Posted by Esta Malibiche on JAN 5,2017 in NEWS
Mwenyekiti wa halmashauri ya
Chalinze, Saidi Zikatimu, akizungumzia mikakati waliyojiwekea kuwalipa
posho wenyeviti wa vijiji na vitongoji sanjali na kuinua mapato ya
ndani (Picha na Mwamvua Mwinyi)
………………………………………………………………………
Na Mwamvua Mwinyi,Chalinze
HALMASHAURI ya mji mdogo wa Chalinze,mkoani Pwani,imetenga kiasi cha sh.mil 36 katika kipindi cha mwaka 2016/2017 kwa ajili ya kuwalipa posho wenyeviti wa vijiji na vitongoji katika halmashauri hiyo.
Kati ya fedha hiyo wenyeviti hao wanalipwa kila mmoja sh.30,000 kwa mwezi hadi mwezi july mwaka huu itakapokoma bajeti hiyo.
Akizungumzia
kuhusiana na mpango huo,kwa waandishi wa habari mjini hapo,mwenyekiti
wa halmashauri ya mji wa Chalinze ,Said Zikatimu ,alisema halmashauri
hiyo imeamua kuwalipa posho wenyeviti hao kwani wanafanyakazi kubwa
ndani ya miaka mitano bila kuambulia chochote.
Alisema
wameshirikiana na mbunge wa jimbo la Chalinze,Ridhiwani Kikwete,kuona
namna ya kuwatupia jicho wenyeviti hao wa vijiji na vitongoji .
Aidha
Zikatimu alieleza kwamba ,fedha hizo zitawawezesha wenyeviti hao
kujikimu na kuondokana na hali ya kuuza ardhi za vijiji kwa visingizio
vya kukosa posho ama mishahara.
Alibainisha
,fedha hiyo pia itaweza kuwasaidia wenyeviti hao kuwa na morali na ari
ya kuchapakazi kwenye maeneo yao na wamejipanga kila mwaka watakuwa
wakitenga fedha hizo.
“Kiasi
hiki cha sh.mil.36 ni fedha watakazolipwa hadi july 2017 na bajeti
inayofuata tutaangalia kama kuna uwezekanao wa kuongeza kiasi
kilichopangwa katika bajeti hii ama ibakie kiasi kilichotengwa kwenye
bajeti hii”alifafanua Zikatimu.
Hata
hivyo Zikatimu alisema ,wanachotarajia ni wenyeviti hao kuendelea kuwa
wasimamizi wazuri katika vyanzo vya mapato na kuachana na tabia ya kuuza
maeneo ya vijiji kinyume na taratibu.
Alisema
wanawahamasisha kusimamia vyanzo vya mapato ili kuinua makusanyo hasa
ya vyanzo vya ndani ikiwemo vizuizi mbalimbali vya pembezoni na ndani ya
mji huo.
Mwenyekiti huyo alitoa wito kwa
halmashauri nyingine nchini kuwaangalia wenyeviti hao kwani kwa Chalinze
imeshaleta tija ndani ya miezi sita tangu kuanza kwa mpango huo.
Aliiomba
serikali na halmashauri hizo ziangalie namna ya kuwatengea fedha
wenyeviti wa vijiji na vitongoji kama ilivyo kwa madiwani na wabunge
wanavyotengewa posho wakimaliza muda wao,ili waweze kuwa na moyo wa
kufanya kazi pasipo kukosa chochote.
“Halmashauri
ni sehemu ya kwanza na serikali kuu ni sehemu ya pili,hivyo halmashauri
zionyeshe nia ili serikali ilione hili,kwa kuwapa kipaombele ya
kuwatengea fedha bila kuwaacha”
Zikatimu
alisema wenyeviti hao wanasimamia chaguzi mbalimbali na ilani ya CCM
hivyo waangaliwe katika suala hilo ili waweze kujiona ni viongozi
wanaoaminika kwenye maeneo yao.
0 maoni:
Chapisha Maoni