Ijumaa, 12 Agosti 2016

Kila kijiji kupatiwa umeme ifikapo 2020

Postedy by a Esta Malibiche on August 12.2016 in News with No comment

tap1
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo  (kulia) akisalimiana na sehemu ya watendaji kutoka Shirika la Umeme  Tanzania (TANESCO) pamoja na wakandarasi wanaosimamia miradi ya umeme vijijini inayosimamiwa na  Wakala wa Nishati  Vijijini (REA) mara baada ya kuwasili wilayani Handeni mkoani  Tanga.
tap2
Meneja wa Shirika la Umeme  Tanzania (TANESCO) mkoani  Tanga Mhandisi Abdulrahman Nyenye akisoma  taarifa ya utekelezaji wa  miradi ya umeme  vijijini chini ya  Wakala wa Nishati Vijijini (REA) mbele  ya Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo  pamoja na watendaji wengine kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Wilaya ya Handeni, Wizara ya Nishati  na Madini, TANESCO na wakandarasi wanaotekeleza miradi ya REA.
tap3
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (kulia) na Mkuu wa Mkoa wa Tanga,  Martine Shigela (kushoto) wakifuatilia  taarifa ya utekelezaji wa miradi  ya umeme  vijijini inayosimamiwa na REA Awamu ya Pili (REA II) iliyokuwa inasomwa na  Meneja wa Shirika la Umeme  Tanzania (TANESCO) mkoani  Tanga Mhandisi Abdulrahman Nyenye (hayupo pichani)
tap4
Mkuu wa Mkoa wa Tanga  Martine Shigela akielezea mafanikio ya miradi ya usambazaji wa umeme  vijijini  iliyotekelezwa na Wakala wa Nishati  Vijijini Awamu ya Pili (REA II)
………………………………………………………………………………….
Na Greyson Mwase, Tanga
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo amesema kuwa   serikali imeweka mikakati ya kuhakikisha kuwa ifikapo  mwaka  2020 kila mwananchi anapata  umeme  wa uhakika na kupelekea uchumi wa nchi kukua kwa kasi.
Profesa Muhongo aliyasema hayo mara baada ya kupokea  taarifa ya utekelezaji wa miradi ya usambazaji wa umeme  vijijini  inayosimamiwa na Wakala wa Nishati Vijijini Awamu ya Pili (REA II) kutoka kwa watendaji wa  Shirika la  Umeme Tanzania (TANESCO) mkoani  Tanga. Profesa Muhongo  yupo mkoani Tanga kwa ajili ya kukagua miradi ya umeme  vijijini inayotekelezwa na REA pamoja na kuzungumza na wananchi.
Profesa Muhongo alisema kuwa kwa kutambua mchango wa  nishati ya umeme katika ukuaji wa viwanda nchini, serikali imeweka mkakati wa kuhakikisha kuwa kasi ya usambazaji wa umeme  vijijini inaongezeka ili ifikapo  mwaka 2020 mgawo wa umeme uwe ni historia
Alieleza kuwa serikali imeamua kuweka nguvu katika usambazaji wa umeme hususan katika maeneo  ya vijijini ili kufuta umaskini kwani kupitia  nishati ya umeme  wananchi waishio  vijijini wana uwezo wa kuanzisha  viwanda vidogo  vidogo na kuongeza ajira na kupunguza wimbi la  vijana wengi kukimbilia mijini kwa ajili ya kutafuta maisha.
Akielezea mpango wa utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini itakayosimamiwa na REA Awamu ya Tatu (REA III), Profesa Muhongo alisema kuwa serikali imetenga zaidi ya shilingi  trilioni moja kwa ajili  ya kusambaza umeme katika maeneo yote kipaumbele kikiwa ni katika vijiji  vilivyokosa umeme REA Awamu ya Pili. (REA II)
Hata hivyo Profesa Muhongo alieleza kuwa wakandarasi waliokwamisha miradi ya REA Awamu ya Pili hawatapewa kazi ya kusambaza umeme vijijini katika REA Awamu ya  Tatu.
“Serikali iko makini katika kuhakikisha kuwa wakandarasi wenye sifa wanapewa kasi ya kusambaza umeme vijijini, hatuhitaji  wakandarasi wasiotekeleza miradi kwa wakati,” alisema Profesa Muhongo.
Profesa Muhongo aliwataka wakandarasi wa kitanzania wenye  vigezo kujitokeza na kuchangamkia fursa ya kusambaza umeme  vijijini kupita REA Awamu ya Tatu.
Aliongeza kuwa kupitia REA Awamu ya Pili wakandarasi wa kitanzania walionyesha uwezo mkubwa sana katika kusambaza umeme  vijijini.
Ili kuendana na mahitaji ya umeme nchini Profesa Muhongo alilitaka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuhakikisha linaongeza Megawati 200 za ziada ndani ya miezi 18.
Alisema wakati serikali kupitia REA ikiendela na kasi yake  ya kusambaza umeme nchi nzima, shirika la TANESCO linatakiwa kuhakikisha nishati ya  uhakika inapatikana ikiwa ni pamoja na ubunifu wa vyanzo vipya  vya umeme.
Awali akielezea utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini mkoani  Tanga, Meneja wa Shirika la  Umeme  Tanzania mkoani  Tanga, Mhandisi Abdulrahman Nyenye alisema kuwa miradi ya umeme vijijini chini ya ufadhili wa REA imekuwa ikitekelezwa katika wilaya zote nane za mkoa wa Tanga ambazo ni pamoja na  Tanga Mjini, Muheza, Korogwe, Handeni, Kilindi, Lushoto, Pangani na Mkinga ambazo zinapata umeme wake kutoka Gridi ya Taifa kupitia  vituo vya Hale, Kange na Tanga (Majani Mapana)
Alisema kundi la kwanza lilihusisha  wilaya za Korogwe, Lushoto, Handeni na Kilindi ambapo  mradi wa wilaya hizi  ulitekelezwa na mkandarasi STEG International Services Ltd ya Tunisia na kusimamiwa na TANESCO.
Alifafanua kuwa gharama za mradi  huo ilikuwa ni Dola za Marekani 9,463,502 ambazo ni sawa na shilingi bilioni 14.6 na kuendelea kusema kuwa kundi la pili lilihusisha  wilaya za Muheza, Mkinga, Tanga  Vijijini na Pangani na kutekelezwa na mkandarasi Sengerema Engineering Group Ltd ya  Tanzania na kusimamiwa na TANESCO.
Alisema kuwa mradi huu uligharimu shilingi  bilioni 15.6 na kusisitiza kuwa miradi yote kwa mkoa wa Tanga imekamilika kwa asilimia 99 ambapo  jumla ya vijiji 178 vimepatiwa huduma ya umeme
Akielezea changamoto katika utekelezaji wa miradi hiyo Mhandisi  Nyenye alieleza kuwa ni pamoja na tatizo la wananchi kuzuia upitishwaji wa laini za umeme kwenye maeneo yao kwa kudai fidia ili kuruhusu mazao  yao yakatwe na hali ya hewa ya mvua isiyotabirika hasa maeneo ya wilaya za Muheza na Lushoto.
Alitaja chagamoto nyingine kuwa ni pamoja na ubovu wa miundombinu  hasa ya barabara kwenye maeneo mengi , hali  duni ya kiuchumi ya wananchi inayopelekea wananchi kushindwa kulipa  gharama za kuunganishiwa umeme na gharama kubwa za ukaguzi  wa miundombinu ya ndani (wiring) zinazotozwa na wakandarasi ambazo zimekuwa ni kikwazo kwa wananchi wanaohitaji  huduma ya umeme.

0 maoni:

Chapisha Maoni