Postedy by Esta Malibiche on August 7.2016 in News with No comment
Mkuu wa Kitengo cha Lishe Wizara ya
Afya Zanzibar Asha Hassan akizungumzia umuhimu wa kunyonyesha maziwa ya
mama pekee katika miezi sita ya mwanzo kama Lishe bora zaidi katika
makuzi ya mtoto wakati wa kilele cha maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji
yaliyofanyika Mwera Wilaya ya Kati Unguja.
Naibu Waziri wa Afya Arusi Said
Suleiman akizungumza na akinamama waliohudhuria maadhimisho ya kilele
cha wiki ya unyonyeshaji duniani katika kijiji cha Mwera Wilaya ya Kati
Unguja.
Mkuu wa Kitengo cha Lishe Wizara ya
Afya Zanzibar Asha Hassan akizungumzia umuhimu wa kunyonyesha maziwa ya
mama pekee katika miezi sita ya mwanzo kama Lishe bora zaidi katika
makuzi ya mtoto wakati wa kilele cha maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji
yaliyofanyika Mwera Wilaya ya Kati Unguja.
Afisa Lishe, UNICEF Dar es salaam
Elizabeth Macha akitoa salamu za Shirika hilo katika maadhimisho ya
kilele cha wiki ya unyonyeshaji duniani yaliyofanyika kitaifa Mwera
Wilaya ya Kati Mkoa Kusini Unguja.
Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya
Zanzibar Dkt. Fadhil Mohamed Abdalla akizungumza katika hafla hiyo
iliyofanyika Mwera Wilaya ya Kati Unguja.
,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,
Na Ramadhani Ali/Maelezo Zanzibar
Shirika la Umoja wa Mataifa la
kuhudumia watoto (UNICEF) limesisitiza umuhimu kwa Tanzania kuongeza
juhudi katika kuweka mikakati ya kuboresha unyonyeshaji wa watoto mara
tu baada ya kuzaliwa hadi kufikia miaka miwili.
Akitoa salamau za kilele cha wiki
ya unyonyeshaji duniani iliyoadhimishwa katika kijiji cha Mwera Wilaya
ya kati Unguja, Afisa Lishe kutoka UNICEF Dar es Salam, Elizabeth
Macha alisema utafiti wa 2014 unaonyesha ni mtoto mmoja kati ya wawili
wenye umri hadi kufiki miezi 23 wanaonyonyeshwa mara baada ya kuzaliwa
kwa Tanzania.
Alisema kwa Zanzibar ni asilimia
61 tu ya watoto wenye umri kati ya miaka 0-23 wanaonyonyeshwa katika
muda wa nusu saa baada ya kuzaliwa na Mkoa wa Kusini Pemba upo nyuma
zaidi ukiwa na asilimia 52.
Aliongeza kusema kuwa watoto
wakicheleweshwa kunyonyeshwa kwa masaa 2 hadi 23 baada ya kuzaliwa
inaongeza hatari ya kufa katika siku 28 za kwanza za maisha ya mtoto kwa
asilimia 40.
Alisisitiza watoto kunyonyeshwa
maziwa ya mama kwa kipindi cha miezi sita ya mwanzo bila kupewa chakula
chengine kwa vile yanamsaidia kukua vizuri kiakili na kimwili.
Alisema watoto wanaonyonyeshwa maziwa ya mama pekee kwa Zanzibar ni asilimia 20 wakati Pemba ina asilimia 10.
Afisa Lishe wa UNICEF alisema
kunyonyesha ni moja ya uwekezaji muhimu ambayo nchi inaweza kufanya kwa
ajili ya ustawi wa wananchi wake.
“Tunaweza kupata maendeleo ya
haraka katika maendeleo yetu endelevu kwa kukuza, kulinda na kusaidia
unyonyeshaji,” alikumbusha afisa Lishe wa UNICEF.
Alisema iwapo mipango mizuri ya
kuboresha unyonyeshaji na kutekeleza kwa vitendo Tanzania inaweza
kufanya unyonyeshaji kuwa sehemu ya mwanzo katika kuimarisha afya kwa
kila mtoto na jamii kwa jumla.
Mkurugenzi wa Kinga na Elimu ya
Afya Zanzibar Dkt. Fadhil Mohhamed Abdalla akimkaribisha mgeni rasmi
katika sherehe hizo alisema asilimia kubwa ya wanawake wananyonyesha
watoto lakini kasoro iliyopo ni kuwachelewa kuwanyonyesha, kuwalisha
vyakula vyengine wakiwa chini ya miezi sita na kuwaachisha maziwa kabla
ya miaka miwili.
Naibu Waziri wa Afya ambae alikuwa
mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji
duniani Arusi Said Suleiman aliwahimiza akinamama kuwanyonyesha watoto
wao maziwa pekee katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo kwani ni kinga
bora kwa afya zao.
Kauli mbiu ya maadhimisho hayo “Unyonyeshaji ni kichocheo cha Maendeleo endelevu. Dumisha unyonyeshaji kwa maslahi ya wote”.
0 maoni:
Chapisha Maoni