Posted by Esta Malibiche on JAN 27,2017 IN NEWS
Khadija Khamis –Maelezo
Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu amewataka Mahakimu,
makadhi na wasuluhishaji wa migogoro ya kazi kutekeleza majukumnu yao
kwa uwadilifu wakizingatia kutoa haki kwa wanaostahiki kupata haki
hizo.
Jaji Makungu aliyasema hayo katika hafla ya kuwaapisha Makadhi wa
Wilaya, Mahakimu wa Mahakama ya Mwanzo na wasuluhishi na waamuzi wa
migogoro ya kazi chini ya kamisheni ya kazi katika mahakama kuu Vuga.
Aliwaeleza wasimamizi hao wapya wa sheria kuwa majukumu
waliyokabidhiwa na Taifa sio mepesi na kuwataka kuzingatia maadili ya
kazi ili haki na sheria iweze kuchukua nafasi yake.
Aidha alisema usuluhishi na utoaji maamuzi panapotokea migogoro
katika sehemu za kazi inasaidia katika kujenga umoja na ushirikiano
miongoni mwa wafanyakazi.
Waliapishwa kuwa Makadhi wa Mahakama ya Wilaya ni Idi Said Khamis na
Sleiman Khamis Machano, Mahakimu wa Mahakama ya Mwanzo ni Hakimu
Amina Mohd Makame na Hamad Ali Sleiman, wasuluhishaji na waamuzi wa
migogoro ya kazi ni Fatma Abdalla Hamad, Jokha Lali Ramadhani , Juma
Ali Makame na Raya Said Ali .
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya siku ya
sheria duniani ambayo kilele chake ni tarehe tisa ya kila mwaka, Jaji
Mkuu Omar Othman Makungu alisema shamra shamra za sherehe hiyo zitaanza
tarehe nne mwezi ujao kwa matembezi ya hiari.
Aliongeza kuwa katika maadhimisho hayo kutakuwa na maonyesho ya
sheria, utoaji wa vyeti kwa mawakili wapya na uzinduzi wa mahakama ya
watoto katika kijiji cha Mahonda Wilaya ya Kaskazi B.
Alifahamisha kuwa kutakuwa na mikakati ya mipango kazi ambayo
itasaidia kufanya kazi kwa wakati muafaka na kuwepo na utaratibu maalumu
wa kuamua kesi ili kuepuka msongamano wa kesi katika mahakama ili
kupunguza malalamiko kutoka kwa wananchi.
Jaji Mkuu wa Zanzibar alisema kaulimbiu ya siku ya sheria duniani mwaka huu ni kusimamia sheria na maadili katika kutenda haki.
0 maoni:
Chapisha Maoni