Na Eleuteri Mangi-MAELEZO
Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu ameahidi kutuma timu ya
wataalam kutoka Idara ya Magonjwa ya Mlipuko ili kuja kushirikiana na
timu ya Mkoa ili kufanya tathmini ili kuweza kuepusha magonjwa ya
mlipuko hasa katika kipindi hichi ambacho mvua zimeanza kunyesha mkoani
humo.
Akiongea wakati akikabidhi
misaada kwa mkoa wa kagera Meja jenerali Mstaafu Salum Kijuu Waziri Ummy
amesema anatambua kipindi hiki cha mvua huwa ni tishio kwa magonjwa ya
mlipuko hivyo wizara itachukua hatua ya kutuma wataalam pamoja na kutoa
elimu ya jinsi ya kujikinga na magonjwa hayo.
“Nafahamu tuko kwenye kipindi cha
mvua nyingi ambacho mara nyingi magonjwa ya mlipuko ikiwemo
kipindupindu huibuka, hivyo kabla ya hayo kutokea kama tahadhari sisi
kama wizara tutatuma wataalam kuja kufanya tathmini na kutoa elimu ya
namna ya kujikinga” Alisema Waziri Ummy.
Aidha Waziri Ummy amekabidhi
misaada ya Dawa na Vifaa vyenye thamani ya shilingi milioni 30
vilivyotolewa na Bohari kuu ya Dawa (MSD) kwa mkuu wa mkoa wa kagera
Meja jenerali Mstaafu Salum Kijuu kwa ajili ya kusaidia waathirika wa
tetemeko mkoani humo.
Pia Waziri Ummy amekabidhi
mashuka 250 yaliyotolewa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kwa
ajili ya Hospitali, Vituo vya Afya na Zahanati mkoani kagera.
Akiwa katika ziara kutembelea
maeneo yaliyoathiriwa na tetemeko la ardhi Waziri Ummy amewataka
watumishi katika sekta ya afya mkoani humo kuweka mkakati wa kuweka
mazingira safi kwenye maeneo yote yaliyoathiriwa na tetemeko
Wakati huo huo Waziri Ummy
ametembelea Kituo cha kulea wazee na watu wasiojiweza cha Kiilima
kilichopo katika Halmashauri ya Bukoba na kuagiza wazee hao kupatiwa
chakula cha milo mitatu ili kulinda afya zao.
Akizungumza baada ya kupokea
misaada hiyo mkuu wa mkoa wa kagera Meja jenerali Mstaafu Salum Kijuu
amewaomba wadau wengine kuendelea kutoa misaada kwa ajili ya kurejesha
hali baada ya maafa kutokea.
0 maoni:
Chapisha Maoni