posted by Esta Malibiche on JAN 31,2017 IN NEWS
Na: Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma
Katika bajeti ya mwaka 2016/17,
Serikali imetenga shilingi bilioni 13.9 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za
walimu 1,157 wa shule za msingi nchini.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo ameyasema
hayo leo, Mjini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge Viti Maalum,
Mhe. Juliana Daniel Shonza juu ya mpango wa kuboresha miundombinu ya
elimu vijijini kama vile nyumba za walimu pamoja na kulipa malimbikizo
ya madeni ya walimu.
“ Katika bajeti ya mwaka 2016/17,
Serikali imetenga shilingi Bil. 13.9 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za
walimu 1,157 kwa shule za msingi na shilingi bilioni 11.14 zimetengwa
kwa ajili ya ujenzi wa nyumba 661 kwa shule za sekondari,” alifafanua
Jafo.
Aliendelea kwa kusema kuwa,
Serikali kupitia Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMESII)
imekamilisha ujenzi wa nyumba 146 kati ya nyumba 183 ambazo kila nyumba
wataishi walimu Sita (6 multi-unit houses).
Aidha ameeleza kuwa ujenzi wa
nyumba hizo umegharimu shilingi bilioni 21.9 ambapo nyumba 37
zinaendelea kujengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 5.5 na zinategemea
kukamilika tarehe 30 Aprili, 2017.
Kuhusu ulipaji wa madeni ya
walimu, Jafo amesema kuwa Serikali imeendelea kulipa madeni kadri
yanavyojitokeza na kuhakikiwa ambapo katika mwezi Oktoba, 2015 Serikali
ililipa madeni ya shilingi bilioni 20.12 kwa walimu 44,700 na shilingi
bilioni 1.107 zililipwa mwezi February, 2016 kwa walimu 3221.
0 maoni:
Chapisha Maoni