
Simbachawene
alisema kuwa nia ya kusitisha waraka huo ni kuweka utendaji mzuri baina ya
Serikali na watendaji wake wa chini.
“Utaratibu
uliopo uendelee mpaka pale Serikali itakapotoa utaratibu mwingine wa matumizi
mbalimbali ya mihuri hiyo baada ya kujadiliwa na kushirikiana vya kutosha”
alifafanua Waziri Simbachawene.
Simbachawene alisema kuwa kuna baadhi ya wenyeviti wa mitaa wamekuwa wakitumia vibaya mihuri hiyo na kupelekea migongano na migogoro ya ardhi katika vijiji na mitaa ikiwemo maeneo ya Ununio, Temeke.
Mbali
na hayo alisema kuwa katika Tangazo la Serikali namba 3 lililotolewa 5
Septemba, 1994 limeeleza baadhi ya vitendea kazi vya mwenyekiti wa mtaa ni
bendera yenye nembo ya Halmashauri, daftari ya kutunza kumbukumbu na rejista ya
makazi.
Alisema kuwa mamlaka ya mwenyekiti haitokani na mihuri, bali utendaji uliopo ndani ya mtaa au kijiji husika, hivyo mamlaka ya mwenyekiti ipo pale pale na haibebwi na muhuri bali muhuri huonesha nguvu ya ofisi baada ya kuwashirikisha watendaji tofauti ndani ya kijiji katika kutoa maamuzi.
“Muhuri
si mali ya mwenyekiti binafsi, hivyo kwa yeyote atakayekiuka matumizi ya mihuri
hiyo Sheria itachukua mkondo wake” alisisitiza Simbachawene.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa Wilaya ya Temeke
Bakiri Makele, ameahidi kushirikiana na Serikali kwa kutumia mihuri hiyo kwa
kufuata Sheria na taraibu zilizopo.
Naye
Katibu wa Wenyeviti hao, Marium Machicha alimshukuru Waziri mwenye dhamana kwa
kauli aliyoitoa baada ya kuliona tatizo hilo na kuahidi kulifanyia kazi.
Serikali
ilitoa Muongozo huo wa namna wa matumizi ya mihuri kwa wenyeviti wa mitaa na
vijiji kwa sababu ya matumizi mabaya ya mihuri kwa baadhi ya wenyeviti wa mtaa
na vijiji nchini.
0 maoni:
Chapisha Maoni