RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein leo amewaongoza
viongozi na wananchi mbali mbali katika kisomo maalum cha kumuombea dua
Rais wa Kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi marehemu
Sheikh Abeid Amani Karume ikiwa pia, ni maadhimisho ya kumbukumbu ya
miaka 44 ya kifo chake.
Marehemu Mzee Karume ambaye pia,
alikuwa Kiongozi wa Chama cha Afro-Shirazi (ASP) na Makamu wa Kwanza wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliuawa siku ya Ijumaa tarehe 07
April, 1972 saa 12:05 jioni katika Makao Makuu ya ASP ambayo sasa ni
Ofisi Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) iliyopo Kisiwandui mjini Unguja.
Katika maadhimisho hayo
yaliyofanyika Ofisi Kuu ya CCM ambako ndipo alipozikwa marehemu, Dk.
Shein na viongozi mbalimbali pamoja na wananchi walishiriki kisomo
maalum cha kumuombea dua kiongozi huyo ambaye kifo chake kiliushitua
ulimwengu mzima.
Baada ya kisomo hicho viongozi
hao walizuru kaburi la marehemu wakiambatana na viongozi wa madhehebu
mbalimbali ya dini ambao walipewa fursa za kumuombea dua marehemu wakiwa
kaburini hapo.
Kisomo hicho cha kumuombea dua
Marehemu Mzee Karume kilihudhuriwa na viongozi mbali mbali akiwemo
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu
Hassan kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John
Pombe Magufuli, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd
na Rais mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Sita, Mhe.
Amani Abeid Karume.
Viongozi wengine walihudhuria
katika hitma hiyo ni Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mzee Ali Hassan Mwinyi, Spika wa Baraza la Wawakilishi Mhe. Zubeir Ali
Maulid, Mufti Mkuu wa Tanzania Bara Sheikh Abubakar Zubeir, Kadhi Mkuu
wa Zanzibar Sheikh Khamis Haji, Sheikh wa Mkoa wa Dar-es- Salam Sheikh
Mussa Salum.






0 maoni:
Chapisha Maoni