Posted by Esta Malibiche on JAN 19,2017 IN NEWS
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Aloyce Nzuki (kulia) akisalimiana na Mwenyekiti
wa Kamati ya Bunge Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhandisi Atashasta
Nditiye baada ya kuwasili makao makuu ya Wizara hiyo Mpingo House Jijini
Dar es Salaam jana huku akiongozana na wajumbe wa kamati hiyo.
Waziri
wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (wa tatu kushoto)
akizungumza katika kikao cha Kamati ya Bunge, Ardhi, Maliasili na Utalii
katika ukumbi wa Ngorongoro wizarani hapo jana. Kutoka kulia ni Naibu
Waziri wa Wizara hiyo, Mhandisi Ramo Makani, Makamu Mwenyekiti wa kamati
hiyo, Kemilembe Lwota, Mwenyekiti wa Kamati, Mhandisi Atashasta
Nditiye, Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali
Gaudence Milanzi na Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Aloyce Nzuki.
Kikao kikiwa kinaendelea katika ukumbi wa Ngorongoro, Makao Makuu ya Wizara hiyo, Mpingo House, Jijini Dar es Salaam.
Kaimu
Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha Kupambana na Ujangili wa Idara ya
Wanyamapori, Bw. Robert Mande akiwasilisha taarifa kuhusu taratibu za
uhifadhi wa ghala la meno ya tembo kwa Kamati ya Bunge, Ardhi, Maliasili
na Utalii katika ukumbi wa Ngorongoro makao makuu ya Wizara hiyo Jijini
Dar es Salaam leo.
Baadhi
ya wajumbe wa kamati ya bunge Ardhi, Maliasili na Utalii katika kikao
hicho. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu, Maliasili na Utalii, Dkt. Aloyce
Nzuki.
Baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo.
Baadhi ya wakurugenzi wa Idara katika Wizara ya Maliasili na Utalii, wakifuatilia mjadala kwenye kikao hicho.
Baadhi ya wajumbe wa Kamati hiyo ya Bunge.
Baadhi ya wajumbe wa Kamati hiyo ya Bunge.
NA HAMZA TEMBA - WMU
...........................................................................
...........................................................................
Kamati
ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imetembelea makao makuu ya Wizara ya
Maliasili na Utalii, Mpingo House jijini Dar es Salaam leo na kuzuru ghala la nyara
za Serikali kuona utunzaji wa meno ya tembo na changamoto zake.
Kabla ya
kutembelea ghala hilo kamati hiyo ilipokea taarifa maalum ya wizara juu ya
mchakato mzima wa taratibu za ukusanyaji wa meno ya tembo, usafirishaji, uhakiki,
usajili kwenye mfumo maalum wa kielektroniki, uhifadhi wake na ulinzi thabiti
wa ghara hilo.
Akizungumza
wakati wa kuwasilisha taarifa hiyo, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha
Kupambana na Ujangili wa Idara ya Wanyamapori, Bw. Robert Mande alisema meno
yanayohifadhiwa katika ghala hilo ni yale yanayotokana na vifo asilia, kuuawa
kutokana na uharibifu wa mali na maisha ya binadamu na yale yanayotokana na
ujangili.
Waziri
wa Maliasili na utalii, Prof. Jumanne Maghembe akijibu moja ya swali la wajumbe
wa kamati hiyo ambao walitaka kujua uwezekano wa kuuza meno hayo ya tembo
yaliyohifadhiwa ili kulipatia taifa mapato, amesema msimamo wa Serikali
ya Tanzania kwa sasa sio wa kuuza wala wa kuchoma meno hayo.
"Msimamo
wetu ni kama ule wa nchi za Kenya, Uganda, Zambia, Malawi na Msumbiji wa
kutokuuza meno haya kwa sasa kwasababu mbalimbali za kimsingi kabisa, moja
ikiwa ni sababu za kiutafiti ambapo vinasaba vya meno ya zamani vinaweza
kutumika kubaini mambo mbalimbali ikiwemo utafutaji wa dawa ya magonjwa ya tembo”,
alisema.
Alisema
kitendo cha kuuza meno hayo pia ni kuchochea zaidi biashara hiyo kwakuwa
kitaongeza upatikanaji wa bidhaa hiyo kwenye masoko hivyo kuendelea kuipa uhai
biashara hiyo haramu duniani.
Hapo awali, Katibu
Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Generali, Gaudence Milanzi akizungumza kwenye kikao
cha kamati hiyo mkoani morogoro kilichohusisha uongozi wa Mamlaka ya Usimamizi
wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) alisema ujangili hapa nchini kwa sasa umepungua
kwa kiasi kikubwa na kwamba nyara zinazokamatwa kwa sasa ikiwemo meno ya tembo ni
za zamani zilizokuwa zikisubiria kusafirishwa nje ya nchi.
Alisema hatua
hiyo ya kupungua kwa uhalifu huo imefanikiwa kutokana na kazi kubwa inayofanywa
vikosi maalum vya Askari wa wanyamapori vya kudhibiti ujangili kwa kushirikiana
na vyombo vingine vya ulinzi na usalama nchini.
Alisema hatua
ya Serikali ya China kupiga marufuku biashara ya meno ya tembo nchini humo ni
jambo la kupongezwa na kwamba uamuzi huo utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza msukumo
wa vitendo vya ujangili nchini na barani Afrika kwa ujumla.
Naye
mwenyekiti wa kamati hiyo ya bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhandisi
Atashasta Nditiye amewapongeza viongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii namna
walivyojipanga katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara hiyo na kuwaahidi
ushirikiano kutoka kwa kamati yake.
Aliahidi kutoa ushirikiano kwa uongozi wa wizara hiyo katika kuhakikisha
kuwa wanaikabili changamoto kubwa ya uvamizi wa mifugo kwenye maeneo ya hifadhi. "Sisi tunaungana na nyie,
hatukubali mifugo kwenye hifadhi zetu, kwakuwa zinaharibu ubora wa hifadhi
hizo, tunawaahidi ushirikiano wa kukabiliana ma changamoto hiyo"
Kamati hiyo
ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii ilitembela pia makao makuu ya Wakala ya
Mbegu za Miti Tanzania (TTSA), Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA) na
Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) zote za mkoani Morogoro.
0 maoni:
Chapisha Maoni