Ijumaa, 13 Januari 2017

Serikali yadhamiria Kumaliza Mgogoro wa LOLIONDO Uliodumu kwa Zaidi ya Miaka 25

Posted by Esta Malibiche on JAN 13,2017 in NEWS

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani (wa pili kushoto) akioneshwa Ramani ya Kijiji cha Ololosokwan na Diwani wa Kata hiyo, Yanick Ndoinyo alipotembelea kijiji hicho hivi karibuni kuona changamoto za uhifadhi. Kulia ni Kaimu Mwenyekiti wa Kijiji cha Ololosokwan, Emmanuel Salteimoi. 

Kundi la mifugo likiwa ndani ya Pori Tengefu la Loliondo, karibu kabisa na mpaka wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti. 

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani (kulia) akizungumza katika kikao cha wadau wa mgogoro wa Pori Tengefu la Loliondo alichokiitisha katika ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, Tarafa ya Loliondo mkoani Arusha hivi karibuni.

..............................................

Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais, Dkt. John Pombe Magufuli mara tu ilipoingia madarakani mwezi Oktoba mwaka juzi ilitoa vipaombele vyake kadhaa vya kutelezwa na wizara zake mbalimbali huku Wizara ya Maliasili na Utalii ikikabidhiwa majukumu mazito matatu ya kutekeleza katika kipindi cha uongozi wake. 


Majukumu hayo yaliyotolewa na Rais Magufuli wakati wa hotuba yake ya kwanza ya kulihutubia bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mjini Dodoma, ni yale ya kuhakikisha kuwa wizara hiyo inakomesha vitendo vya ujangili, kuongeza mapato ya serikali na kushuulikia utatuzi wa migogoro ya mipaka kwenye maeneo ya hifadhi nchini. 


Wizara ya Maliasili na Utalii, imesema kuwa imejipanga kuhakikisha kuwa malengo yake ya uhifadhi wa Maliasili, Malikale na Kuendeleza Utalii pamoja na utekelezaji wa vipaombele ilivyopewa na Serikali ya awamu ya tano kuwezesha kufikia malengo hayo yanatimia kwa wakati.

Kwa upande wa utatauzi wa migogoro kwenye maeneo ya hifadhi nchini, Wizara hiyo imejipanga kuwashirikisha wadau wote wanaohusika na migogoro hiyo kwa kukaa nao pamoja kwenye vikao vya majadiliano na kuweka mikakati ya pamoja ya kufikia suluhu ya migogoro hiyo kwa faida ya Serikali na wadau wote wanaohusika.

Hivi karibuni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani alifanya ziara ya kiutafiti katika Hifadhi ya Ngorongoro pamoja na Pori Tengefu la Liliondo, lengo kuu la ziara hiyo ikiwa ni kuona uhalisia wa changamoto zilizopo pamoja na kupata taarifa sahihi kutoka kwa wadau husika, alifanya hivyo bila ya kujitambulisha kwa lengo la kupata taarifa sahihi kuhusiana na migogoro hiyo.

Akiwa katika Tarafa ya Loliondo alitembelea kijiji cha Ololosokwan, Pori Tengefu la Liliondo, sehemu ya mpaka wake na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na eneo la muwekezaji, kampuni ya Ortello Business Corporation (OBC) na kampuni ya &Beyond (Kleins Camp).


Akiwa katika eneo hilo alizungumza na viongozi wa kijiji cha Ololosokwan ambao waliwasilisha changamoto kadhaa ikiwemo ongezeko la mifugo kutoka nchini Kenya na vijiji jirani hususani wakati wa kiangazi kwa ajili ya kutafuta malisho na uelewa tofauti wa mpaka baina ya vijiji na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.


Diwani wa Ololososkwan, Yanick Ndoinyo alisema uhifadhi umekuwa ukiwanufaisha kwa kiasi kikubwa kwa kuwa kupitia utalii kijiji hicho hupata fedha taslim zaidi ya shilingi milioni 300 kwa mwaka kupitia mikataba ya wawekezaji na mgao kutoka Serikalini.

Pamoja na mchango huo amesema “wawekezaji wa eneo hili wamekuwa wakitekeleza miradi ya jamii ambapo wamechimba visima vinne, wamejenga madarasa mawili na kisima kingine kinajengwa jirani na kata hii, lakini kampuni zote kwa ujumla zinatoa ajira kwa wanavijiji, kwahiyo kwakweli sisi ni kijiji ambacho tumeona manufaa ya utalii “

Ndoinyo alisema fedha hizo zimekuwa zikisaidia kusomesha watoto masikini kuanzia elimu ya awali hadi chuo kikuu, kusaidia ujenzi wa zahanati na huduma nyingine za jamii.

Kwa upande wa kampuni ya Ortello Business Corporation (OBC) ambao wamewekeza katika pori hilo kupitia Afisa Mahusiano wao, William Parmat walisema changamoto kubwa inayowakabili ni ya wananchi kuingiza mifugo katika eneo la uwekezaji jambo linalosababisha uharibifu mkubwa wa mazingira ikiwemo wanyamapori kutoweka.

Muwekezaji huyo alisema wapo tayari kuweka makubaliano ya uhifadhi na wananchi pamoja na kusaidia kujenga miundombinu ya huduma za jamii. Alisema changamoto ya mifugo imesababishwa na msukumo wa baadhi ya asasi za kiraia kwa wananchi kwamba Serikali inataka kuchukua pori hilo hivyo waingize mifugo yao kwa ajili ya kulilinda.

Naibu Waziri Makani aliuahidi uongozi wa kijiji cha Ololosokwan pamoja na wawekezaji hao kuwakutanisha wadau wote wanaohusika na mgogoro wa pori hilo kwa ajili kujadili changamoto zilizopo na kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu.

Akiwa kwenye Pori Tengefu la Loliondo na kwenye mpaka wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti alishuhudia makundi ya mifugo ikiwa ndani ya pori hilo na mingine ikizagaa maeneo ya mpakani na Hifadhi hiyo. Alielezwa na Viongozi wa Wilaya ya Ngorongoro kuwa, mifugo hiyo huingizwa kwa ajili ya malisho wakati wa usiku kwenye hifadhi ya Serengeti. 


Inaelezwa kuwa eneo la Pori Tengefu la Loliondo lina umuhimu wa pekee katika uhifadhi kwa sababu ni sehemu ya mazalia ya wanyamapori, mapito ya wanyamapori na vyanzo vya maji. Kutokana na sababu hizo, eneo hilo linapaswa kuendelea kuhifadhiwa ipasavyo, kwa kuwa linachangia kwa kiwango kikubwa kuimarisha mfumo wa ikolojia ya Hifadhi ya Serengeti.

Siku chache baada ya ziara hiyo ya kiutafiti, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alifanya ziara ya kikazi mkoani Arusha na kuwaagiza viongozi wa Serikali kukaa pamoja na wadau wanaohusika na migogoro ya ardhi katika Tarafa ya Loliondo na kuitafutia suluhu ya kudumu.

Baada ziara hiyo ya Waziri Mkuu, Naibu Waziri Makani aliendelea na ziara yake katika tarafa ya Loliondo ambayo aliikatisha kupisha ziara Waziri Mkuu. Mara hii ziara hiyo ikihusisha pia ufuatiliaji wa maagizo ya Waziri Mkuu aliyoyatoa kwenye ziara yake mkoani Arusha.

Aliwasili Loliondo kwa ajili ya kuweka mkakati wa kumaliza changamoto ya mgogoro uliodumu kwa zaidi ya miaka 25 kati ya mwekezaji, wanavijiji, mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), suala la mifugo, uharibifu wa mazingira na utata wa mpaka wa Hifadhi ya Serengeti na Loliondo.  

Tarehe 29 Desemba, 2016 alifanya mkutano na wadau wanaohusika moja kwa moja na mgogoro wa Loliondo, mkutano huo ulifanyika katika ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, Tarafa ya Loliondo, Kupitia mkutano huo aliunda kamati maalum ya kutafuta suluhu ya kudumu ya mgogoro huo.

Kamati hiyo inahusisha taasisi za serikali, asasi za kiraia, viongozi wa dini, wazee wa kimila (Leigwanan), viongozi wa vijiji, wajumbe wa kamati teule ya vijiji 15 ya mpango bora wa matumizi ya ardhi na uendelezaji wa uhifadhi na wawakilishi wa wanawake na vijana. Aliunda pia kamati ya kuandaa kanuni za kundesha vikao vya kamati hiyo.

Naibu Waziri huyo aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa kamati hiyo, na Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Rashid Mfaume Taka akateuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti.  

“Kamati ya kanuni itumie muda wa wiki mbili hadi kufikia tarehe 17 Januari, 2017 iwe imeshakamilisha rasimu ya kanuni ili tarehe 18 Januari, 2017 tuzipitie, tuzijadili na kuzipitisha. Hatua itakayofuata ni mawasilisho ya taarifa mbalimbali kutoka kwa wadau pamoja na majadiliano”, alisema Makani.

Aliagiza pia taarifa mbalimbali za kamati zilizowahi kushuulikia mgogoro huo miaka ya nyuma na mapendekezo yake pamoja na taarifa mbalimbali za sheria za uhifadhi na vijiji kwa ajili ya kusaidia majadiliano hayo ziwasilishwe.

Kikao hicho kilikubaliana kazi hiyo ifanyike ndani ya miezi mitatu hadi kufikia tarehe 31 Machi, 2017 iwe imekamilika na muafaka upatikane kwa ajili ya kuishauri Serikali namna bora ya kumaliza mgogoro huo.

Wadau wote walikubaliana kushiriki vikao vya majadiliano huku wengine wakipongeza hatua iliyofikiwa na Serikali ya kutaka kumaliza mgogoro huo, hata hivyo Naibu Waziri Makani alitoa angalizo kwa wadau hao; "Kuna watu humu ndani na hata nje ambao hawataki tumalize migogoro Loliondo, nitoe rai kwao, waache chokochoko.

“Wafikishiwe salamu, tutawabaini, tutawakamata na kuwashitaki kwa kosa la kukwamisha jitihada za Serikali kuwaletea wananchi maendeleo yao, Wananchi muone umuhimu wa jitihada za Serikali kumaliza changamoto hii na kutuunga mkono”, alisema Makani.

Akizungumza katika mkutano huo, mchangiaji mmoja ambaye hakutambulisha jina lake alisema “Eneo hili Loliondo lenye kata saba na vijiji 15 lilikosekana dawati la pamoja, kwa mfumo huu tutaenda mbele, Taasisi nyingi zimekuwa zikipotosha umma kuhusiana na taarifa za Loliondo, tutashukuru kuona tunapata muafaka kupitia kamati hii iliyoundwa leo”

Changamoto ya Mgogoro wa Pori Tengefu la Loliondo ni mkwamo kwa maendeleo ya wananchi wa Loliondo na Taifa kwa ujumla, Kila mwananchi wa Loliondo ana nafasi kubwa  ya kuhakikisha mgogoro huu unafikia tamati kwa kushirikiana na Serikali na wadau wengine. Kila mmoja atimize wajibu wake mgogoro huu utakuwa historia na Loliondo itakua salama na kupiga hatua kimaendeleo. 

0 maoni:

Chapisha Maoni