Jumatatu, 16 Januari 2017

MBUNGE WA JIMBO LA MUFINDI KUSINI MENDRAD KIGOLA AWAZUNGUMZIA WATUMISHI WA MUNGU WANAODAI KUPONYA UKIMWI

  Posted by Esta Malibiche on JAN 16,2017 in NEWS
 
  Tokeo la picha la kigola
MBUNGE wa Jimbo la Mufindi Kusini, Mendrad Kigolla amewaomba watumishi wa Mungu wanaowaombea watu wenye maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) kuwahimiza pia kutumia dawa ili wasipoteze maisha kupitia maombi hayo.
Akichangia taarifa ya utekelezaji wa shughuli za mapambano dhidi ya Ukimwi iliyotolewa na Mratibu wa Ukimwi wa Mkoa Dk Paul Luvanda alisema wapo baadhi ya wenye maambukizi hayo na Ukimwi waliofariki baada ya kuacha kutumia dawa za kupunguza makali ya VVU (ARVs) wakitegemea kupona kwa maombi.
“Kuna wahubiri wengi tu siku hizi wanaotangaza kuponya watu Ukimwi, baadhi yao wamewafanya wenye ugonjwa huo kuacha kutumia dawa wakiamini watapona kwa maombi pekee,” alisema.
Alisema zipo takwimu (hakuzitaja) zinazoonesha kuwepo kwa idadi kubwa ya walioacha kutumia dawa hizo kwa imani ya kupona kwa njia ya maombi, kufariki dunia.
“Ombi langu kwa watumishi hao wa Mungu, kazi yenu ni njema sana lakini ombeeni watu wapone kwa imani wakati wakiendelea kutumia dawa hizo ili kupunguza madhara ya ugonjwa huo,” alisema.
Akiwasilisha taarifa ya hali ya janga la Ukimwi na maambukizi ya VVU mkoani Iringa, Dk Luvanda alisema bado tatizo ni kubwa linalohitaji jitihada kubwa kulitokomeza.
Alisema kwa mujibu wa utafiti wa viashiria vya maambukizi mapya ya VVU na maralia wa mwaka 2011/2012, takwimu zinaonesha kuwa kiwango cha maambukizi mapya ya VVU mkoani Iringa ni asilimia 9.1, takwimu inayoufanya mkoa huo uwe wa pili kwa maambukizi hayo kitaifa baada ya Njombe.
“Kati ya hizo asilimia 10.9 ya maambukizi ni kwa wanawake wenye umri wa kati ya miaka 15 na 49 wakati asilimi 6.9 ni kwa wanaume wenye umri huo,” alisema.
Alisema takwimu hizo zinaonesha asilimia 7 ya wasichana wenye umri wa kati ya miaka 15 na 24 wanaishi na maambukizi mapya ya VVU mkoani Iringa huku asilimia 1.5 ya wavulana wenye umri huo wakiwa na maambukizi hayo.
Dk Luvanda alisema hali ya maambukizi ya VVU kiwilaya inaonesha wilaya ya Mufindi ndiyo inayoongoza mkoani Iringa kwa kuwa na asilimia kubwa ya wananchi wanaoishi na maambukizi hayo.
“Taarifa kutoka vyanzo mbalimbali vya tafiti zinaonesha wilaya ya Mufindi inaongoza kwa asilimia 12.4, Kilolo asilimia 8.8, Iringa Manispaa asilimia 8.4 na Iringa Vijijini asilimia 6.9,” alisema.
Katika kupambana na janga hilo, Dk Luvanda alisema mwaka 2014 mkoa wa Iringa ulianza kutekeleza mpango mkakati wa kupambana na VVU na Ukimwi kwa kuzingatia vipaumbele vya Taifa na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Alisema mpango huo unalenga kuona ifikapo mwaka 2020 asilimia 90 ya watu wenye maambukizi wanaajitambua,  wameanza kutumia ARVs na kiwango chao cha VVU mwilini kina shuka chini.
Alisema kwa kutimiza hayo wataweza kupunguza maambukizi mapya ya VVU, kupunguza vifo vinavyosababishwa na Ukimwi na kupunguza unyanyapaa na ubaguzi kwa waathirika wa VVU na Ukimwi.

0 maoni:

Chapisha Maoni