Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amemuagiza
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA),
kupunguza idadi ya vikao vya baraza visivyo na ulazima ili kuondokana na
matumizi mabaya ya fedha na badala yake fedha hizo zielekezwe kwenye
uendelezaji wa miundombinu ya bandari za maziwa.
Ametoa
agizo hilo mara baada ya kukagua shughuli za utendaji wa bandari ya
Kasanga iliyopo mkoani Rukwa inayohudumia mkoa wa Kigoma, nchi ya
Burundi na Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo (DRC) ambapo amebaini
mapungufu ya kiutendaji ikiwemo malipo yasiyotumia njia za kielektroniki
na miundombinu isiyo rafiki katika kukidhi ushindani wa kibiashara
katika bandari hiyo.
Waziri
Mbarawa ameitaka TPA kuweka mfumo wa uendeshaji vikao kwa njia ya
kieletroniki (video conference) kwa lengo la kudhibiti matumizi ya fedha
nyingi zilizokuwa zikitumika katika uendeshaji wa vikao hivyo.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akitoa
maelekezo kwa Meneja wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Mkoa wa Rukwa
Arch. Deocles Alphonce wakati alipokagua ujenzi wa ofisi za Bonde la
Ziwa Rukwa na Maabara zake zilizopo Sumbawanga Mjini.
“Nataka
TPA muanze kutumia video Conference katika vikao vyenu ili fedha
zilizokuwa zikitumika zifanyie kazi nyingine za maendeleo ya Taifa”,
amesema Waziri Prof. Mbarawa.
Ameongeza
kuwa TPA imekuwa na wajibu mkubwa wa kuchangia pato la Taifa kupitia
huduma za upakiaji na upakuaji wa mizigo hivyo wanapaswa kuanza kutumia
mfumo wa kielekroniki katika ukusanyaji wa mapato katika bandari zote
nchini ili kudhibiti upotevu wa mapato.
“Tukianzisha
mfumo wa kielekroniki katika bandari hii tutakuwa na uwezo wa
kufuatilia mapato yanayopatikana katika utoaji wa huduma na kujua kama
malengo yamefikiwa”, amesema Prof. Mbarawa.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akikagua
nondo zilizosukwa kwa ajili ya ujenzi wa Daraja la Kalambo lililopo
katika barabara ya Sumbawanga-Matai-Kasanga yenye urefu wa KM 112,
Mkoani Rukwa.
Katika
Hatua nyingine Profesa Mbarawa amekagua barabara ya
Sumbawanga-Matai-Kasanga Port yenye urefu wa KM 112 inayojengwa kwa
kiwango cha Lami na kumtaka Mkandarasi wa barabara hiyo China Railway 15
Bureau Group Corporation kukamilisha ujenzi huo ifikapo Julai mwakani.
Amesema
kukamilika kwa barabara hiyo kutaunganisha mji wa Sumbawanga na
Bandari ya Kasanga na hivyo kurahisisha shughuli za usafirishaji wa
abiria na mizigo kutoka bandarini hapo na hivyo kuwa kichocheo cha
ukuaji wa uchumi katika Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.
“Kukamilika
kwa barabara hii kutawawezesha wananchi kusafirisha bidhaa zao, kutoka
sehemu moja hadi nyingine na hivyo kukuza uchumi wao na kuongeza pato la
Taifa”, amesisitiza Prof. Mbarawa.
Aidha
Waziri Mbarawa amemuhimiza Mkandarasi huyo kujenga barabara hiyo kwa
viwango vilivyopo katika mkataba na kuzingatia thamani ya fedha katika
ujenzi huo ili kuwezesha barabara hiyo kudumu kwa muda mrefu.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akiendelea na
ukaguzi wa ujenzi wa barabara ya Sumbawanga-Matai-Kasanga yenye urefu
wa KM 112, Mkoani Rukwa.
Naye
Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini, Mkoa wa Rukwa Eng. Masuka Mkina
amesema kuwa ujenzi wa barabara hiyo umekamilika kwa asilimia 62 ambapo
kukamilika kwa ujenzi huo utatagharimu kiasi cha zaidi ya shilingi
Bilioni 133.
“Mpaka
sasa Mkandarasi ameweza kukamilisha kujenga makalvati makubwa 11 kati
ya 13, na makalvati ya kawaida 169 kati ya 241”, amesema Eng Mkina.
Waziri
Prof. Mbarawa yupo katika ziara ya kukagua miradi ya miundombinu na
kuangalia utendaji kazi wa taasisi zilizopo katika Mkoa wa Rukwa.
Mhandisi
Mshauri wa Kampuni ya Nicholas O’Dwyer Eng. Farley Vicente akitoa
taarifa kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame
Mbarawa kuhusu ujenzi wa barabara ya Sumbawanga-Matai-Kasanga yenye
urefu wa KM 112, Mkoani Rukwa.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akitoa
maelekezo kwa Mkandarasi wa China Railway 15 Bureau Group Corporation
kutoka China Zhang Tonggang (mwenye sweta nyekundu) inayojenga barabara
ya Sumbawanga-Matai-Kasanga yenye urefu wa KM 112 kwa kiwango cha lami,
Mkoani Rukwa.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akihakiki
taarifa za mapato katika Bandari ya Kasanga iliyopo Mkoani Rukwa.
Katikati ni Msimamizi wa bandari hiyo Bw. Seleman Kalugendo.
Meneja
wa Shirika la Posta Tanzania Bi. Zahara Suleiman akifafanua jambo kwa
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa kuhusu
huduma ya kutuma na kupokea Vifurushi wakati Waziri alipotembelea
ofisini hapo.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akitoa
Maelekezo kwa Meneja wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) nyanda za juu
kusini Bw. Peter Kaguru wakati alipotembelea ofisi hizo Mkoani Rukwa.
0 maoni:
Chapisha Maoni