Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama
akiwasilisha bajeti ya ofisi yake wakati wa kikao cha Kamati ya Kudumu
ya Bunge ya Katiba na Sheria ya Kupitisha Bajeti uliofanyika katika
Ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere Dar es Salaam Aprili 12,
2016
Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria ya kupitisha bajeti wakifuatilia
bajeti ya ofisi hiyo walipokutana kuijadili na kuipitisha bajeti hiyo
katika Ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere Dar es Salaam Aprili
12, 2016.
Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na
Usimamizi wa Rasilimaliwatu Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Issa Nchansi
akifafanua jambo wakati wa kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba
na Sheria ya kupitisha bajeti kilichofanyika tarehe 12 Aprili, 2016
katika Ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa kikao cha Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria ya Kupitisha Bajeti Mhe. Mohamed
Mchengerwa ambaye ni mbunge wa Rufiji (katikati) akieleza jambo wakati
wa kikao hicho walipokutana kujadili Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu
Aprili 12, 2016 katikaUkumbi wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere Dar
es Salaam.
Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa
Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Brig.Jen Mbazi Msuya (katikati) akifuatilia
bajeti ya Idara yake pamoja na wataalamu wake kushoto kwake ni Charles
Msangi na kulia ni Daniel Alfei wakati wa kikao cha Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Katiba na Sheria ya Kupitisha Bajeti Aprili 12, 2016.
(Picha Zote na Ofisi ya Waziri Mkuu)
………………………………………………………………………………………….
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu (Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama
ameiagiza Idara ya Uratibu wa Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu kufanya
tathimini ya hali halisi za athari zilizosababishwa na ndege aina ya
kwerea kwerea katika mashamba ya mtama na uwele yaliyopo Mkoani Dodoma
katika Wilaya Bahi.
Waziri Mhagama aliyasema hayo
wakati wa Kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria cha
Kupitisha Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kilichofanyika jana katika
Ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.
Kikao hicho kiliibua hoja za
wajumbe ikiwemo hoja iliyo bainisha athari za maafa kwa wakazi wa Wilaya
ya Bahi kuhusu ukosefu wa chakula baada ya mashamba yao kuvamiwa na
ndege waharibifu aina ya Kwerea kwerea.
Hoja hiyo iliibuliwa na Mbunge wa
Bahi Bw. Omar Badwel alisema wananchi wake wapo katika wakati mgumu
hivyo wanahitaji msaada kutoka serikalini kwa kuwa mazao yao yamevamiwa
na ndege hao.
“Kwerea kwerea wamekuwa ni
changamoto kwa wakazi wa wilaya yangu hususani maeneo ya Manyoni
ninaomba serikali kupitia Idara ya Maafa isaidie kwa kuwapa chakula na
mbegu Wananchi ili waweze kujikimu na kuitatua changamoto hiyo”Alisema
Badwel.
“Mazao yaliyoshambuliwa na kuharibiwa na ndege aina ya kwerea kwerea ni mazao ya mtama na uwele, Alisisitiza”.
Waziri Mhagama alisema anatafuta
uwezekano wa kuona umuhimu wa kushirikisha Wizara ya kilimo na Mifugo
kwa kuangalia namna zinavyoweza kushirikiana kuondoa wadudu waharibifu
wa mazao mkoani Dodoma.
“Serikali itafanya tathmini kwa
waathirika hao wa maafa Wilayani Bahi, ni vizuri Idara ya Maafa ifanye
hivyo haraka ili kusaidia kunusuru hali ya wakazi wa Dodoma”Alisisitiza
Mhagama.
Waziri Mhagama alimpongeza
Mhe.Badwel kwa kuwajali wananchi wa Bahi kwa kuibua jambo muhimu hivyo
aliahidi kulitafutia ufumbuzi wa haraka.
“Suala hili ni muhimu kwa kuwa
linagusa maisha ya Wananchi moja kwa moja sisi kama serikali
tumelichukua kwa uzito na tutahakikisha Idara ya maafa inatembelea
maeneo husika kwa ajili ya kufanya tathimini za haraka kwa waathirika
waliopoteza mazao yao ili kujua namna tunavyoweza kutoa msaada wa haraka
katika maeneo husika ” alisema Mhagama.
Awali; kikao hicho kililenga
kupitia na kujadili bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu yenye fungu namba 25
(Ofisi Binafsi ya Mhe.Waziri Mkuu), 37(Sera, Uratibu a Bunge), 15 na 65
(Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu) na fungu 27 na 61 (Tume ya
Msajili wa Vyama vya Siasa na Tume ya Uchaguzi.
0 maoni:
Chapisha Maoni