Posted by Esta Malibiche on JAN 27,2017 IN NEWS
*Ni wale waliohusika na upotevu wa sh. milioni 700
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Njombe Bw. Christopher Ole Sendeka
kuwachukulia hatua watumishi Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa
waliohusika na upotevu wa fedha za maendeleo.
Amesema zaidi ya sh. milioni 700
zilizopelekwa katika halmashauri kwa ajili ya miradi mbalimbali ya
maendeleo zikiwemo sh. milioni 300 za ujenzi wa Ofisi ya Halmashauri
hiyo.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo jana
jioni (Alhamisi, Januari 26, 2017) wakati akizungumza na wananchi
katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Halmashauri
alipokuwa katika ziara yake katika Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe.
“Mkuu wa Mkoa watu wote
waliohusika na upotevu huu watafutwe popote walipo na kuchukuliwa hatua
na kisha nipewe taarifa ya hatua ulizochukua. Hatuwezi kuwavumilia watu
hao ambao wanachora ramani kwa sh milioni 200 na sh. milioni 100
zingine hazijulkikani zilipo,“ alisema.
Pia Waziri Mkuu alimuagiza Mkuu
huyo wa Mkoa kufuatilia kiasi kingine cha sh milioni 400 zilizopelekwa
wilayani hapo kwa ajili ya maendeleo ambazo nazo hazijulikani zilipo.
“Tafuta waliohusika popote walipo hata kama ni nje ya Njombe waje
kutueleza ziliko fedha zetu,”
Mbali na kutoa agizo hilo kwa
Mkuu wa Mkoa, pia Waziri Mkuu ameuagiza uongozi wa Taasisi ya Kupambana
na Kuzuia Rushwa nchini (TAKUKURU) kuhakikisha inashirikiana nayo
inafanya uchunguzi ili kubaini watu waliohusika na upotevu huo.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu
alisema Serikali haitowavumilia watumishi wote wanaojihusisha na
vitendo vya ubadhilifu wa fedha za umma, hivyo amewataka watumishi
wafanye kazi kwa kuzingatia sheria na maadili.
Waziri Mkuu aliwataka
watumishi wa umma nchini kuacha tabia ya kudokoa fedha za maendeleo
zinazopelekwa katika Halmashauri zao kwa sababu Serikali iko macho na
itawashughulikia wote watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo.
Aidha, Waziri Mkuu alitoa wito
kwa Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kusimamia vizuri fedha za
maendeleo zinazopelekwa kwenye maeneo yao na kuhakikisha zinatumika kama
ilivyokusudiwa.
Awali akiwa njiani kuelekea
Ludewa Mjini akitokea katika kata ya Mundindi Waziri Mkuu alisimamishwa
na wananchi wa kijiji cha Mlangali ambao waliiomba Serikali iwasaidie
kuzipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo ya maji.
Mwenyekiti wa kijiji hicho Bw.
Michael Lameck alisema alimueleza Waziri Mkuu kwamba awali walikuwa
wanapata maji ila kwa sasa hayatoki kutokana na uchakavu wa miundombinu
hali iliyowafanya kuchangishana na kupata sh. milioni 95 kati ya 200
zinazohitajika.
Kufuatia hali hiyo Waziri
Mkuu alimuagiza Mhandisi wa Maji wa Wilaya hiyo, Bw. Nasib Mlenge kwenda
kijijini hapo leo Januari 27 kukutana na Bw. Lameck ili kushirikiana
naye na kuangalia alipofikia na kuendeleza uboreshaji wa miundombinu
hiyo ili wananchi hao wapate maji.
“Mwenyekiti amechangisha sh.
milioni 95 na kununua baadhi ya vifaa nyinyi mnashindwa nini. Lazima
muwe makini na matatizo ya wananchi na Serikali haitaki masuala ya
urasimu. Watu wana shida ya maji na mnajua tatizo mmekaa tu,” alisema.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, JANUARI 27, 2017.
0 maoni:
Chapisha Maoni