Makamu
wa Rais Mh. Mama Samia Suluhu Hassan amewahakikishia Wanasayansi
Watafiti waliopo nchini kuwa Serikali ya Tanzania inatambua mchango wao
na wataendelea na juhudi za kuwalinda kwani ni nguzo muhimu ya kufikia
malengo ya milenia katika Nyanja mbalimbali ikiwemo Uchumi, Afya, Elimu
na Maendeleo endelevu.
Makamu
wa Rais ameyasema hayo mapema leo Jijini Dar es Salaam wakati
alipozindua rasmi Kongamano la 30 la Kimataifa la Wanasayansi Watafiti
lililoandaliwa na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu
(NIMR) ambalo ni la siku tatu kuanzia Oktoba 4 hadi 6.2016.
Akiwahutubia
Wanasayansi hao watafiti zaidi ya 300 kutoka Tanzania na Mataifa ya
Nje, amesema kuwa Taifa bila watafiti hakuna maendeleoo hivyo uwepo wa
watafiti hao ni kielelezo tosha cha kufikia maendeleo hivyo anaamini
kuwa baada ya mkutano huo, Wataalam hao watakuwa chachu ya kichocheo cha
uchumi kupitia tafiti zao.
Akiwaondoa
hofu wanasayansi watafiti hao, Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu
amebainisha kuwa, Serikali imesikitishwa na tukio lililotokea hivi
karibuni la kuchomwa moto baadhi ya watafiti huko Mkoani Dodoma kuwa ni
la kinyama na halivumiliki na sheria itachukua mkondo wake na wahusika
wote watafikishwa mikononi mwa sheria.
Kwa
upande wake Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto, Mh. Dk. Hamisi Kigwangalla katika mkutano huo amebainisha kuwa,
Wizara yake inashirikiana bega kwa bega na wanasayansi na imekuwa
ikiwatumia katika mikakati mbalimbali ya kitaifa na hata kujenga sera za
Afya na mambo mengine ya kimaendeleo.
“Wanasayansi
watafiti kwa uzoefu wao tunautumia kwa kiwango kikubwa sana hapa
nchini. Kwani wamekuwa chachu kubwa sana na hata mfumo wa Kiserikali
umekuwa ukitengeneza mfumo mahususi wa kufanya kazi kwa pamoja kwani
hata sera na mikakati ya nchi pia tumekuwa tukiwatumia wanasayansi hao”
amesema Dk. Kigwangalla.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NIMR, Dk. Mwele Malecela amesema
kongamano hilo linajumuisha nchi mbalimbali za Afrika, Ulaya na Amerika
ambapo washiriki zaidi ya 300 wanashiriki huku mada zaidi ya 220
zitawasilishwa na kujadiliwa kwa pamoja na wataalam hao.
“Jumla
ya mada 220 zinawasilishwa kuanzia leo na kujadiliwa katika Kongamano
hili la Siku tatu ambalo pia litahusisha mkutano Mkuu wa mwaka wa NIMR”.
Amesema Dk. Mwele.
Katika
kongamano la mwaka huu, linaongozwa na kauli mbiu ya “Uwekezaji katika
tafiti zenye ubunifu ili kufikia malengo endelevu ya dunia”.
Nchi
ambazo zinashiriki kongamano hilo kuwa ni Afrika Kusini, Kenya, Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Kongo, Uganda, Australia, Denmark, Ubeljiji,
Uholanzi, Uingereza, Ujerumani, Uswis, Kanada, Sweden, Norway, Marekani,
Bangladesh, Thailand na wenyeji Tanzania.
Baadhi ya wadau na Wanasayansi Watafiti wakifuatilia Kongamano hilo la 30 la NIMR mapema leo
Meza
kuu ikifuatilia tuko hilo la ufunguzi: Makamu wa Rais Mh. Mama Samia
Suluhu Hassan (Wa pili kulia) akifuatiwa na Naibu Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mh. Dk. Hamisi Kigwangalla.
Kushoto ni Dk. Honorati Masanja kutoka taasisi ya Utafiti ya Ifakara na kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa NIMR, Dk. Mwele Malecela
Tukio likiendelea
Makamu
wa Rais Mh. Mama Samia Suluhu Hassan akikabidhi ngao kwa mmoja wa
wadhamini wa kongamano hilo. Kushoto ni Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mh. Dk. Hamisi Kigwangalla na Kulia
ni Mkurugenzi Mkuu wa NIMR, Dk. Mwele Malecela
Naibu
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mh. Dk.
Hamisi Kigwangalla akizungumza na wanahabari (Hawapo pichani) muda mfupi
baada ya ufunguzi wa kongamano hilo
Mkurugenzi
Mkuu wa NIMR, Dk. Mwele Malecela akizungumza na wanahabari (Hawapo
pichani) muda mfupi baada ya ufunguzi wa kongamano hilo.
0 maoni:
Chapisha Maoni