KIONGOZI
wa Jumuiya ya Mabohora Duniani, Dk Syedna Mufaddal Saifuddin amesema
wataendelea kuisaidia Tanzania kutokana na kuridhishwa na utendaji kazi
wa serikali ya Awamu ya Tano inayoendelea kuhakikisha nchi inakuwa na
amani.
Pia alitangaza mkutano mkuu wa dunia wa jumuiya hiyo utafanyika Dar es Salaam, Oktoba mwaka huu.
Alisema
hayo jana mjini hapa alipowasili Uwanja wa Ndege wa Dodoma kwa ziara ya
siku 14 nchini ambako alipokewa na Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga, Mkuu wa Mkoa
wa Dodoma, Jordan Rugimbanana viongozi mbalimbali wa Jumuiya ya Waislamu
Tanzania (BAKWATA) wakiongozwa na Mufti wa Tanzania, Shehe Mkuu
Abubakar bin Zubeiry.Alisema Tanzania ni moja ya nchi za kujivunia
kutokana na amani iliyopo na kama jumuiya wataendelea kusaidia nchi
katika nyanja mbalimbali ikiwemo elimu.
“Nitaendelea kuhimiza jumuiya yetu iendelee kutoa misaada kwa ajili ya kuboresha elimu nchini,” alisema.
Pia
aliahidi kutoa Dola za Marekani 53,000 (Sh milioni 111) kwa serikali na
dola 21,000 (Sh milioni 44) kwa Bakwata, fedha ambazo zitatumika kwa
shughuli mbalimbali za maendeleo.
Naye
Balozi Mahiga, akizungumza kwa niaba ya Rais John Magufuli alisema
wamekuwa wakiridhishwa na jinsi jumuiya hiyo inavyoendelea kutunza
amani, umoja na masikilizano huku akitolea mfano jinsi walivyojitolea
madawati kwa shule za Dar es Salaam.
Alisema
wataendelea kushirikiana na jumuiya hiyo kutokana na wao kuwa
wafanyabiashara na Serikali ya Tanzania kipaumbele chake ni kuwa nchi ya
viwanda.
Alisema
katika msingi wa lengo la uchumi wa viwanda, Jumuiya ya mabohora
imejikita katika viwanda mbalimbali kama Dar es Salaam, Mwanza na maeneo
mengine.
Mwenyekiti
Msaidizi wa Jumuiya ya Mabohora Mkoa wa Dar es Salaam, Zainuddin
Adamjee alisema wamepata faraja kubwa kuona baada ya miaka 43, Rais
Magufuli anatamka serikali kuhamia Dodoma katika kutimiza azma ya Rais
wa Kwanza, Julius Nyerere aliyetangaza serikali kuhamia Dodoma mwaka
1973. Alisema sasa Dodoma mpya inakwenda kujengwa.
|
0 maoni:
Chapisha Maoni