Alhamisi, 26 Januari 2017

RC MOROGORO AZIAGIZA HALMASHAURI KUSIMAMIA MRADI WA ‘THAMINI UHAI’

Posted by Esta Malibiche on JAN 27,2017 IN NEWS

TUKIO 1

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro DKT.Stephen Kebwe wa kwanza kulia aliyesimama katika hafla ya kukabidhi hati ya makubaliano ya mradi wa thamini Uhai.

TUKIO

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro,Frank Jacob akisaini hati za makubaliano.

TUKIO 2

Mwakilishi wa Mradi wa Thamini Uhai akikabidhi hati za Makabidhiano Kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro DKT.Stephen Kebwe.
Mkuu wa Mkoa  wa  Morogoro Dkt. Stephen Kebwe,  ameziagiza Halmashauri za  Wilaya ya Ulanga, Kilombero na Malinyi kuendelea kusimami shughuli zote zilizokuwa zinasimamiwa na Mradi wa “Thamini Uhai” ili kuendelea kuboresha huduma kwa akina mama waja wazito  na watoto katika Wilaya hizo.

Dkt. Kebwe ametoa agizo hilo Januari, 26 mwaka huu katika Uwanja wa Mapinduzi  Mjini Mahenge wakati akikabidhiwa mradi wa Tuthamini Uhai mradi ambao sasa utasimamiwa na Mkoa ukishirikiana na Halmashauri zilizotajwa  hapo juu.

Amesema, Mradi wa Thamini Uhai unaolenga kupunguza  vifo vya akina mama vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto wachanga, umekuwepo Mkoani Morogoro kwa takribani miaka tisa sasa huku ukiwa na mafanikio makubwa kwa afya za akina mama waja wazito na watoto.

Mkuu wa Mkoa huyo amesema, kuna umuhimu  sasa kwa Halmashauri hizo kusimamia vema shughuli zote zilizokuwa zinafanywa na Mradi wa Thamini Uhai ili kuendelea kutoa huduma hiyo kwa makundi yaliyotajwa.

“Naagiza  kila Halmashauri kuendelea kusimamia yale yote ambayo yalishaanzishwa na Mradi wa Thamini Uhai” alisema Dkt. Kebwe.   “Naagiza kila Halmashauri kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya kununua dawa na vifaa tiba vya kutosha na kuhakikisha watumishi wa mradi huo wanapata mafunzo ya muda mfupi na muda mrefu ili kuboresha huduma zinazotolewa. “ alisisitiza Dkt. Kebwe.

Nae Mkurugenzi  Mtendaji wa mradi wa Tuthamini Uhai Dkt.  Nguke Mwakatundu amesema, shirika la Thamini Uhai ni shirika linaloshughullikia uhifadhi, uokoaji na uboreshaji wa akina mama wajawazito na watoto katika mikoa ya Kigoma, Pwani na Morogoro kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania.

Hata hivyo amesema hadi muda wa mradi wa shirika hilo unakwisha mafanikoa mengi yamejitokeza yakiwemo ya Kuwaokoa akina mama wajawazito na watoto. Hata hivyo ameitaka Serikali iendelee kuongeza juhudi katika kuendeleza mradi huo huku akiamini kuwa wanauacha mradi huo katika Mikono salama ya Serikali.

Hata hivyo Dkt. Mwakatundu amemueleza Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kuwa wataendelea kushirikiana na Serikali na wako tayari kutoa maelezo au kutoa utaalam wao wa utendaji kazi wa shirika hilo pale ambapo Serikali itahitaji.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Frank Jacob, akitoa maelezo mafupi ya mradi huo amesema, mradi umekuwa na mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya akina mama wanaokwenda kujifungua katika vituo vya Afya kwa idadi ya akina mama 800 mwaka 2008, hadi akina mama 4000 mwka 2015.

Vituo vya Afya ambavyo vilikuwa chini ya Mradi huo na ambavyo kulijengwa vyumba vya upasuajikwa ajili ya akina mama wajawazito ni pamoja na kituo cha Afya cha Mlimba kilichoko Wilayani Kilombero, Mtimbira Wilayani Malinyi na Kituo cha Afya cha Mwaya Wilayani Ulanga.

0 maoni:

Chapisha Maoni