Posted by Esta Malibiche on JAN 30,2017
Wizara ya Nishati na Madini
inapenda kuufahamisha umma kuwa, Zoezi la kuwaokoa wachimbaji 15
waliofukiwa na kifusi tarehe 26/01/2017 kwenye mgodi wa dhahabu eneo la
kijiji cha Mawemeru, Nyarugusu Wilayani Geita limekamilika kwa
mafanikio.
Ajali ya kufukiwa wachimbaji hao
iliyohusisha Watanzania 14 na raia 1 wa China ilitokea kwenye leseni ya
uchimbaji wa Kati wa madini ya dhahabu yenye Namba ML 492/2013
inayomilikiwa na Bw. Ahmed Mubarak Adam.
Chanzo cha ajali hiyo ilikuwa ni kuanguka kwa shaft ya mgodi huo na kufukiwa na kifusi wakati wachimbaji hao wakifanya kazi mgodini chini ya ardhi.
Tukio la uokoaji limefanikiwa leo
tarehe 29/01/2017 ambapo wahanga hao walianza kutolewa shimoni kuanzia
saa 5 hadi saa 5:30 asubuhi wote 15 wakiwa hai ingawa walikuwa
wamedhoofika kiafya. Aidha, wachimbaji hao wamepewa huduma ya kwanza
katika eneo la ajali na kisha kukimbizwa Hospitali Teule ya Rufaa ya
Geita. Hadi sasa wachimbaji hao wapo Hospitali wakiendelea na matibabu
kwa uchunguzi zaidi wa afya zao.
Juhudi za kuokoa wachimbaji hao
ambazo zilifanyika kwa kufukua kifusi katika eneo la ajali zilianza mara
baada ya tukio hilo kutokea. Uongozi wa Mkoa wa Geita ukiongozwa na
Mkuu wa Mkoa Meja. Jen.(Mst) Ezekiel E. Kyunga ulishirikiana na Wataalam
wa Wizara ya Nishati na Madini na Kampuni za Madini mbalimbali mkoani
Geita katika zoezi la ufukuaji kifusi ili kuokoa maisha ya wchimbaji
hao.
Kampuni zilizoshiriki kwa kutoa mitambo na vifaa mbalimbali ni Kampuni ya Busolwa Mining Ltd; Kampuni ya Geita Gold Mine (GGM); Kampuni ya Nyarugusu Mining Ltd; Nsangano Mining Project; Metchell Tanzania Drilling; WAJA Hospital pamoja na wachimbaji wadogo wa Mkoa wa Geita wakiongozwa na Viongozi wa wachimbaji madini Wilaya, Mkoa na Taifa.
Akizungumza mara baada ya
kuokolewa wachimbaji hao, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard
amewashukuru wadau wote walioshiriki kwa hali na mali kufukua kifusi na
hatimaye kufanikiwa kuwatoa wachimbaji chini ya ardhi wakiwa hai.
Dkt. Kalemani amewaomba
Watanzania kuendelea na moyo huo pale majanga kama haya yanapotokea.
Aidha, Dkt. Kalemani ameagiza shughuli zifungwe kwa muda wa siku tano
kwenye mgodi uliopata ajali kuanzia tarehe 29/01/2017 ili kutoa nafasi
kwa Kamishna wa Madini kufanya tathmini ya hali ya usalama wa mgodi na
kutoa maelekezo kabla ya shughuli kuanza.
Vilevile, amewataka wachimbaji
wawe watulivu katika kipindi ambacho tathmini ya hali ya usalama wa
mgodi inafanyika na kuagiza Uongozi wa Mkoa kuhakikisha kuwa ulinzi
unaimarishwa eneo la mgodi ili watu wasiweze kuingia na kuhatarisha
maisha yao.
Pia, ameagiza ukaguzi wa kina
ufanyike kwenye migodi mingine ya wachimbaji wadogo na ya kati eneo la
Nyarugusu na kwingineko nchini ili kuhakikisha kuwa migodi inakuwa
salama kwa wachimbaji wa migodi husika.
Imetolewa na;
KATIBU MKUU
WIZARA YA NISHATI NA MADINI
29/1/2017
0 maoni:
Chapisha Maoni