Jumatatu, 30 Januari 2017

WATANZANIA WAOMBWA KUMUUNGA MKONO RAIS DK.JOHN MAGUFULI

Posted by Esta Malibiche on JAN 30,2017 IN NEWS

 Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini, John Shibuda (katikati), akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano wa kuuaga mwaka wa 2016 na kuukaribisha mwaka 2017 Dar es Salaam jana. Kulia ni Msajili Msaidizi Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini, Sisty Nyahoza na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ADA na Waziri wa Nchi asiye na Wizara Maalum, Zanzibar.

 Mkutano ukiendelea.
 Waandishi wa habari wakiwa kwenye mkutano huo.
Mwanahabari Suleiman Msuya akiuliza swali katika mkutano huo.
 
WATANZANIA wameombwa kumuunga mkono Rais Dk.John Magufuli kwa jitohada zake anazozifanya za kupongoza nchi.
 
Mwito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini John Shibuda wakati akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano wa kuuaga mwaka wa 2016 na kuukaribisha mwaka 2017 Dar es Salaam jana.
 
Alisema Serikali ya awamu ya tano imekuwa ikifanyakazi kubwa ya kudhibiti mirija ya unyonyaji wa pato la Taifa kupitia watumishi hewa, wanafunzi hewa, kaya masikini bandia na kupitia wahujumu uchumi wa matumizi mabaya ya dhamana za Taifa mambo ambayo yalikuwa yakipigiwa kelele na vyama vya upinzani.
 
“Binafsi nawaomba watanzania bila ya kujali itikadi za vyama vyao kumuunga mkono Rais wetu Dk.John Magufuli na wasaidizi wake Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na wengine wote kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuongoza Taifa letu la Tanzania” alisema Shibuda.
 
Alisema anaupongeza utumishi wa Serikali ya awamu ya tano kwa uzinduzi wa urejeshaji wa uwajibikaji wa watumishi wote kwani hivi sasa watumishi wengi wanatabia za miiko ya utiifu kwa umma.
 
Akizungumzia Zanzibar alisema uchaguzi umekwisha pita na Rais wa nchi hiyo ni Dk. Ali Mohammed Shein ambaye anatakiwa kuongoza nchi hiyo na wenzake waliochaguliwa ili kuiletea maendeleo Zanzibar hivyo siasa za mihemuko ziachwe.
 
Shibuda alitumia nafasi hiyo kuwapongeza wazanzibar hasa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa ushindi walioupata Jimbo la Dimani na kuwaomba walioshindwa wasivunjike moyo kuvunjika jembe siyo mwisho wa uhunzi kwani hata timu kubwa hufungwa na timu ndogo.
 
Akizungumzia katazo la vyama vya siasa kutofanya mikutano hadi mwaka 2020 alisema majibu ya suala hilo yatatolewa baadae baada ya kulifanyia kazi jambo hilo. 
 
Katika hatua nyingine Shibuda alisema Baraza la Vyama vya Siasa litakuwa mshirika rafiki wa wadau wote wa siasa na kusimamia maslahi mapana ya jamii na Taifa yanayosimamiwa na Serikali na kuungwa mkono na Bunge mfano Azimio la EPA.
 
Shibuda alitoa ushauri kwa vyama vyote vya upinzani kuzingatia umakini wa mabadiliko ya Tabia nchi ya mfumo wa uwajibikaji wa Serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli.
 

0 maoni:

Chapisha Maoni