Jumanne, 3 Januari 2017

CCM KIBAHA MJINI YAJIPANGA KUSHINDA UCHAGUZI MDOGO KATA YA MISUGUSUGU

Posted by Esta mMalibiche on JAN 3,2017 in


Wajumbe wa halmashauri kuu ya CCM ,Kibaha Mjini wakifuatilia jambo katika kikao cha halmashauri hiyo kilichokaa ili kujiwekea mikakati ya ushindi katika uchaguzi mdogo  wa kata ya Misugusugu,ambapo desemba 31 /2016 CCM inatarajia kuzindua kampeni zake rasmi.(picha na Mwamvua Mwinyi) 

Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
CHAMA cha Mapinduzi(CCM) Kibaha Mjini ,kimejipanga kushinda katika uchaguzi mdogo wa udiwani kata ya Misugusugu ambapo chama hicho kinatarajia kuzindua rasmi kampeni zake  des 31 mwaka huu.

Uchaguzi huo unarejea kwasababu march 31/ 2016,mahakama ya mkoa wa Pwani ilitengua uteuzi wa diwani wa chama hicho Addhudad Mkomambo ambae alishinda katika uchaguzi mkuu uliopita.
Aidha katika uzinduzi huo mwenyekiti wa CCM mkoani Pwani,Mwinshehe Mlao anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Katibu wa CCM Kibaha Mjini,Abdallah Mdimu ,aliyasema hayo katika kikao cha halmashauri kuu ya CCM wilaya ,kilichokaa ili kujiwekea mikakati madhubuti ya kupata ushindi kwenye uchaguzi huo.
Alieleza kwamba uchaguzi huo ulitenguliwa kutokana na namba saba kuzidi kwa hesabu kati ya waliopiga kura na kura walizopata wagombea wa vyama vyote hivyo mahakama kufanya maamuzi hayo ili kujiridhisha.
“Wapiga kura wote walikuwa 4,830,waliopiga kura 3,191,huku katika matokeo CCM ilipata kura 1,545,chadema 1,525,ACT 66 na CUF 55 "
"Ambapo kura saba hazikujulikana ni za nani kati ya zilizopigwa na matokeo hivyo mahakama kuamua kutengua ushindi wa awali”alisema Mdimu.


Mdimu alisema chama hicho kimejipanga vizuri na tayari wameshazunguka katika matawi yote nane yaliyopo katika kata hiyo ili kuhakikisha kiti hicho kinarudi kwa CCM.

Hata hivyo ,katibu huyo alisema ,mgombea mteule wa nafasi ya udiwani kupitia CCM katika kata ya Misugusugu,amechaguliwa kuwa ni Ramadhani Bogas ambae alishinda katika kura za maoni na kisha kupitishwa kwenye vikao mbalimbali vya wilaya na mkoa . 



Alibainisha kuwa Ramadhani Bogas hivi karibuni alishinda kwenye kura za maoni zilizopigwa ndani ya chama hicho na kuwashinda wenzie saba ambao walijitokeza kugombea akiwemo diwani wa awali wa kata hiyo Addhudad Mkomambo .



Nae katibu wa CCM mkoani Pwani,Haji Hassan Mtenga,aliwataka wanachama wa chama hicho kuwa wamoja na kuondoa makundi yasiyo na tija ndani ya chama.


Aliwaambia kwamba ni wakati wa kutunza wajibu wao kwa ajili ya kushika dola na kuondokana na tofauti zao ambazo wakati mwingine huzaa maumivu .

Mtenga aliziomba jumuiya zote ziungane pamoja kujenga mipango na mikakati itakayowasaidia kuvuka katika uchaguzi huo mdogo na kupata ushindi.
Kwa upande wake mwenyekiti wa CCM Kibaha Mjini,Maulid Bundala aliwaomba wananchi hususan vijana kujiokeza kwa wingi katika uzinduzi wa kampeni hizo sambamba na kumpigia kura mgombea kupitia CCM siku ya kupiga kura.
Aliwataka wanaCCM kuacha kujibweteka na kusubiri ushindi uje miguuni pasipo kupigana kufa na kupona ili ushindi upatikane.
“Hapa ni kazi kazi,ipo kazi ya ziada ya kufanya ,kumbukeni hakuna ushindi unaokuja kwa kubahatisha na hakuna mashindano rahisi,tusidharau tupambane kwa lengo la kurejesha nafasi hiyo mikononi mwa CCM”alisema Bundala.
Bundala alisema maendeleo yanapatikana ndani ya chama kubwa CCM ,na haina ubishi ,kwani kila mmoja naona namna serikali ya awamu ya tano kupitia CCM inavyofanyakazi na kuinua uchumi kwa kasi nchini.

0 maoni:

Chapisha Maoni