Posted by Esta Malibiche on Oct7.2016 in KITAIFA
Waziri wa Mambo ya Katiba na Sheria Mh.
Harrison Mwakyembe akiongea na wanahabari (hawapo pichani) kuhusu mauaji
ya wataalamu wa utafiti yaliyotokea hivi karibuni mjini Dodoma, kulia
ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Profesa Sifuni Mchome na kushoto ni Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw. Amon Mpanju. (Picha na Benjamin Sawe-
Maelezo).
Waziri wa Mambo ya Katiba na Sheria Mh.
Harrison Mwakyembe akiongea na wanahabari (hawapo pichani) kuhusu mauaji
ya wataalamu wa utafiti yaliyotokea hivi karibuni mjini Dodoma, kulia
ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Profesa Sifuni Mchome na kushoto ni Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw. Amon Mpanju. (Picha na Benjamin Sawe-
Maelezo).
Na Beatrice Lyimo- MAELEZO
SERIKALI imesema itahakikisha kuwa
wahusika wa mauaji ya Watafiti mkoani Dodoma wanakamatwa na kufikishwa
mahakamani ili waweze kujibu mashtaka yanayowakabili.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es
salaam na Waziri ya Mambo ya Katiba na Sheria Dkt. Harrison Mwakyembe
wakati wa mkutano na waandishi wa habari juu ya mauaji ya Wataalamu hao
yaliyotokea wilayani Chamwino.
Amesema kuwa Serikali imesikitishwa na
hatua iliyochukuliwa na baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Iringa Mvumi
wilayani Chamwino kuwaua watafiti hao ambao walikuwa kazini.
Kufuatia hali hiyo amewaagiza Mkurugenzi
wa Mashtaka (DPP) kushirikiana na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI)
katika kufanya upelelezi wa mauaji ya wataalamu hao ili wahusika waweze
kufikishwa vyombo vya usalama haraka na haki iweze kutendeka.
Amesema kuwa ushirikiano huo utasaidia
kuimarisha upepelezi ambao utawezesha uandaaji wa mashtaka ili wahusika
wote waweze kufikishwa Mahakamani kwa ajili ya kujibu mashtaka
yanayowakabili.
“Wizara inawataka Mkurugenzi wa Mashtaka
DPP ajihusishe kikamilifu na upelelezi wa kesi hii ya mauaji ya
watafiti kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai DCI kwa
mujibu wa Sheria ya Huduma ya Uendeshaji wa Mashtaka” alifafanua Dkt.
Mwakyembe.
Ameongeza kuwa ili kukomesha wimbi la
wananchi kuchukua sheria mkononi, Wizara itachukua hatua kali
kuhakikisha waliohusika kwa namna moja ama nyingine kwa kushawishi,
kuhamasisha au kuchochea, kupanga, kushambulia kwa mapanga na kushiriki
kuchoma moto gari wanafikishwa mahakamani ili Sheria ichukue mkondo
wake.
Katika hatua nyingine, Waziri Mwakyembe
amewataka baadhi ya waandishi wa habari kubadilisha mfumo wa kutoa
taarifa za matukio zinazochochea uvunjifu wa amani kama vile kuandika
kuwa “wananchi wenye hasira kali” maneno ya aina hii hushawishi wengine
kufanya hivyo kwa kisingizio cha hasira.
Mbali na hayo Waziri huyo amevitaka
vyombo vya dola kuchukua hatua za kisheria kwa wote waliohusika na
vitendo vya kuchukua sheria mkononi ikiwemo kuwafikisha mahakamani.
0 maoni:
Chapisha Maoni