Jumatano, 11 Januari 2017

Benki ya KCB yatoa mafunzo ya ujasiriamali kwa wanawake Dar

  Posted by Esta Malibiche on JAN 11,2017 In  NEWS
Benki ya KCB Tanzania imetoa mafunzo kwa wanawake wajasiriamali inayoitwa “2JIAJIRI” ambayo yanalenga kuwasaidia wanawake wajasiriamali kutoka katika matatizo yanayosababisha biashara zao zishindwe kuendelea.
Programu hiyo pia itaongeza ajira nchini kwa wanawake na hivyo biashara zao zitapanuka na kuwa na uwezo wa kuajiri wengine. 

Mafunzo haya yameendeshwa na wataalamu kutoka Tanzania Entrepreneurship and Competitiveness Center -TECC waliobobea katika masuala ya kijasiriamali, kifedha na ushindani wa biashara
Akizungumza kuhusu mafunzo hayo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya KCB, Godfrey Ndalahwa alisema “Mpango huu ni endelevu na tumepanga kufundisha wajasiriamali 315 nchi nzima. Leo tunafundisha wajasiriamali 100 katika makundi mawili tofauti. Mafunzo haya ni bure kabisa, KCB Bank itagharimia gharama zote. Tunachokihitaji kutoka kwao ni mahudhurio ya siku zote tatu na usikivu wa hali ya juu.”

Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya KCB Tanzania Godfrey Ndalahwa, akiongea na wanawake wajasiriamali waliohudhuria mafunzo ya ujasiriamali yaliyotolewa na benki hyo mkoani Dar es Salaam.
Ndalahwa alisema kuwa mafunzo hayo yatafanyika mikoa yote ambayo benki ya KCB ina matawi ikiwepo Dar Es salaam, Mwanza, Morogoro, Arusha, Moshi na pia Zanzibar kwa kulenga wanawake wajasiriamali wadogo na wa kati ambao tayari wanaendesha biashara lakini wanataka kuziimarisha zaidi.
Alisema lengo ni kuwawezesha kudhibiti vipengele vya uzalishaji na mgawanyo wa mapato na faida {control over factors of production and distribution of income and benefits) lakini zaidi ni kuwawezesha kuyatawala maisha yao kiuchumi na kijamii.

Mkuu wa Masoko na Mawasiliano ya Umma wa benki ya KCB, Christine Manyenye akiongea na wanawake wajasiriamali waliohudhuria mafunzo ya ujasiriamali yaliyotolewa  na benki hiyo Dar es Salaam.
“Matatizo tunayotarajia kutatua kutoka kwa wanawake wajasiriamali ni elimu ya kifedha, kufikia huduma za kifedha, Ukosefu wa dhamana, kutokujua vizuri masuala ya kisheria, uelewa finyu wa sera za serikali na kiuchumi, njia hafifu za kuendesha biashara endelevu, ukosefu wa mtaji na utaalamu wa kuanzisha biashara kubwa,” alisema.
Mkurugenzi aliongeza kwamba baada ya mafunzo hayo benki itawapatia wanawake wajasiriamali hao maafisa watatu watakaotembelea biashara zao na hii ni kwa wale tu ambao watahudhuria mafunzo ya siku tatu yote na kuonyesha nia ya kujiendelea kibiashara. Maafisa hao watakua ni afisa fedha, afisa sheria na afisa masoko.

Baadhi ya wanawake wajasiriamali waliohudhuria mafunzo ya ujasiriamali yaliyotolewa na Benki ya KCB mkoani Dar es Salaam.

0 maoni:

Chapisha Maoni