Ijumaa, 15 Aprili 2016

MBUNGE WA JIMBO LA KALENGA GODFREY MGIMWA AANZA KUTEKELEZA VIFO VYA MAMA NA MTOTO



MBUNGE wa Jimbo la Kalenga Mkoani Iringa kupitia chama cha mapinduzi ccm Mh, Godfrey Mgimwa Alisema katika kukabiliana na tatizo la vifo vya Wajawazito na Watoto wachanga tayari ameanza kupeleka dawa kwa baadhi ya vituo vya afya katika jimbo lake ikiwa ni pamoja na  kuboresha vituo vya afya ambapo vituo takribani vinne vimekwisha kamilika.

Mgimwa aliyasema hayo katika mahojiano maalum na mtandao huu wa kali ya habari  alipotakiwa kueleza utekelezaji wa majukumu yake tangu alipo chaguliwa kuwa Mbunge wa jimbo hilo.

Alisema kuwa uboreshaji wa huduma za afya unakwenda sambamba na kuwapo wataalamu wa kutosha ambapo kwa nafasi yake amekwisha kuanza hatua ya kuiomba serikali kuongeza wataalam katika jimbo lake na kuvitaja vituo vya afya ambavyo vimekarabatiwa kuwa ni kituo cha afya Nzihi, Mgama, Kiponzelo na Hospitali ya Tosamaganga ambayo inahitaji gari la kubebea wagonjwa kutokana na gari lililopo kuwa dogo na kwamba halitoshi.


Alisema amejipanga katika bunge la bajeti lijalo kulisemea swala la miradi na kuhakikisha bajeti inayopangwa inakidhi mahitaji ya jamii ambayo pamoja na mambo mengine itasaidia pia kuimarisha huduma za afya ya wajawazito na watoto wachanga

“Nimejipanga vizuri kulisemea tatizo hili pamoja na miradi iliyopo kwenye jimbo langu kama vile mradi wa maji Welu na Kiwele ambao haujakamilika ili ipangwe bajeti itakayokamilisha mradi huo kwa ajili ya jamii. Tuna barabara na pia ambazo nitahakikisha fedha zinatoka kwa ajili ya ujenzi huo na pia tutaboresha mawasiliano ya simu ili kuwarahisishia wananchi kupata taarifa kwa wakati pamoja na kuendelea kukamilisha mradi wa umeme vijijini” alisema Mgimwa

‘’Kuhusu Tanzania kuwa na Idadi kubwa ya vifo vya akina mama vitokanavyo na uzazi Mgimwa amesema atahakikisha anaweka  mpango mkakati kwa kusimamia vipaumbele vyake kwa kushauri serikali kutenga Fedha za kutosha ili kuweza kuboresha huduma za afya kwa akina mama na watoto wanapozaliwa wawe na afya nzuri na pia kuwawezesha wazee nao kupata huduma bora kwani wao wanastahili pia” alisema

Alisema mama mjamzito hatakiwi kusumbuliwa kwa namna yeyote ambapo anatakiwa kupata huduma bora kwa ajili ya kulinda afya yake

“Mwanamke mjamzito hatakiwi kusumbuliwa kabisa na kwa namna yeyote na kwa  kulitambua hili mimi kwenye jimbo langu ninaweka mfumo utakaowasaidia akina mama kwa haraka na kwa ubora zaidi ili wasipate shida’’.

 Mgimwa alisema ongezeko la watu haliwezi kuathiri mipango ya serikali bali linatakiwa kuwekewa mipango endelevu ya bajeti itakayokidhi ongezeko la watu na kwamba tatizo siyo ongezeko bali ni namna ya kukabiliana na ongezeko hilo kwa kuweka mipango ya huduma.

  “Jambo la msingi ni kuweka mkazo juu ya swala hili  la ongezeko la watu ili wanapoongezeka waweze kuongeza maendeleo ya taifa. Inatakiwa tuweke mazingira mazuri ili wanapoongezeka wapate huduma muhimu, kwa mfano tunaweza kuwekeza katika elimu ili wanapoongezeka wapate elimu kwa ajili ya maendeleo ya taifa” alisema.

Hata hivyo alisema uzazi wa mpango si suala la kulisemea sana kimpango kwa sababu lina mambo mengi kutokana na magonjwa na vifo.

“Hatuwezi kusema tunapunguza ili twende na bajeti ila tunatakiwa kujipanga. Tujifunze kwa taifa la Nigeria lina idadi ya watu wengi lakini uchumi wao upo vizuri pia tuangalie Marekani ina watu wengi lakini uchumi wao ni mzuri. Cha msingi ni kuweka mipango ya kuimarisha uchumi ili uendane na ongezeko la watu” alisema mgimwa.



0 maoni:

Chapisha Maoni