Jumatatu, 16 Januari 2017

SOKO JIPYA LA MAILMOJA LATARAJIWA KUKAMILIKA MWEZI HUU,KWA GHARAMA YA MIL.424

Posted by Esta Malibiche on JAN 16,2017 in NEWS

Ofisa  habari  wa halmashauri ya Mji wa Kibaha, Innocent Byarugaba, akionyesha ramani  ya soko  jipya la  Mailmoja linalojengwa eneo la Mnarani ambapo baada ya kukamilika linatarajiwa kuwa na uwezo wa kuchukua wafanyabiashara 600.(Picha na Mwamvua Mwinyi)

Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
UJENZI wa soko jipya la Maili Moja wilayani Kibaha mkoani Pwani unatarajiwa kukamilika kabla ya kuvunjwa kwa soko lililopo sasa katika zoezi la bomoabomoa inayotarajiwa kufanyika  Jan 23 mwaka huu .
Soko hilo lipo katika hatua nzuri ya ujenzi ambapo linatarajiwa kugharimu zaidi ya sh.mil.424 hadi kumalizika kwake.
Aidha halmashauri ya Mji wa Kibaha ,imesisitiza kuwa zoezi la bomobomoa hiyo itagusa wafanyabiashara na wakazi waliojenga kwenye mita 60 badala ya 120  .
Akitolea ufafanuzi masuala hayo ,ofisa habari wa halmashauri ya Mji wa Kibaha,Innocent Byarugaba,alisema soko la sasa linavunjwa kutokana na kujengwa ndani ya hifadhi ya barabara kuu ya Dar es salaam-Morogoro.
Alieleza kwamba awali gharama zilizotengwa ilikuwa mil.200,hata hivyo gharama imeongezeka katika ujenzi wa jengo la wafanyabiashara wa nafaka mil.78,jengo la mama lishe mil.88.609.699,kifusi na kalavati mil.34.
Alitaja gharama nyingine kuwa ni zimeongezeka kwenye kuweka miundombinu katika hali ya usafi mil 9.001 na kazi za nyongeza mil.26 hivyo kufikia gharama ya mil.424.654.999.4.
“Soko hilo litakapokamilika litakuwa na uwezo wa kuchukua wafanyabiashara 600 ambao watatosha kufanya shughuli zao mbalimbali kwa nafasi.


“Ikumbukwe kuwa halmashauri iliamua kutenga eneo la Mnarani kwa ajili ya ujenzi wa soko la Maili Moja kwa wafanyabiashara kutokana na soko hilo kutarajiwa kuvunjwa na wakala wa barabara Tanzania (TANROADS)ili kupisha hifadhi ya barabara ndani ya mita 60”alisema Byarugaba .

Hata hivyo alieleza kuwa ujenzi wa vizimba na meza ndani ya paa unafanywa na wafanyabiashara utakamilika kabla ya Januari 23 mwaka huu.

Byarugaba alisema kuwa wakati wa kuanza utaratibu wa kujenga soko hilo jipya pasipo kumwacha mfanyabiashara yoyote vitengo vyote vilishirikishwa ambavyo jumla yake ni 24 ,"kutokana na uwingi wa wafanyabishara walikuwa wakiwatumia wawakilishi huku halmashauri ikitoa wawakilishi wakiongozwa na Mkurugenzi wa halmashauri Jennifer Omolo.
“Timu hii ilikuwa na kazi kubwa ya kuhamasisha wafanyabiashara wanaojiandaa kuhama kupisha hifadhi ya barabara, kuwatambua watakaopewa kipaumbele katika kuhamia soko jipya, kufanya mikutano ya mara kwa mara ili kuweka mikakati na kupeana taarifa za ujenzi,” alisema Byarugaba.
Ofisa habari huyo alifafanua ,ujenzi wa vyumba vya mzunguko wa soko vinajengwa na wafanyabiashara wenyewe kwa kuingia mkataba maalumu na halmashauri na wafanyabiashara 151 wamesaini mikataba ya ujenzi kati ya 220 waliojaza fomu za maombi.

Kwa upande wa wafanyabiashara wa soko la Mailmoja,akiwemo mzee wa shamba,alisema wafanyabiashara wamebariki kuhama ili kupisha maendeleo ya Mji huo.
Alisema shaka ipo ,wakihofia hadi kufikia Jan 23 kuna uwezekano wa kutokamilika vibanda vitakavyotosholeza wafanyabiashara ambao tayari wameingia mkataba na halmashauri.
Mzee wa shamba alisema kikubwa ni kuongeza kasi ya ujenzi ili kukamilisha kwa wakati na kuwaondolea usumbufu wafanyabiashara hao.
Nae meneja wa TANROADS Pwani,Injinia Yudas Msangi alisema zoezi la bomoa bomoa limesuasua kwa kipindi kirefu.
Alisema awali ilikuwa lifanyike,agost mwaka jana,muda uliongezwa hadi mwezi novemba ,na wahusika walishawekewa X,kisha serikali ya mkoa iliongeza miezi mitatu hadi Jan 23 ili kupisha ujenzi wa soko.

Msangi aliwaomba wananchi na wafanyabiashara kuanza kuondoka kwa hiari pasipo kusubiri bughudha .

Miundombinu ya soko jipya la Mailmoja imefikia sehemu nzuri ya ujenzi kwani paa limekamilika kwa ajili ya wafanyabiashara 119, vizimba vya taka, choo, maji umeme, ugawaji wa vyumba 151 kwa waliojaza mikataba na kibanda cha umeme na mambo yanaendelea 

0 maoni:

Chapisha Maoni