Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Joseph Kabila amesema Serikali yake itaendelea kutumia bandari ya Dar es Salaam kupitishia mizigo yake ili kuendeleza ushirikiano na manufaa ya kiuchumi baina ya wananchi wa nchi hizo.
Akizungumza na waandsihi wa habari leo Ikulu jijini Dar es Salaam mara baada ya kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Magufuli, alisema kuwa nchi ya Kongo imekua ikitumia Bandari ya Dar es Salaam tangu hapo awali, na sasa wanatarajia kutumia bandari hiyo kwa kupitisha mizigo zaidi.
“Tunatarajia kufanya biashara zaidi na Bandari ya Dar er Salaam kwa kupitisha mizigo kwa wingi, miaka ya nyuma tulikua na matatizo kidogo ila kwa sasa kuna kazi kubwa inafanyika ya kuboresha Bandari ya Dar es Salaam na sisi tutaweza kupitisha mizigo yetu kwa wingi,” alisema Rais Kabila.
Aidha Rais Kabila alisema kuwa katika mazungumzo yake na Rais Magufuli walijadili masuala mbalimbali ikiwemo hali ya usalama katika mipaka ya Congo na uwekezaji.
Kwa upande wake Rais Magufuli, alisema kuwa katika kuboresha usafirishaji mizigo kwenda nchini Kongo, Bandari ya Dar es salaam imepunguza maeneo ya vituo vya kupima mizigo ambapo kwa sasa kuna maeneo matatu yenye vituo vya kupimia mizigo ambavyo ni Vigawanza, Manyoni na Nyakaliwa.
Ambapo pia Bandari hiyo imeongeza kipindi cha msamaha wa kuhifadhi mizigo bandarini kutoka nchini Kongo kutoka siku 14 hadi siku 30.
Aidha, Rais Magufuli alisema kuwa biashara kati ya Tanzania na Kongo imendelea kuimarika hadi kufikia shilingi bilioni Tsh. 393.6 kutoka Tsh. Bilioni 23.1 kwa mwaka 2009.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Nishati na Madini Mhe. Sospeter Muhongo na Waziri wa Mafuta wa Kongo Mhe. Ngoyi Makena wametia saini mkataba wa makubaliano wa kutafuta mafuta katika ziwa Tanganyika.
Ziara ya Rais wa Kongo nchini inalenga kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia pamoja na kukuza maendeleo ya uchumi baina ya nchi hizo mbili.
Na Immaculate Makilika – MAELEZO