Alhamisi, 1 Septemba 2016

UGONJWA WA KICHAA CHA MBWA WAIBUKA TENA MAENEO YA KISIWA CHA PEMBA

Posted by Esta Malibiche on Sept 1.2016 in News with No comment

PEMBA-ZANZIBAR
Na Masanja Mabula –Pemba
UGONJWA wa  Kichaa cha Mbwa uliokuwa umedhibitiwa  kwa kipindi cha miaka miwili , umeripotiwa kutokea tena  katika  baadhi ya maeneo ya Kisiwa cha Pemba  Wizara  ya Kilimo , Maliasili , Mifugo na Uvuvi  imethibitisha .
Afisa Mdhamini Wizara hiyo Pemba Sihaba Haji Vuai amesema katika kipindi cha tarehe 7 hadi 21 mwezi wa nane mwaka huu  , jumla ya kesi sita  za watu kuumwa na mbwa wenye kichaa zimeripotiwa
Amefahamisha kuwa  kati ya hizo kesi nne zimetokea  katika vijiji vya Mtambile , Cumbageni katika Wilaya ya Mkoani nyengine zimeripotiwa Vitongoji na Pondeani Wilaya ya Chake Chake  Mkoa wa Kusini Pemba .
 Akizungumza na mwandishi wa habari Ofisini Kwake Wete , Sihaba Kesi nyengine zimetokea katika Vijiji vya Makangale Wilaya ya Micheweni na Mtemani katika Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba .
“Ugonjwa wa kichaa cha Mbwa ambao ulikuwa umedhibitiwa , sasa umeripuka  katika maeneo tofauti ya Kisiwa cha Pemba , na tayari kesi sita za watu kuumwa na mbwa wenye ugonjwa huo zimeripotiwa ”alifahamisha .
Alieleza , chanjo iliyofanywa na Idara ya Mifugo 2010 -2013 , ilisaidia kuudhibiti ugonjwa huo ambapo katika kipindi cha  mwaka 2014-2015 hakuna kesi iliyoripotiwa kutokea  .
Kufuatia hali Afisa Mdhamini ameiagiza  Idara ya Mifugo kuhakikisha   mbwa wote watakaobainika kuwa na ugonjwa huo wanauliwa ili kuzuia  kuenea kwa ugonjwa huo .
Aidha alifahamisha , Wizara kupitia Idara ya Mifugo imeanza kujiandaa kwa zoezi la chanjo ya wanyama wakiwemo mbwa na paka , huku akiwataka wafugaji wa mbwa kuhakikisha wanafikisha mbwa wao kwenda kupatiwa chanjo wakati ukifika.
Akizungumzia suala la matibabu kwa wananchi walitafunwa na Mbwa mwenye ugonjwa huo  Afisa Mdhamini Wizara ya Afya Pemba Ali Bakar Ali alisema , kuna upungufu wa dawa za kuwatibu wananchi waliofikwa na kadhia hiyo .
Alifahamisha , tatizo hilo halihisiani na ukata wa fedha bali hata katika bohari kuu ya madawa  hakuna dawa za kutosha .
“Kunaupungufu wa dawa za kutibu wananchi walitafunwa na Mbwa mwenye kichaa , na hili sio tatizo la fedha , bali hata kwenye bohari kuu dawa hakuna ”alifahaamisha .
Baadhi ya wananchi waliozungumza na mwandishi wa habari hizi wameiomba Wizara ya Kilimo , Maliasili , Mifugo na Uvuvi kuharakisha zoezi la kuwachanja mbwa ili kukinga ongezeko la ugonjwa huo .

0 maoni:

Chapisha Maoni