Jumatano, 5 Oktoba 2016

Naibu Waziri ofisi ya rais (TAMISEMI) Selemani Jafo awataka maafisa elimu wa wilaya na mikoa kuacha tabia ya kusubwiri kupelekea kazi mezani

Posted by Esta Malibiche on Oct5.2016 in NEWS

ja1
Naibu Waziri ofisi  ya rais  (TAMISEMI) Selemani Jafo, akimpa mkono wa shukrani mwenyekiti wa umoja wa chama cha wafanyabiashara wa misitu wilayani Kisarawe (UWAMAMI)Ally Mnemvu mara baada ya kumkabidhi madawati 150 .(picha na Mwamvua Mwinyi)
ja2
Naibu waziri  ofisi  ya rais  (TAMISEMI) Selemani Jafo  ,watatu kushoto akiwa ameketi kwenye moja ya madawati ambayo alipokea kutoka umoja wa wafanyabiashara wa misitu Kisarawe (UWAMAMI),wa pili  kushoto ni mkuu wa wilaya ya Kisarawe, Happiness Seneda. (Picha na Mwamvua Mwinyi)
……………………………………………………………..
Na Mwamvua Mwinyi, Kisarawe
Naibu waziri  ofisi ya rais  Tamisemi,Selemani Jafo  ,amewataka maafisa elimu wa wilaya na mikoa kuacha tabia ya kusubiri  kupelekewa  kazi mezani na badala yake watoke kutembelea kwenye maeneo yao ya kazi.
Aidha ametoa maelekezo kwa maafisa hao kuanza kujenga tabia ya kukagua mambo yanayoendelea kwenye maeneo yao ikiwemo zoezi la utengenezaji madawati ili kuwa na takwimu halisi.
Katika hatua nyingine amesema ofisi yake inawashukuru watanzania ,kwa kufanikisha juhudi ya kuchangia madawati kwa asilimia 98 ya utengenezaji wa madawati.
Jafo  ambae pia ni mbunge wa jimbo la Kisarawe ,aliyasema hayo, wakati alipokuwa akikabidhiwa madawati 150 yaliyogharimu mil.15 kutoka kwa umoja wa wafanyabiashara wa misitu Kisarawe (UWAMAMI).
Alisema mara  nyingi alipokuwa akitembelea katika halmashauri mbalimbali amekutana na taarifa ya takwimu ya madawati tofauti na taarifa ya shule husika.
Jafo  alieleza kuwa tatizo hilo lipo hivyo maafisa elimu wanapaswa kutoka maofisini na kuwajibika kikamilifu.
Hata hivyo alisema hawatakuwa tayari kuwaadhibu walimu kumbe baadhi ya maafisa elimu wenyewe  wameshindwa kutimiza wajibu wao.
“Wahakikishe wanaacha kufanya kazi za mezani na kimazoea bali watoke kwenda kukagua kazi zao wenyewe ili kujua takwimu za zoezi hilo na wanafunz ili kuondokana na wanafunzi hewa na kupata takwimu halisi ya zoezi zima la madawati” alisema Jafo.
Hata hivyo Jafo aliwashukuru wananchi ,wadau,taasisi na mashirika mbalimbali kwa kufikia hatua nzuri ili kuondoa tatizo la kukaa chini kwa wanafunzi.
“Zipo halmashauri ambazo hazijakamilisha zoezi hilo naamini watakamilisha zoezi kwa kufuatilia madawati ambayo bado yanatengenezwa.
“Nawapongeza kwani awali madawati ya shule za msingi  mahitaji yalikuwa mil. 3.5 lakini kwa sasa kero inaonekana kwenda kubaki historia” alisema Jafo.
Jafo alieleza kuwa tatizo lililopo mbele kwa sasa ni miundombinu ikiwemo uhaba wa madarasa na vyoo hivyo kuna kila sababu ya kupanga mipango mkakati ya kushirikiana ili kukabiliana na hali hiyo.
Aliwashukuru UWAMAMI kwa kutoa madawati hayo 150 na kusema atatoa maelekezo kuwa madawati hayo yapelekwe katika shule zipi.
Nae mkugenzi wa halmashauri ya Kisarawe,Musa  Gama alisema wana upungufu wa madawati 404 .
Alisema madawati bado yanatengenezwa katika maeneo mbalimbali na wanaamini zoezi hilo watalimaliza mwishoni mwa  mwezi huu.
Kwa upande wake ,katibu  wa UWAMAMI ,Ally Kombe, aliomba ushirikiano baina ya  serikali na chama hicho ili kufikia malengo ya mipango waliojiwekea kukabiliana na changamoto za kijamii wilayani hapo.
Kombe alisema tayari wameshasaidia ujenzi wa madarasa katika baadhi ya shule zilizopo Kisarawe na kupanda miti maeneo ya shule na kijiji.

0 maoni:

Chapisha Maoni