Posted by Esta Malibiche on Oct4.2016 in SIASA
Na Is-haka Omar, Zanzibar.
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM)
Zanzibar kimewasihi viongozi wa ngazi mbali mbali katika Wilaya ya
Kaskazini “B” kufanya vikao halali vya mara kwa mara ili kuibua na
kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu changamoto zinazowakabili wanachama na
wananchi kwa ujumla.
Nasaha hizo zimetolewa na Katibu
wa Kamati Maalum wa NEC, Idara ya Itikadi na uenezi CCM Zanzibar Waride
Bakar Jabu wakati akizungumza na wafuasi wa Chama hicho katika Matawi
ya CCM Boma Kiwengwa na Kinduni Mahonda katika mwendelezo wa ziara ya
kuimarisha chama ndani ya Wilaya hiyo.
Alisema vikao halali vya kikatiba
ndani ya Chama hicho ndio jukwaa rasmi la kujadiliana, kushauriana na
kufanya maamuzi sahihi ya kulinda na kuimarisha uhai wa CCM .
Waride alifafanua kwamba
kutokuwepo na vikao kwa baadhi ya ngazi za kiutendaji kunakwamisha
utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 20-15/2020 kwa baadhi ya maeneo
nchini.
“Sio vizuri mambo yanayohusu
Chama chetu yakajadiliwa nje ya vikao halali wakati sehemu rasmi za
kufanya hivyo zipo na kama kuna jambo la msingi hakuna anayezuiwa
kujenga hoja kupitia vikao, na tukifanya kinyume na hivyo tutatengeneza
fitna na migogoro isiyokuwa ya lazima.
Pia kupitia vikao mtaweza kuwa na
hoja ya pamoja ya kujibu baadhi ya njama na Propaganda zinazofanywa na
wapinzani katika maeneo yenu”,. Alisisitiza Waride na kuongeza kwamba
CCM itaendelea kuwa kinara wa siasa za maendeleo na haki endapo kila
kiongozi atatekeleza wajibu wake kulingana na majukumu aliyopewa
kikatiba.
Alifafanua kwamba Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Chama wametekeleza miradi
mbali mbali ya maendeleo nchini lakini imekuwa haijulikani kwa baadhi ya
wananchi na viongozi kutokana na kutokuwepo na kutokuwepo na mfumo
mzuri wa kupeana taarifa kupitia vikao.
Alisema chama hicho kitahakikisha
ahadi mbali mbali zilizoahidiwa katika Uchaguzi Mkuu uliopita
zinatekelezwa kabla ya mwaka 2020, ili kila mwananchi aweze kunufaika na
fursa zinazotokana na matunda ya Chama hicho.
Katibu huyo aliahidi kuchukua
hatua za makusudi kwa kuishawishi serika kuendelea kutafuta wawekezaji
wenye nia ya kuwekeza katika sekta za Kilimo, Uvuvi na Utalii ili
wananchi hasa wanaoishi vijijini waweze kupata ajira na kuongeza kipato
chao.
Kupitia vikao hivyo, Waride
aliwakumbusha wananchi umuhimu wa kulinda amani na utulivu wa nchi
pamoja na kushirikiana na viongozi wao wa majimbo na serikali katika
harakati kukuza uchumi wa Zanzibar.
Akijibu baadhi ya hoja za
wanachama wa Chama hicho, Katibu wa Kamati Maalum, Idara ya
Organazesheni ya CCM Zanzibar, Haji Mkema aliwataka Wazazi na Walezi wa
CCM ndani ya Wilaya hiyo kuwarithisha Vijana historia na Itikadi halisi
za CCM ili wawe waumini wa kweli wa Chama hicho.
Alisisitiza umuhimu wa wanachama
wa chama hicho kutumia fursa zilizowazunguka ndani ya Wilaya hiyo
zikiwemo Utalii na kilimo kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira huku
wakisubiri juhudi zinazofanywa na serikali kumaliza tatizo hilo.
Aliwambia na kuwataka vijana wa
Chama hicho kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kuwa mfano mwema wa
kuigwa katika jamii kwani wao ndio warithi wa viongozi wanaostaafu
utumishi ndani ya chama hicho.
Wakizungumza wanachama hao,
walikiomba chama kuwachukulia hatua za kinidhamu baadhi ya viongozi
wanaofanya kazi za CCM chini ya kiwango ili kuongeza kasi ya utendaji
ndani ya Wilaya hiyo.
Waliwakumbusha Viongozi wa ngazi
mbali mbali kutoa taarifa sahihi kwa wanachama wao juu ya fursa na
mambo yanayogusa moja kwa moja uimarishaji wea Chama ili yajulikane kwa
wanachama kwa lengo la kuepusha migogo na makundi yasiyokuwa ya lazima.
0 maoni:
Chapisha Maoni