Jumatatu, 23 Januari 2017

TRA MKOA WA IRINGA KUKUSANYA ZAIDI YA 63BN/- MWAKA 2016/17

Posted by Esta Malibiche on JAN 23,2017 IN NEWS




Mamlaka ya Mapato Manzania (TRA) mkoani Iringa imepangiwa lengo lakukusanya mapato ya shilingi 63bn/- katika mwaka wa fedha 2016/2017, amesema Charles Kichere Naibu Kamishna Mkuu wa TRA.

Kichere aliyasema hayo katika mkutano wa TRA na wafanyabiashara kutoka mikoa ya Njombe na Iringa uliofanyika mkoani Iringa.

Alisema kuwa mkoa wa iringa ukiwa ni mmoja ya mikoa tajiri nchini itakusanya mapato hayo kutoka vyanzo mbalimbali vya mapato.

Kichere alisema kuwa mapato hayo yatakusanywa kutoka kwa wafanyabiashara, walipa kodi, waajiri, makandarasi pamoja na wadau wengine wa kodi.

“Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) imeendelea kubuni mikakati mbali mbali ya kuongeza ukusanyaji wa mapato ili kuendana na kauli mbiu ya serikali ya awamu ya tano isemayo “HAPA KAZI TU” ili kutimiza na kuvuka lengo la kukusanya shilingi trilioni 15.1 kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2016/17,” alisema Kichere.

Alisema hivi sasa nchini inaelekea katika uchumi wa kati na wa viwanda hakunabudi kutimiza lengo la kuifanya bajeti ya taifa kujitegemea kwa kiwango kikubwa. 

Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha bajeti ya shilingi trilioni 29.5 ya mwaka wa fedha 2016/17 ambayo iliwasilishwa na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango June 08, 2016.

Bajeti hiyo ilipigiwa kura na wabunge waliokuwepo bungeni, ambapo jumla ya wabunge 251 walipiga kura za ndio za kuipitisha bajeti hiyo kati ya wabunge 252 waliokuwepo ukumbini wakati kura hizo zikipigwa.

Katika hatua nyingine, Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Charles Kichere amewashauri wafanyabiashara nchini kutumia mashine za kielectroniki (EFDs) kwani kutasaidia kukuza pato la Taifa.

Naye, Onesmo Mwajombe mfanyabiashara kutoka mkoa wa Njombe aliomba serikali kupeleka hela kwenye mabenki ili waweze kukopa, ambapo aliongeza kuwa mitaji yao iko taabani.

Alisema kuwa ili serikali iweze kukusanya mapato kutoka kwa wafanyabiashara hainabudi kupeleka fedha kwenye mabenki ili wafanyabiashara waweze kukopa kwa ajili kuimarisha mitaji.

“Tukiende kwenye mabenki kukopa fedha ya mitaji tunaambiwa wapo kwenye kipindi cha mpito…, ” alisema Mwajombe.

0 maoni:

Chapisha Maoni