MKUU wa Mkoa wa Iringa,
Amina Masenza amecharuka na kutoa onyo kali kwa watendaji wa serikali
wanaoshindwa au kupuuza utekelezaji wa maagizo yanayotolewa kwao kwa njia
mbalimbali yakiwemo mafunzo.
“Sitaki longolongo
ziendelee, taarifa zenu za utendaji mnazoandika mkiwa mmekaa kwenye madawati
yetu ofisini ni marufuku. Asiyetaka kutekeleza majukumu ya serikali kwa vitendo
aseme ili tumuondoe,” Masenza alisema.
Aliyasema hayo juzi mjini
Iringa kwenye kikao maalumu cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kilichopokea na
kupitia taarifa ya hali ya upatikanaji na utumiaji wa huduma za kifedha mkoani
Iringa.
Taarifa hiyo
iliwasilishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Kuendeleza Hudumza ya Fedha
Tanzania (FSDT), Sosthenes Kewe.
Masenza alisema taarifa
za utafiti wa kutambua na kupima mahitaji na upatikanaji wa huduma za fedha
miongoni mwa wananchi zina umuhimu mkubwa kwa maendeleo yahusuyo upatikanaji wa
huduma jumuishi za fedha.
“Kwahiyo watendaji wa
serikali wa ngazi zote mnatakiwa kuzitumia taarifa za tafiti hizo kuboresha
upatikanaji na utumiaji wa huduma za fedha katika maeneo yenu,” alisema.
Awali Mkurugenzi
Mtendaji wa FSDT, Kewe alisema; “tumekutana na wajumbe wa RCC wa mkoa wa Iringa
tukilenga kutoa taarifa ya upatikanaji na utumiaji wa huduma za fedha katika
mkoa na kupima kama wanatakwimu za kutosha zinazosaidia kufanya maamuzi
mbalimbali ya kisera.”
Alisema utafiti wa mwaka
2013 uliofanywa na taasisi ya FinScope, unaonesha Iringa ni mkoa wa pili nchini
baada ya Dar es Salaam kwa kutumia huduma za kibenki na wa tano kwa kutumia huduma
za fedha.
Alisema hali halisi ya
upatikanaji na utumiaji wa huduma hizo unazingatia upatikanaji wa fursa nyingi
za kiuchumi kikiwemo kilimo na ufugaji.
Ili kuboresha taarifa za
upatikanaji na utumiaji wa hudumia hizo, Kewe alisema FinScope itafanya utafiti
mwingine mwaka huu ili matokeo yake yatumike kupanga mipango ya kuboresha
maeneo mbalimbali ya kisera katika ngazi ya serikali za mitaa.
“Tumechagua mikoa mitatu
ya Iringa, Rukwa na Mwanza ambayo uchambuzi wa utafiti huo utakaofanywa mapema
mwaka huu utatoa picha halisi ya upatikanaji wa huduma hizo kiwilaya na mikoa
mingine inayobaki uchambuzi wake utakuwa wa ngazi ya mkoa,” alisema.
Alisema wamechagua
Iringa kwasababu ya fursa kubwa ya kilimo waliyonayo, Rukwa kwasababu hauna
huduma za kutosha za kifedha na Mwanza watakakofuatilia kwa kina shughuli za
ujasiriamali.
Katibu Tawala wa Mkoa wa
Iringa, Wamoja Ayubu alishukuru mkoa wa Iringa kuingizwa katika mikoa mitatu
ambayo uchambuzi wa utafiti huo utafanywa hadi kwa ngazi ya wilaya.
“Takwimu
zikichanganuliwa kiwilaya, itatusaidia kujipanga na kujiwekea mikakati ya
makusudi katika maeneo yote yatakayoonekana yana mahitaji zaidi ya huduma hizo,”
alisema.
0 maoni:
Chapisha Maoni