OFISI
YA TAIFA YA TAKWIMU (NBS) imetangaza mfumuko wa Bei wa Taifa wa mwezi
Julai 2016 na kueleza kuwa umepungua hadi kufikia asilimia 5.1 kutoka
asilimia 5.5 iliyokuwepo mwezi Juni mwaka huu.
Akitangaza
taarifa ya mfumuko wa Bei wa Taifa wa mwezi Julai, 2016 leo jijini Dar
es salaam, Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya
Takwimu, Bw. Ephraimu Kwesigabo amesema kuwa kasi ya upandaji wa bei ya
bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Julai, 2016 imepungua
ikilinganishwa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia mwezi Juni 2016.
Ameeleza
kuwa kupungua kwa mfumuko wa Bei wa mwezi Julai 2016 kumechangiwa na
kupungua kwa kasi ya bei ya baadhi ya bidhaa za vyakula na zile zisizo
za vyakula kwa kipindi kilichoishia Julai 2016 zikiwemo bidhaa za samaki
kwa asilimia 6.6, mafuta ya kupikia asilimia 4.9 na maharage kwa
asilimia 1.9 huku bei zisizo za vyakula zikihusisha ni gesi kwa asilimia
21.5, mafuta ya taa 9.4 na dizeli kwa asilimia 10.3.
Kwa
upande wa bidhaa zisizo za vyakula zilizoonesha kupungua bei ni pamoja
na bidhaa za gesi kwa asilimia 21.5, mafuta ya taa kwa asilimia 9.4 na
dizeli kwa asilimia 10.3.
Aidha,
ameeleza kuwa pamoja kupungua huko, kasi ya upandaji wa bei ya bidhaa
na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Julai, 2016 kwenye baadhi ya bidhaa
umeonesha kuongezeka katika kipindi hicho hasa kwenye kama mchele,
mahindi, unga wa mahindi, vyakula kwenye migahawa na mkaa.
Bw.
Kwesigabo amesema kuwa Fahirisi za Bei nazo zimeongezeka hadi kufikia
103.50 mwezi Julai, 2016 kutoka 103.47 za mwezi Juni 2016, ongezeko
ambalo limechangiwa na kuongezeka kwa bei ya baadhi ya bidhaa za vyakula
zile zisizokuwa za vyakula.
Amesema
ongezeko hilo la Fahirisi linahusisha kundi la bidhaa na huduma za
vyakula na vinywaji baridi, Vinywaji vyenye kilevi na bidhaa za Tumbaku,
Mavazi ya nguo na viatu, nishati, maji na Makazi pamoja na Samani,
vifaa vya nyumbani na ukarabati wa nyumba.
Kundi
lingine linahusisha gharama za Afya, usafirishaji, Mawasiliano,
Utamaduni na Burudani, Elimu, hoteli na migahawa pamoja na bidhaa na
huduma nyinginezo ambazo jumla ya Fahirisi za Bidhaa hizo kwa mwezi huo
zimefikia 103.50.
“Baadhi
ya bidhaa zilizo sababisha kuongezeka kwa Fahirisi ni pamoja na mafuta
ya kupikia asilimia 1.1, samaki wabichi asilimia 6.0, matunda asilimia
4.9, maharage makavu kwa asilimia 2.7, ndizi za kupika asilimia 1.9 na
mahindi kwa asilimia 1.5,” amesisitiza Kwesigabo.
Mbali
na hilo ameeleza kuwa Mfumuko wa Bei wa Bidhaa za vyakula na vinywaji
baridi kwa mwezi Julai 2016 umepungua hadi kufikia asilimia 7.6 kutoka
asilimia 8.1 ya mwezi Juni 2016.
Kwa
upande wa uwezo wa shilingi ya 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na
huduma umefikia shilingi 96 na senti 62 mwezi Julai 2016 ikilinganishwa
na shilingi 96 na senti 65 ya mwezi Juni, 2016.
Aidha,
hali ya Mfumuko wa Bei kwa baadhi ya nchi za Afrika Mashariki imeonesha
kuwa nchi ya Kenya Mfumuko wa Bei wa mwezi Julai umeongezeka hadi
kufikia asilimia 6.39 kutoka asilimia 5.80 za mwezi Juni, 2016, Uganda
ikiwa na Mfumuko wa Bei uliopungua wa asilimia 5.1 kwa mwezi Julai
kutoka asilimia 5.9 za mwezi Juni, 2016.
Na Aron Msigwa –MAELEZo
0 maoni:
Chapisha Maoni