Postedy by Esta Malibiche on August 8.2016 in KITAIFA with No comment
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na
mkewe Mary wakipata maelezo kuhusu jiko banifu kutoka kwa mkuu wa
wilaya ya Nkansi, Saidi Mtanda (kushoto) kuhusu jiko banifu
lililobuniwa na kutengenezwa na Samuel Msigale (watatu kulia) ambaye
ni mjasiliamali kutoka Nkansi mkoani Rukwa. Alikuwa kitembelea
maonyesho ya wakulima Nanenane kwenye uwanja wa maonyesho ya wakulima
Nanenane wa John Mwakangale Agosti 8, 2016. (Picha na Ofisi ya waziri
Mkuu)
……………………………………………………………………………………………..
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
ameiagiza Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kuhakikisha inafufua sekta
ya ushirika na kuwachukulia hatua kali watendaji wote waliohujumu
ushirika na kusababisha machungu kwa wanaushirika ili iwe fundisho kwa
wengine.
Pia ameitaka Wizara hiyo kupitia
upya sekta ya ushirika kwa kuanza na viongozi walipo ndani ya wizara
hadi mikoani kuhakikisha kama wanafanya kazi zao ipasavyo na kuwaondoa
watakaobainika kwa uzembe.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo leo
(Jumatatu, Agosti 08, 2016) wakati akifunga maadhimisho ya sherehe za
nane nane kwa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini yaliyofanyika kwenye uwanja
wa John Mwakangale mkoani Mbeya.
Hata hivyo Waziri Mkuu amesema
mkulima, mfugaji na mvuvi mdogo au mmoja mmoja hawezi kupunguza umaskini
bila ya kuwa na chombo cha kuwaunganisha na kuwapa nguvu ya kutetea bei
ya mazao yao kama ushirika. Aidha, ushirika imara utawasaidia kutafuta
soko, kupata mikopo ya riba nafuu.
Amesema pamoja na umuhimu wa
kuwepo kwa ushirika, tasnia hiyo imewaumiza wakulima wengi na kuwafanya
kukata tamaa katika uzalishaji kutokana na usimamizi mbovu, ubadhirifu
na ubabe wa baadhi ya viongozi wa ushirika.
“Wahimizeni na kuwashawishi
wakulima, wafugaji na wavuvi kujiunga katika vikundi vya ushirika vya
uzalishaji na SACCOS. Aidha, elimu ya ushirika inayotolewa kwenye
maonesho ya mwaka huu, iwe changamoto kwenu kwamba umoja ni nguvu na
utengano ni udhaifu,” amesema.
Wakati huo huo Waziri Mkuu amesema
Serikali haitamvumilia mfugaji anayelisha katika maeneo ya hifadhi na
vyanzo vya maji, Wakuu wa Mikoa na Wilaya waendelee kulinda maeneo hayo.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa
Kilimo, Mifugo na Uvuvi William Ole Nasha alisema sekta ya kilimo
imekuwa na mafanikio makubwa ambapo katika kipindi cha miaka mine
mfululizo nchi imeweza kuzalisha chakula cha ziada, ambapo kwa mwaka huu
imezalisha kwa asilimia 123.
“Mafanikio hayo yanachangiwa
jitihada za Serikali katika kutoa ruzuku ya pembejeo, taasisi za utafiti
ambazo zimekuwa zikitafiti aina bora ya mbegu zikitafuta mbegu bora na
wakulima walioamua kuwekeza kwenye kilimo,” alisema.
Naibu Waziri Ole Nasha alisema
katika ukanda wa Nchi za Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ni
nchi mbili tu za Tanzania na Zambia kati ya nchi 15 za jumuia hiyo
hazikabiliwiu na baa la njaa.
Licha ya mafanikio hayo Naibu
Waziri huyo aliwaomba wakulima kuendelea kuzalisha kwa kufuata kanuni
bora za kilimo pamoja na kutumia pembejeo bora.
Naye Mwenyekiti wa Mtandao wa
Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini,
Ladislaus Mwanakatwe ameipongeza Serikali kwa jitihada zake za kuwatetea
pamoja na utatuzi wa kero za muda mrefu zilizokuwa zinawakabili
wakulima ikiwemo ya tozo.
Hata hivyo Mwanakatwe ameiomba
serikali kuitafutia ufumbuzi changamoto ya upatikanaji wa masoko ya
uhakika ya mazao ya kilimo. Pia ameomba Serikali iwezeshe Benki ya
Kilimo (TADB) kufungua matawi katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ili
wakulima wake waweze kupata mikopo kwa urahisi.
0 maoni:
Chapisha Maoni