Posted by Esta Malibiche on JAN 16,2017
Wanafunzi wa Shule ya Msingi ya
Mtakatifu Therese wakitoa heshima za mwisho mbele ya jeneza lenye mwili
wa mwanafunzi mwenzao Maria Masala wakati wa ibada ya kuuaga mwili huo
iliyofanyika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Therese Ukonga Madafu Dar es
Salaam jana.
Jeneza lenye mwili wa mtoto huyo likiombewa kabla ya
kuingizwa kanisani
Wanafunzi wenzake na mtoto huyo wakiwa katika ibada ya kumuaga mwenzao.
Padre aliyekuwa akiendesha ibada hiyo akilinyunyuzia mafuta ya baraka jeneza lenye mwili wa mtoto Maria.
Msemaji wa familia ya ASP Masala akitoa taarifa na historia
fupi ya marehemu Maria.
Baba wa marehemu, ASP Masala (wa pili
kulia aliyevaa shati la kitenge), akiwa na ndugu zake na waumini
waombolezaji katika ibada ya kuuaga mwili wa mtoto wake kabla ya
kuondoka kwenda nyumbani kwao mkoani Rukwa kwa mazishi.
Padre aliyekuwa akiendesha ibada hiyo akilinyunyuzia mafuta ya baraka jeneza lenye mwili wa mtoto Maria.
Watawa wa Kanisa Katoliki la Mtakatifu Therese wakitoa
heshima za mwisho.
Waombolezaji wakiwa wamejipanga foleni wakati wakienda
kutoa heshima za mwisho.
Waombolezaji wakiwa katika foleni ya kutoa heshima za mwisho.
Mtawa wa kanisa hilo akisaidiwa baada ya kushindwa kuvumilia uchungu wa kuondokewa na mpendwa wake mtoto Maria.
Ngugu yake Maria akisaidiwa baada ya kutoa heshima
zake za mwisho.
Baba ya mtoto huyo ASP Masala akilia kwa uchungu wakati
akitoa heshima zake za mwisho kwa mwanaye.
Waombolezaji wakiwa wamebeba jeneza lenye mwili wa mtoto Maria wakati wakitoka katika kanisa hilo.
Jeneza likiingizwa katika gari tayari kwa safari ya kwenda
mkoani Rukwa kwa mazishi.
Waombolezaji wakiwa wamepigwa na bumbuwazi
kufuati vifo hivyo.
Ni huzuni na simanzi wakati wa kuuaga mwili wa mtoto huyo.
Na Dotto Mwaibale
WINGU zito vilio majonzi na simanzi
vilitanda kutokana na vifo vya watoto wawili wa maofisa wa Jeshi la
Magereza waliofariki dunia kwa kukosa hewa baada ya kujifungia kwenye
gari la mmoja wa wazazi wao walimokuwa wakicheza.
Tukio hilo limetokea juzi jioni katika
Kota za Magereza Ukonga jijini Dar es Salaam, wakati wazazi wao
walipokuwa wakitengeneza gari hilo lililogoma kuwaka.
Watoto waliopoteza maisha ni mtoto wa
Mrakibu wa Jeshi la Magereza (ASP), Demetrus Masala, aitwaye Maria (6),
ambaye alikuwa darasa la kwanza katika Shule ya Mtakatifu Therese Ukonga
na Sajini Francis, ambaye ni Esther (4), mwanafunzi wa shule ya awali
katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo
ambao hawakupenda majina yao yaandikwe kwenye vyombo vya habari kwa
sababu si wasemaji wa familia walidai kuwa watoto hao walipoteza maisha
katika gari lenye namba ya usajili T 291 CXR aina ya Toyota Passo ,mali
ya ASP Masala.
Mashuhuda hao walidai kuwa siku ya tukio
gari hilo liligoma kuwaka na ndipo Masala alipokwenda kumuomba jirani
yake ambaye anaishi mlango wa pili Sajini Francis aende kumsaidia
kulibusti ambapo alichukua betri katika gari yake ili amsaidie jirani
yake huyo.
Ilielezwa kuwa licha ya kuibusti betri
ya gari la ASP Masala haikupokea moto ikiashiria kuwa Alternator
ilikuwa ni mbovu kwani ilikuwa haifui umeme.
Baada ya kushindikana kuiwasha gari hilo
waliamua kuachana nalo na kushauriana ASP Masala aende kumfuata fundi
na ndipo alipolifunga gari lake na kuondoka pasipo kujua watoto wao
walikuwa ndani ya gari hilo kwani walipokuwa wakilitengeneza walionekana
wakiwa pembeni yake.
Wazazi hao hawakujua watoto hao
waliingia saa ngapi ndani ya gari hilo lakini ilidaiwa kuwa awali wakati
wakicheza jirani na gari hilo waliwafukuza ambapo baadae waliingia tena
bila ya wao kufahamu hasa kutokana na gari hilo kuwa na vioo vya giza
isipokuwa cha mbele ambapo walikuwemo ndani ya gari hilo kuanzia saa 7
mchana hadi saa 11 jioni.
Ilidaiwa kuwa baada ya kukaa kwa muda
mrefu Francis ambaye ni dereva ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
alibaini watoto hao wawili hawaonekani katika eneo hilo ndipo walipoanza
kuwatafuta katika nyumba za jirani bila mafanikio.
Inadaiwa wakati wakiendelea kuwatafuta
kuna kijana aliwadokeza kuwa wakati gari hilo likiendelea kutengenezwa
watoto hao walikuwa ndani ya gari hilo.
Kauli hiyo inadaiwa ndiyo iliyomshtua
Francis na kuamua kuchungulia ndani ya gari hilo ambapo waliwaona watoto
hao wakiwa wamekaa siti ya nyuma wamelala fofofo huku mwingine akivuja
damu puani.
Hali hiyo ilisababisha Francis na watu
wengine waliokuwepo eneo hilo kusogea na kuvunja kioo kidogo cha gari
hilo na kuwatoa watoto hao wakiwa katika hali mbaya.
Imedaiwa kwa sababu ya hali waliyokuwa
nayo waliamua kuwakimbiza katika Hospitali ya Kardinal Rugambwa Ukonga
kwa ajili ya matibabu ya haraka lakini hata hivyo walibaini mtoto Maria
tayari alikuwa amekwisha fariki dunia.
Madaktari walijaribu kumpa huduma ya
kwanza mtoto Esther kwa kumuongezea Oksjeni na baadaye walimkimbiza
Hospitali ya Mkoa wa Ilala ya Amana ambapo naye walibaini kuwa tayari
alikuwa amekwisha fariki.
Baadhi ya waumini wa Kanisa Katoliki la
Ukonga la Mtakatifu Therese wakizungumza na wanahabari walielezea
kusikitishwa na tukio hilo, wakidai mtoto Maria juzi asubuhi walishiriki
naye Jumuiya ya Mtakatifu Maria Consolata ambayo ilifanyika nyumbani
kwao.
Walisema kwa nyakati tofauti mtoto huyo alishiriki na wazazi wake kupanga viti tayari kwa maandalizi ya jumuiya.
Mkazi mmoja wa eneo hilo alidai, kifo cha watoto hao ni pigo kwa wazazi hao ambao ni majirani na marafiki wa muda mrefu.
Imedaiwa kuwa wazazi hao kila mmoja
alikuwa na watoto wawili, wa kwanza wote wakiume na wapili wa kike ambao
ndio waliofariki katika tukio hilo la kusikitisha.
“ Kifo hiki kimeacha pengo kwani wote
wameondokewa na watoto wao wa pili kuzaliwa na wote ni wa kike wamebaki
wakiume tu…inauma sana na ni funzo kwetu kuwa tayari wakati wowote,”
ilielezwa.
Mwili wa mtoto Maria ulisafirishwa jana kwenda mkoani Rukwa kwa mazishi ambayo yanatarajia kufanyika kesho.
Hata hivyo inadaiwa mama mzazi wa Maria
hayupo jijini Dar es Salaam alisafiri kwenda Rukwa kwa ajili ya sherehe
za mwisho wa mwaka na bado yupo huko.
Familia ya Francis inatarajia kufanya mazishi ya mtoto wao Esther leo katika Makaburi ya Segerea, Ukonga.
Padre aliyeongoza ibada ya kuuaga mwili
wa mtoto Maria aliwataka wazazi na waumini wa kanisa Katoliki la
Mtakatifu Therese kutohusisha tukio hilo na imani potofu na kusema kila
binadamu anakuja duniani kwa mpango wa mungu na kuondoka kwa mpango wa
mungu ingawa vifo vya watoto hao ni vyakusikitisha hasa ukizingatia umri
wao mdogo waliokuwa nao na kuwa kazi ya mungu haina makosa.
Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa
Serikali ya Mtaa wa Mwembe Madafu, Deus Nchimbi alisema, kifo cha watoto
hao ni pigo kwa familia hizo marafiki.
“Kikubwa ni kuomba amani na kuwaombea
marehemu lakini watoto wamekufa kifo cha uchungu kwa kukosa hewa huenda
wangekuwa na wakubwa wangeweza kufungua gari,”alisema Nchimbi.
Alisema kilichobaki ni kuikumbusha jamii
kuwa makini na vyombo vya moto na kuwapa uhuru watoto waweze kufahamu
aina ya mali zilizopo nyumbani.
Changamoto kubwa iliyoibuka katika tukio
hilo ni kwa wazazi wote wa pande mbili kugoma kulizungumzia tukio hilo
kwa waandishi wa habari kwa madai kuwa wanaopaswa kulizungumzia ni
Jeshi la Magereza wakati suala hilo ni la kifamilia zaidi na linagusa
maisha ya kijamii.
"Tumepewa maagizo kutoka juu kuwa
waandishi wa habari hampaswi kuchukua taarifa hii kwani ndugu za
marehemu bado wanamajonzi hivyo subirini wakisha zika mje kuwahoji
wafiwa hayo ndiyo maagizo na jeshini hatuna kauli nyingi ni moja tu"
alisema ofisa mmoja wa jeshi hilo ambaye hakujitambulisha jina lake.
0 maoni:
Chapisha Maoni