Posted by Esta Malibiche on JAN 18,2017 IN NEWS
Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inapenda kutoa taarifa kwa umma, kuhusu
kuwepo kwa virusi vya mafua makali ya ndege katika nchi jirani ya
Uganda. Aidha taarifa hiyo imeeleza kuwa maeneo yalioathirika ni maeneo
yanayozunguka ziwa Victoria pamoja na ziwa lenyewe. Ugonjwa huu
umengundulika baada ya kuwepo kwa vifo vingi vya ndege pori katika
maeneo ya Lutembe beach, Masaka, Kachanga, Bukibanga na Bukakata ya
nchini Uganda. Vilevile, vifo hivi vimetokea kwa baadhi ya ndege
wafugwao (kuku na bata) na inahisiwa kuwa ndege hao wamepata virusi vya
ugonjwa huo kutoka kwa ndege pori wanaohama kutoka nchi za Ulaya. Vifo
hivyo vya ndege pori vilianza kuonekana tangu tarehe 2 Januari, 2017 na
vimeonekana kuendelea hadi sasa. Kwa hapa nchini Tanzania hakuna vifo
vya ndege vilivyoripotiwa hadi sasa.
Kwa kuwa hadi sasa hakuna
binadamu yeyote aliyeonekana kuwa na dalili za ugonjwa huo huko nchini
Uganda, tahadhari inatolewa kwa kuwa kuna uwezekano mkubwa wa ugonjwa
kusambaa kwa binadamu ikiwa hatua madhubuti za kujikinga
hazitazingatiwa.
UGONJWA WA MAFUA YA NDEGE
Ugonjwa huu unasababishwa na
virusi vya aina ya “Influenza” na huenezwa na ndege pori wanaohama hama
(Migratory birds). Ndege hawa hubeba virusi vya ugonjwa huu bila ya
kuonesha dalili za ugonjwa, hivyo huweza kuambukiza ndege wanaofugwa
majumbani mfano kuku na bata wakati wanapokutana nao. Aidha ndege hao
huweza kuambukiza ugonjwa huu kwa kupitia njia ya kinyesi ambacho
hudondoshwa ardhini au kwenye mabwawa na madimbwi ya maji.
Binadamu anaweza kuambukizwa
ugonjwa huu kwa kugusana na ndege au kinyesi cha ndege aliyeathirika na
ugonjwa huu. Hivyo ni muhimu kutokugusa mizoga ya ndege pori au kinyesi
chake. Maambukizi ya ugonjwa huu yanaweza pia kutoka kwa ndege pori na
kuathiri jamii ya kuku na bata na ndege ambao wanafugwa nyumbani. Hivyo
wananchi wanaombwa pia kutoa taarifa iwapo wataona dalili zozote za
ugonjwa na vifo katika jamii ya ndege hawa wa kufugwa pamoja na ndege
pori. Aidha, iwapo kutakuwa na maambukizi kwa jamii ya ndege hawa wa
kufugwa, binadamu anaweza pia kupata maambukizi wakati wa kuchinja kuku,
kunyonyoa manyoya, na wakati wa kutayarisha kabla ya kumpika.
Vilevile kuna uwezekano wa
virusi hivi kuambukizwa kutoka kwa binadamu mwenye uambukizo kwenda kwa
binadamu mwingine na hii ikitokea inaweza kusababisha mlipuko mkubwa
unaoweza kusambaa pande zote za dunia (Influenza Pandemic).
Maambukizi ya binadamu kwenda
binadamu mwingine hutokea kwa njia ya kugusana na maji maji ya kutoka
njia ya hewa iwapo mgonjwa atakohoa au kupiga chafya bila kufunika pua
au mdomo, au kwa njia ya kugusa sehemu zenye virusi zilizochafuliwa na
mgonjwa na mtu huyo kujigusa mdomomi au puani.
Dalili za ugonjwa wa mafua ya
ndege ni pamoja na; homa kali, kutokwa na makamasi mepesi pamoja na
mafua, kuumwa na kichwa, kukohoa, vidonda kooni, kupumua kwa shida na
vichomi. Vilevile baadhi ya wagonjwa wanaweza kuwa na dalili kama
kuharisha, kutapika, kuumwa na tumbo na kutokwa na damu puani na kwenye
ufizi.
HATUA ZINAZOCHUKULIWA NA WIZARA KATIKA KUZUIA UGONJWA HUU USIINGIE NCHINI
Kuanzia mwaka 2007, nchi yetu
imekuwa katika tahadhari ya ugonjwa wa mafua makali ya ndege na iliandaa
Mpango Mkakati wa Kuzuia na kudhibiti ugonjwa wa mafua makali ya Ndege,
ambao ndio ulitumika kuboresha utayari wa nchi na kuweza kufanikisha
kudhibiti mafua makali ya nguruwe yaliyokuwa tishio duniani mwaka 2009.
Aidha, mnamo mwaka 2012, Wizara kwa kushirikiana na Sekta za Mifugo,
Maliasili na Taasisi za Utafiti za NIMR na TAWIRI, chini ya uratibu wa
Ofisi ya Waziri Mkuu iliweza kuandaa Mpango Mkakati wa miaka 5 wa
Kudhibiti na Kuzuia magonjwa ya binadamu yanayoweza kutoka kwa wanyama,
na mpango huu unatekelezwa hadi sasa. Kufuatia tishio la ugonjwa huu ,
mpango huu utatumika pia katika kutekeleza afua zilizoanishwa ili
udhibiti ugonjwa huu usiingie nchini.
Vile vile hatua zifuatazo zimechukuliwa baada ya kupata taarifa ya tahadhari ya ugonjwa huu hapo jana 16 Januari 2017;
Kushirikiana na ofisi ya uratibu
wa magonjwa yanayowapata binadamu na wanyama (Zoonotic Diseases)
iliyoko chini ya ofisi ya Waziri Mkuu (One Health Coordination Office),
ambapo mkutano maalum umepangwa kufanyika tarehe 18 Januari 2017 ili
kuweza kukutanisha wadau wote na hivyo kuandaa Mpango kazi wa namna ya
kuzuia na kudhibiti ugonjwa huu.
Barua za tahadhari za ugonjwa
huu zimepelekwa kwa Makatibu Tawala wa mikoa yote ya Tanzania Bara
pamoja na . Fact Sheet (Ainisho Sanifu) za namna ugonjwa huu unavyoweza
kuenezwa, kudhibitiwa pamoja na namna ya kutambua ugonjwa huu
Kupitia kwa Waganga Wakuu wa
Mikoa na Wilaya, Wizara imetoa maelekezo ya kuimarisha mfumo wa
ufuatiliaji na utambuzi wa magonjwa (Surveillance) katika vituo vya
kutolea huduma nchini kote. Aidha katika vituo maalum ambapo ufuatiliaji
wa karibu umekuwa unafanyika kwa miaka kadhaa sasa, yaani katika mikoa
ya Mwanza, Kigoma, Arusha, Manyara, Dodoma, Dar es salaam na Mtwara,
tumeimarisha usimamizi wa ufuatiliaji wa karibu na kuelekeza kuwa kwa
sasa wagonjwa wote wanoonekana kuwa na dalili zinazofanana na mafua
makali ya influenza wachukuliwe sampuli ambazo zitapimwa kwenye maabara
ya Taifa ya NHLQATC ambayo ina uwezo wa kufanya utambuzi huo.
Kuimarisha ufuatiliaji wa
ugonjwa pia katika viwanja vya ndege, mipakani pamoja na bandari ili
kubaini wagonjwa waingiao nchini wakiwa na dalili za ugonjwa huo.
Wizara pia inaandaa Timu kwa
kushirikiana na Wizara ya Mifugo ili timu hii ya Taifa iweze kwenda
kujenga uwezo wa kamati za kudhibiti milipuko ya mgonjwa na majanga
hususani kwenye mkoa wa Kagera na mkoa wa Mwanza. Aidha Timu hii pia
itashirikiana na Timu za Mikoa kuandaa Mpango Mkakati wa Kudhibiti
Ugonjwa huu usiingie ikiwa ni pamoja na kuainisha maeneo ya kuboresha
ikiwemo upatikanaji wa vifaa kinga (Personal Protection Equipment, PPE)
Ili kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huu jamii inaaswa kuzingatia yafuatayo:
Kutoa taarifa endapo wataona
kutokea kwa vifo vya ndege pori au wafugwao (kuku, bata na wengineo)
kwa wataalamu wa mifugo, afya au ofisi ya serikali iliyo karibu nawe
Kutokugusa mizoga au ndege wagonjwa bila kutumia vifaa kinga
Kuepukana na tabia ya kuishi nyumba moja na ndege wafugwao
Kuepuka kuchinja kuku au bata wanaoonyesha dalili yoyote ya ugonjwa
Kunawa mikono vizuri kwa kutumia sabuni
Kupika nyama au mayai ya ndege kwa muda mrefu usiopungua nusu saa. .
Kuepuka kushika ndege wa porini na ndege wa majumbani wanaohisiwa kuwa na ugonjwa huu.
Hitimsho
Serikali inasisitiza kuwa mpaka
sasa ugonjwa wa mafua ya ndege haujaingia hapa nchini ila upo katika
nchi jirani ya Uganda katika jamii ya ndege pori kwa sasa. Kwa kuwa
magonjwa hayaangalii mipaka, tunahitaji kuchukua tahadharii madhubuti
ili kuzuia ugonjwa huu usiingie hapa nchini. Hivyo Wananchi wanahimizwa
kuzingatia kanuni za afya za kuzuia ugonjwa huu ikiwa ni pamoja na kutoa
taarifa mara moja waonapo vifo vya ndege au kuku. Pia wanatakiwa
kuripoti haraka kwenye vituo vya kutolea huduma za afya mara waonapo
dalili zozote za ugonjwa huu. Vile vile wananchi wanatakiwa kutokuwa na
hofu kwani Serikali imejiandaa na itachukua hatua madhubuti za kudhibiti
ugonjwa huu.
Mhe. Ummy Mwalimu (Mb)
Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wazee na Watoto.
Tarehe 18 Januari, 2017
0 maoni:
Chapisha Maoni